Contents

Holy Bible

Swahili New Testament

New Testament

Matthew

Chapter 1

1Yesu Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake: 2Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake, 3Yuda alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami, 4Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni, 5Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese, 6naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa mke wa Uria). 7Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa, 8Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia, 9Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia, 10Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia, 11Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni. 12Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerobabeli, 13Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori, 14Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi, 15Eliudi alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo, 16Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo. 17Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo. 18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. 20Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao." 22Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: 23"Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi"). 24Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. 25Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.

Chapter 2

1Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, 2wakauliza, "Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu." 3Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. 4Basi akawaita pamoja makuhani wakuu wote na walimu wa Sheria, akawauliza, "Kristo atazaliwa wapi?" 5Nao wakamjibu, "Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika: 6`Ewe Bethlehemu katika nchi ya Yuda, kwa vyovyote wewe si mdogo kabisa kati ya viongozi wa Yuda; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli."` 7Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. 8Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, "Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende nikamwabudu." 9Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. 10Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. 11Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani na manemane. ic 12Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine. 13Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokwambia, maana Herode anakusudia kumwua huyu mtoto." 14Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. 15Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: "Nilimwita Mwanangu kutoka Misri." 16Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. 17Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia: 18"Sauti imesikika mjini Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki." 19Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa." 21Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: "Ataitwa Mnazare."

Chapter 3

1Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea: 2"Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia." 3Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."` 4Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 5Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, 6wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. 7Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja? 8Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli. 9Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, `Baba yetu ni Abrahamu!` Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. 10Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni. 11Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu. Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika." ic 13Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye. 14Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe." 15Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo Yohane akakubali. 16Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake. 17Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye."

Chapter 4

1Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi. 2Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. 3Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate." 4Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: `Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."` 5Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, 6akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: `Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."` 7Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: `Usimjaribu Bwana, Mungu wako."` 8Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, 9akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu." 10Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake."` 11Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia. 12Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya. 13Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zabuloni na Naftali, akakaa huko. 14Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya: 15"Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ng`ambo ya mto Yordani, Galilaya nchi ya watu wa Mataifa! 16Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!" 17Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, "Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia!" 18Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. 19Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. ic 21Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi Yesu akawaita, 22nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata. 23Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. 24Habari zake zikaenea katika mkoa wote wa Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. 25Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ng`ambo ya mto Yordani, walimfuata.

Chapter 5

1Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea, 2naye akaanza kuwafundisha: 3"Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao. 4Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa. 5Heri walio wapole, maana watairithi nchi. 6Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa. 7Heri walio na huruma, maana watahurumiwa. 8Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. 9Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu. 10Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao. 11"Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu. 13"Ninyi ni chumvi ya dunia! Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. 14"Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. 15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. 16Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni." 17"Msidhani ya kuwa nimekuja kutangua Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha. 18Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya Sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia. 19Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika Ufalme wa mbiguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika Ufalme wa mbinguni. 20Ndiyo maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa Mafarisayo na walimu wa Sheria, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni. 21"Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.` 22Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: `Pumbavu` atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu. 23Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe, 24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi ukatoe sadaka yako. 25"Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani, kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani. 26Kweli nakwambia, hutatoka humo mpaka umemaliza kulipa senti ya mwisho. 27"Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: `Usizini!` 28Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake. 29Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, ling`oe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu. 30Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali zaidi kupoteza kiungo kimoja cha mwili, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu. 31"Ilikwisha semwa pia: `Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka.` 32Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mtu akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. 33"Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.` 34Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; 35wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. 36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu. 38"Mmesikia kwamba ilisemwa: `Jicho kwa jicho, jino kwa jino.` 39Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili. 40Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. 41Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. 42Akuombaye mpe, na mtu akitaka kukukopa kitu usimnyime. 43"Mmesikia kwamba ilisemwa: `Mpende jirani yako na kumchukia adui yako.` 44Lakini mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu. 46Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda ninyi? Hakuna! Kwa maana hata watoza ushuru hufanya hivyo! 47Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo. 48Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Chapter 6

1"Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo. 2"Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. 3Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata rafiki yako asijue ufanyalo. 4Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. 5"Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. 6Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. 7"Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi. 8Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba. 9Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: `Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. 10Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. 11Utupe leo chakula chetu tunachohitaji. 12Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. 13Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu.`fa na utukufu, hata milele. Amina. 14"Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. 16"Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni hakika, hao wamekwisha pata tuzo lao. 17Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, 18ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza. 19"Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. 20Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. 21Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako. 22"Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. 23Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga ulioko ndani yako ni giza, basi, hilo ni giza la kutisha mno. 24"Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja. 25"Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi? 26Waangalieni ndege wa mwituni: hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyoye. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani kuliko hao? 27Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake? 28"Na kuhusu mavazi, ya nini kuwa na wasiwasi? Tazameni maua ya porini jinsi yanavyostawi. Hayafanyi kazi wala hayasokoti. 29Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. 30Ikiwa basi Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatafanya zaidi kwenu ninyi? Enyi watu wenye imani haba! 31"Basi, msiwe na wasiwasi: `Tutakula nini, tutakunywa nini, tutavaa nini!` 32Maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote. 33Bali, zingatieni kwanza Ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo mengine yote mtapewa kwa ziada. 34Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.

Chapter 7

1"Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; 2kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu. 3Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 4Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako`, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako? 5Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako. 6"Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga. 7"Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa. 8Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa. 9Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? 10Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? 11Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba. 12"Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. 13"Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. 14Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. 15"Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. 16Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! 17Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema. 19Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni. 20Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. ic 21"Si kila aniambiaye, `Bwana, Bwana,` ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: `Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.` 23Hapo nitawaambia: `Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.` 24"Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. 25Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba. 26"Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. 27Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa." 28Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake. 29Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.

Chapter 8

1Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata. 2Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia akisema, "Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!" 3Yesu akanyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka! Takasika." Mara huyo mtu akapona ukoma wake. 4Kisha Yesu akamwambia, "Sikiliza, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona." 5Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, ofisa mmoja Mroma alimwendea, akamsihi 6akisema, "Mheshimiwa, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana." 7Yesu akamwambia, "Nitakuja kumponya." 8Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. 9Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, `Nenda!` naye huenda; na mwingine, `Njoo!` naye huja; na mtumishi wangu, `Fanya kitu hiki!` naye hufanya." 10Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, "Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli aliye na imani kama hii. 11Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa mbinguni. 12Lakini wale ambao wangalipaswa kuwa katika Ufalme huo watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno." 13Kisha Yesu akamwambia huyo ofisa Mroma, "Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini." Na mtumishi wake akapona saa ileile. 14Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. 15Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. 16Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. 17Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: "Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, ameyachukua magonjwa yetu." 18Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng`ambo ya ziwa. 19Mwalimu mmoja wa Sheria akamwendea, akamwambia, "Mwalimu, mimi nitakufuata kokote uendako." 20Yesu akamjibu, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia." 21Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, "Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu." 22Lakini Yesu akamwambia, "Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao." 23Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. 24Ghafla, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu alikuwa amelala usingizi. 25Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, "Bwana, tuokoe, tunaangamia!" 26Yesu akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?" Basi, akainuka, akazikemea pepo na mawimbi; kukawa shwari kabisa. 27Watu wakashangaa, wakasema, "Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na mawimbi vinamtii!" 28Yesu alifika katika nchi ya Wagerasi,fb ng`ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita katika njia hiyo. 29Nao wakaanza kupiga kelele, "Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?" 30Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa. 31Basi, hao pepo wakamsihi, "Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale." 32Yesu akawaambia, "Haya, nendeni." Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa maji. 33Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa. 34Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.

Chapter 9

1Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake. 2Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako." 3Baadhi ya walimu wa Sheria wakaanza kufikiri, "Mtu huyu anamkufuru Mungu!" 4Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, "Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu? 5Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, `Umesamehewa dhambi zako`, au kusema, `Simama, utembee`? 6Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako." 7Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake. 8Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo. 9Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, "Nifuate." Naye Mathayo akainuka, akamfuata. 10Yesu alipokuwa nyumbanifc ameketi kula chakula, watoza ushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake. 11Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, "Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?" 12Yesu aliwasikia, akasema, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi. 13Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: `Nataka huruma, wala si dhabihu.` Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi." 14Kisha wanafunzi wa Yohane mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, "Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?" 15Yesu akawajibu, "Je, walioalikwa arusini wanaweza kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. 16"Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka. 17Wala hakuna mtu awekaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila divai mpya hutiwa katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama." 18Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, "Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali njoo umwekee mkono wako naye ataishi." 19Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata. 20Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. 21Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: "Nikigusa tu vazi lake, nitapona." 22Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, "Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya." Mama huyo akapona saa ileile. 23Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaofanya matanga, 24akasema, "Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu." Nao wakamcheka. 25Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama. 26Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote. 27Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, "Mwana wa Daudi, utuhurumie!" 28Yesu alipoingia nyumbani, vipofu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, "Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?" Nao wakamjibu, "Naam, Mheshimiwa." 29Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, "Na iwe kwenu kama mnavyoamini." 30Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: "Msimwambie mtu yeyote jambo hili." 31Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote. 32Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. 33Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, "Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!" 34Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, "Anawatoa pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya." 35Yesu alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila namna. 36Basi, alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa hoi na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji. 37Hapo akawaambia wanafunzi wake, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. 38Kwa hivyo mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake."

Chapter 10

1Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. 2Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; 3Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. 5Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: "Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa Wasamaria. 6Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. 7Mnapokwenda hubirini hivi: `Ufalme wa mbinguni umekaribia.` 8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. 9Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. 10Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. 11"Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 12Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. 13Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu itawarudia ninyi. 14Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. 15Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora. 16"Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. 17Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. 18Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa. 19Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. 20Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. 21"Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 22Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa. 23"Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika. 24"Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. 25Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi? 26"Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. 27Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong`onezwa, litangazeni hadharani. 28Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. 29Shomoro wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. 30Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31Kwa hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi. ic 32"Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 33Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 34"Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. 36Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. 37"Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. 39Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. 40"Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma. 41Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. 42Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake."

Chapter 11

1Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. 2Yohane mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, 3wamwulize: "Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?" 4Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: 5vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. 6Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami." 7Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: "Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? 8Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. 9Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. 10"Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: `Tazama, hapa namtuma mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako.` 11Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. 12Tangu wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. 13Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi. 14Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Eliya ambaye angekuja. 15Mwenye masikio na asikie! 16"Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: 17`Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!` 18Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: `Amepagawa na pepo.` 19Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: `Mtazameni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wahalifu!` Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake." 20Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya: 21"Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu. 22Hata hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na Sidoni. 23Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. 24Lakini nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko kwako wewe." 25Wakati huo Yesu alisema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo. 26Naam Baba, ndivyo ilivyokupendeza. 27"Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha. 28Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. 30Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."

Chapter 12

1Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. 2Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, "Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato." 3Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. 5Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? 6Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuufd kuliko Hekalu. 7Kama tu mngejua maana ya maneno haya: `Nataka huruma wala si dhabihu`, hamngewahukumu watu wasio na hatia. 8Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato." 9Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. 10Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, "Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?" Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. 11Lakini Yesu akawaambia, "Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? 12Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato." 13Kisha akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. 14Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. 15Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, 16akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, 17ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: 18"Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. 19Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. 20Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. 21Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini." 22Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona. 23Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, "Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?" 24Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, "Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo." 25Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. 26Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? 27Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi. 28Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. 29"Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake. 30"Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. 31Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. 32Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. 33"Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. 34Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. 35Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. 36"Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. 37Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia." 38Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako." 39Naye akawajibu, "Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona. 40Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha. 41Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona! 42Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuufe kuliko Solomoni. 43"Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate. 44Hapo hujisemea: `Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.` Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa, 45huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu." 46Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye. 47Basi, mtu mmoja akamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe." 48Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, "Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?" 49Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, "Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu! 50Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu."

Chapter 13

1Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa. 2Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashua, akaketi. Hao watu walisimama kwenye ukingo wa ziwa, 3naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. 4Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. 5Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. 6Jua lilipochomoza, zilichomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. 7Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga. 8Lakini nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: nyingine punje mia moja, nyingine sitini na nyingine thelathini. 9Mwenye masikio na asikie!" 10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, "Kwa nini unasema na watu kwa mifano?" 11Yesu akawajibu, "Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. 12Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 13Ndiyo maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. 14Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: `Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. 15Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao. wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.` 16"Lakini heri yenu ninyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. 17Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie. 18"Basi, ninyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi. 19Yeyote asikiaye ujumbe wa ufalme bila kuuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. 20Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye ujumbe huo na mara akaupokea kwa furaha. 21Lakini haumwingii na kuwa na mizizi ndani yake; huendelea kuuzingatia ujumbe huo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya ujumbe huo, anakata tamaa mara. 22Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye huo ujumbe, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali huusonga ujumbe huo, naye hazai matunda. 23Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu ausikiaye ujumbe huo na kuuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini." 24Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. 26Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. 27Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, `Mheshimiwa, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?` 28Yeye akawajibu, `Adui ndiye aliyefanya hivyo.` Basi, watumishi wake wakamwuliza, `Je, unataka twende tukayang`oe` 29Naye akawajibu, `La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang`oa na ngano pia. 30Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu."` 31Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake. 32Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikishaota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, na ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake." 33Yesu akawaambia mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga pishi tatu, hata unga wote ukaumuka." 34Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano, 35ili jambo lililonenwa na nabii litimie: "Nitasema kwa mifano; nitawaambia mambo yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu." 36Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani." 37Yesu akawaambia, "Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. 38Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao Ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. 39Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. 40Kama vile magugu yanavyokusanywa kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; 41Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika Ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, 42na kuwatupa katika tanuru ya moto, na huko watalia na kusaga meno. 43Kisha, wale wema watang`ara kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Sikieni basi, kama mna masikio! 44"Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile. 45"Tena, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. 46Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile. 47"Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. 48Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. 49Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, 50na kuwatupa hao wabaya katika tanuru ya moto. Huko watalia na kusaga meno." 51Yesu akawauliza, "Je, mmeelewa mambo haya yote?" Wakamjibu, "Naam." 52Naye akawaambia, "Hivyo basi, kila mwalimu wa Sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale." 53Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, 54akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi hata wakashangaa, wakasema, "Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? 55Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?" 57Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, "Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!" 58Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.

Chapter 14

1Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. 2Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake." 3Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni 4kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!" 5Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. 6Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, 7hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. 8Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji." 9Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. 10Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. 11Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. 12Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu. 13Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. 14Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. 15Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula." 16Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula." 17Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili." 18Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa." 19Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. 20Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto. 22Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng`ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu. 23Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, 24na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. 25Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. 26Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu. 27Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!" 28Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako." 29Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. 30Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!" 31Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?" 32Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. 33Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu." 34Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. 35Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, 36wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.

Chapter 15

1Kisha Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza, 2"Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula!" 3Yesu akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali Sheria ya Mungu? 4Mungu amesema: `Waheshimu baba yako na mama yako,` na `Anayemkashifu baba yake au mama yake, lazima auawe`. 5Lakini ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema: `Kitu hiki nimemtolea Mungu,` 6basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe. 7Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu: 8`Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. 9Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu."` 10Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe! 11Kitu kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi." 12Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?" 13Lakini yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda, utang`olewa. 14Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni." 15Petro akadakia, "Tufafanulie huo mfano." 16Yesu akasema, "Hata nyinyi hamwelewi? 17Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa nje chooni? 18Lakini yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. 19Maana moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa. 20Hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu najisi." 21Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. 22Basi, mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo." 23Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele." 24Yesu akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo." 25Hapo huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa, nisaidie." 26Yesu akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." 27Huyo mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao." 28Hapo Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake akapona tangu saa hiyo wakati huohuo. 29Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. 30Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. 31Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa Israeli. 32Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani." 33Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?" 34Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache." 35Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. 36Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. 37Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba. 38Hao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.

Chapter 16

1Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye ishara itokayo mbinguni. 2Lakini Yesu akawajibu, "Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: `Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!` 3Na alfajiri mwasema: `Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!` Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui. 4Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote isipokuwa tu ile ya Yona." Basi, akawaacha, akaenda zake. 5Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate. 6Yesu akawaambia, "Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!" 7Lakini wao wakawa wanajadiliana: "Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate." 8Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? 9Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo? 10Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki? 11Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!" 12Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo. 13Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?" 14Wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii." 15Yesu akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?" 16Simoni Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai." 17Yesu akasema, "Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni. 18Nami nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwambaff huu nitalijenga kanisa langu; wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda. 19Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni." 20Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo. 21Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: "Ni lazima mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu nitafufuliwa." 22Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: "Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!" 23Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, "Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!" 24Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; 26lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake? 27Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake. 28Kweli nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika Ufalme wake."

Chapter 17

1Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. 2Huko, wakiwa wanamtazama, akageuka sura, uso wake ukang`aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama nuru. 3Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. 4Hapo Petro akamwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri sana kwamba tupo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya." 5Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni." 6Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. 7Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, "Simameni, msiogope!" 8Walipoinua macho yao hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake. 9Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: "Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu." 10Kisha wanafunzi wakamwuliza, "Mbona walimu wa Sheria wanasema ati ni lazima kwanza Eliya aje?" 11Yesu akawajibu, "Kweli, Eliya atakuja kutayarisha mambo yote. 12Lakini nawaambieni, Eliya amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao." 13Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane mbatizaji. 14Walipojiunga tena na ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti, 15akasema, "Mheshimiwa, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya." 17Yesu akajibu, "Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia ninyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto." 18Basi, Yesu akamkemea huyo pepo, naye akamtoka, na yule mtoto akapona wakati huohuo. 19Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha, wakamwuliza, "Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?" 20Yesu akawajibu, "Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, hata iwe ndogo kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: `Toka hapa uende pale,` nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu."fg kuondolewa ila kwa sala na kufunga." 21missing 22Walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu aliwaambia, "Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu. 23Watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa." Wanafunzi wakahuzunika mno. 24Walipofika Kafarnaumu watu wenye kukusanya fedha ya zaka ya Hekalu walimwendea Petro, wakamwuliza, "Je, mwalimu wenu hulipa fedha ya zaka?" 25Petro akajibu, "Naam, hulipa." Basi, Petro alipoingia ndani ya nyumba, kabla hata hajasema neno, Yesu akamwuliza, "Simoni, wewe unaonaje? Wafalme wa dunia hukusanya ushuru au kodi kutoka kwa kina nani? Kutoka kwa wananchi ama kutoka kwa wageni?" 26Petro akajibu, "Kutoka kwa wageni." Yesu akamwambia, "Haya basi, wananchi hawahusiki. 27Lakini kusudi tusiwakwaze, nenda ziwani ukatupe ndoana; chukua samaki wa kwanza atakayenaswa, fungua kinywa chake, na ndani utakuta fedha taslimu ya zaka. Ichukue ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako."

Chapter 18

1Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, "Ni nani aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni?" 2Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao, 3kisha akasema, "Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni. 4Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika Ufalme wa mbinguni. 5Yeyote anayemkaribisha mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananikaribisha mimi. 6"Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. 7Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. 8"Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. 9Na kama jicho lako likikukosesha, ling`oe na kulitupa mbali nawe. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili. 10"Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.fh 11missing 12Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, na huenda kumtafuta yule aliyepotea. 13Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee. 15"Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa ninyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. 16Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe. 17Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watoza ushuru. 18"Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni. 19Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo. 20Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao." 21Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, "Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?" 22Yesu akamjibu, "Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba. 23Ndiyo maana Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake. 24Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta elfu kumi. 25Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru wauzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. 26Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, `Unisubiri nami nitakulipa deni lote.` 27Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake. 28"Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha denari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akisema, `Lipa deni lako!` 29Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, `Unisubiri nami nitalipa deni langu lote.` 30Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni. 31"Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia. 32Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, `Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. 33Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?` 34"Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote. 35Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote."

Chapter 19

1Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda katika mkoa wa Yudea, ng`ambo ya mto Yordani. 2Watu wengi walimfuata huko, naye akawaponya. 3Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, "Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?" 4Yesu akawajibu, "Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, 5na akasema: `Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?` 6Kwa hiyo wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe." 7Lakini wao wakamwuliza, "Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?" 8Yesu akawajibu, "Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 9Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini." 10Wanafunzi wake wakamwambia, "Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa." 11Yesu akawaambia, "Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu. 12Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee." 13Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea. 14Yesu akasema, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana Ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa." 15Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo. 16Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, "Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uzima wa milele?" 17Yesu akamwambia, "Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uzima, shika amri." 18Yule mtu akamwuliza, "Amri zipi?" Yesu akasema, "Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, 19waheshimu baba yako na mama yako; na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe." 20Huyo kijana akamwambia, "Hayo yote nimeyazingatia tangu utoto wangu; sasa nifanye nini zaidi?" 21Yesu akamwambia, "Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako uwape maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate." 22Huyo kijana aliposikia hayo, alienda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi. 23Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kweli nawaambieni, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni. 24Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni." 25Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa, wakamwuliza, "Ni nani basi, awezaye kuokoka?" 26Yesu akawatazama, akasema, "Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana." 27Kisha Petro akasema, "Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?" 28Yesu akawaambia, "Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake katika ulimwengu mpya, ninyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uzima wa milele. 30Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Chapter 20

1"Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. 2Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. 3Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. 4Akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.` 5Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. 6Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, `Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?` 7Wakamjibu: `Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.` Yeye akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.` 8"Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, `Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.` 9Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja. 10Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja. 11Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung`unikia yule bwana. 12Wakasema, `Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?` 13"Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, `Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja? 14Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. 15Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"` 16Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho." 17Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia, 18"Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe. 19Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa." 20Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu. 21Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto." 22Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza." 23Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu." 24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili. 25Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao. 26Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; 27na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. 28Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi." 29Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. 30Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!" 31Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!" 32Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka niwafanyie nini?" 33Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe." 34Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.

Chapter 21

1Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 2akawaambia, "Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. 3Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, `Bwana anawahitaji,` naye atawaachieni mara." 4Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie: 5"Uambieni mji wa Sioni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwana punda, mtoto wa punda." 6Hivyo, wale wanafunzi walienda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. 7Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake. 8Umati mkubwa wa watu ukatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. 9Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaaza sauti: "Hosana Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Hosana Mungu juu mbinguni!" 10Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, "Huyu ni nani?" 11Watu katika ule umati wakasema, "Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti katika mkoa wa Galilaya." 12Basi, Yesu akaingia Hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya Hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. 13Akawaambia, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: `Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.` Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi." 14Vipofu na vilema walimwendea huko Hekaluni, naye Yesu akawaponya. 15Basi, makuhani wakuu na walimu wa Sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaaza sauti zao Hekaluni wakisema: "Sifa kwa Mwana wa Daudi," wakakasirika. 16Hivyo wakamwambia, "Je, husikii wanachosema?" Yesu akawajibu, "Naam, nasikia! Je hamjasoma Maandiko haya Matakatifu? `Kwa vinywa vya watoto wadogo na wanyonyao unajipatia sifa kamilifu."` 17Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko. 18Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. 19Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauma chochote ila majani matupu. Basi akauambia, "Usizae tena matunda milele!" Papo hapo huo mtini ukanyauka. 20Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, "Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?" 21Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: `Ng`oka ukajitose baharini,` itafanyika hivyo. 22Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata." 23Yesu aliingia Hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, "Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?" 24Yesu akawajibu, "Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. 25Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?" Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: "Tukisema, `Yalitoka mbinguni`, atatuuliza, `Basi, mbona hamkumsadiki?` 26Na tukisema, `Yalitoka kwa watu,` tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii." 27Basi, wakamjibu, "Hatujui!" Naye Yesu akawaambia, "Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. 28"Ninyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, `Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.` 29Yule kijana akamwambia, `Sitaki!` Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi. 30Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, `Naam baba!` Lakini hakwenda kazini. 31Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?" Wakamjibu, "Yule mtoto wa kwanza." Basi, Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, watoza ushuru na waasherati wataingia katika Ufalme wa Mungu kabla yenu. 32Maana Yohane alikuja kwenu akawaonyesha njia njema ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watoza ushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote ninyi hamkubadili mioyo yenu, na hamkusadiki." 33Yesu akasema, "Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda nchi ya mbali. 34Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. 35Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamwua na mwingine wakampiga mawe. 36Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. 37Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: `Watamheshimu mwanangu.` 38Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: `Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!` 39Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamwua. 40"Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?" 41Wao wakamjibu, "Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wa mavuno." 42Hapo Yesu akawaambia, "Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? `Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!` 43"Kwa hiyo nawaambieni, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake."fi likimwangukia mtu yeyote, litamponda." 44missing 45Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao. 46Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.

Chapter 22

1Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: 1Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, 2"Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 2"Walimu wa Sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua Sheria ya Mose. 3Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje arusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. 3Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri. 4Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, `Waambieni wale walioalikwa: karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ng`ombe wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari, njoni arusini.` 4Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba. 5Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, 5Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya Sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao. 6na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. 6Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi. 7Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. 7Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: `Mwalimu.` 8Kisha akawaambia watumishi wake: `Karamu ya arusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. 8Lakini ninyi msiitwe kamwe `Mwalimu,` maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu. 9Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje arusini.` 9Wala msimwite mtu yeyote `Baba` hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni. 10Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya arusi ikajaa wageni. 10Wala msiitwe `Viongozi,` maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo. 11"Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya arusi. 11Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu. 12Mfalme akamwuliza, `Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la arusi?` Lakini yeye akakaa kimya. 12Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa. 13Hapo mfalme akawaambia watumishi, `Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno."` 13"Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa Ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Ninyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie.fj wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali. 14Yesu akamaliza kwa kusema, "Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa." 14missing 15Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. 15"Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko ninyi wenyewe. 16Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. 16"Ole wenu viongozi vipofu! Ninyi mwasema ati mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, kiapo hicho kinamshika. 17Haya, twambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa Kaisari?" 17Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: dhahabu au Hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? 18Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, "Enyi 18Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika. 19Nionyesheni fedha ya kulipia kodi." Nao wakamtolea sarafu ya fedha. sarafu ya fedha. 19Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu? 20Basi, Yesu akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?" 20Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake. 21Wakamjibu, "Ni vya Kaisari." Hapo Yesu akawaambia, "Basi, mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari, na Mungu yaliyo yake Mungu." 21Na anayeapa kwa Hekalu ameapa kwa hilo Hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake. 22Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao. 22Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake. 23Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. Hao ndio wale wasemao kwamba wafu hawafufuki. 23Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu zaka, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya Sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndiyo hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine. 24Basi, wakamwambia, "Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, amzalie ndugu yake watoto. 24Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! ic 25Sasa, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. 25"Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyang`anyi na uchoyo. 26Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. 26Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia. 27Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. 27"Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu. 28Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana Wote saba walimwoa." 28Hali kadhalika ninyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu. 29Yesu akawajibu, "Kweli mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu! 29"Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema. 30Maana wafu watakapofufuliwa hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika mbinguni. 30Mwasema: `Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!` 31Lakini kuhusu suala la wafu kufufuka, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? 31Hivyo mnathibitisha ninyi wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa watu waliowaua manabii. 32Aliwaambia, `Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!` Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai." 32Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza! 33Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake. 33Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu? 34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. 34Ndiyo maana mimi ninawapelekea ninyi manabii, watu wenye hekima na walimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji. 35Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, 35Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kuuawa kwa Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka kuuawa kwa Zakariya, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua Hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu. 36"Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika Sheria ya Mose?" 36Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya. 37Yesu akamjibu, "`Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote.` 37"Yerusalemu, Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. 38Hii ndiyo amri kuu ya kwanza. 38Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame. 39Ya pili inafanana na hiyo: `Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.` 39Nakwambia kweli, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: `Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."` ic 40Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili." 41Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, 42"Ninyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?" Wakamjibu, "Wa Daudi." 43Yesu akawaambia, "Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema: 44`Bwana alimwambia Bwana wangu: keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.` 45Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo `Bwana,` anawezaje kuwa mwanawe?" 46Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.

Chapter 24

1Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu. 2Yesu akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa." 3Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?" 4Yesu akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. 5Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye Kristo,` nao watawapotosha watu wengi. 6Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. 7Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. 8Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. 9"Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu. 10Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. 11Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. 12Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. 13Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka. 14Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote. 15"Basi, mtakapoona `Chukizo Haribifu` lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), 16hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. 17Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. 18Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. 19Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! 20Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! 21Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. 22Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. 23"Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: `Kristo yuko hapa` au `Yuko pale,` msimsadiki. 24Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. 25Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati. 26Basi, wakiwaambieni, `Tazameni, yuko jangwani,` msiende huko; au, `Tazameni, amejificha ndani,` msisadiki; 27maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. 28Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. 29"Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. 30Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. 31Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu. 32"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.fk 34Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. 35Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 36"Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye. 37Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. 38Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina. 39Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja. 40Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 42Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu. 43Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. 44Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia." 45Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake? 46Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo. 47Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote. 48Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: `Bwana wangu anakawia kurudi,` 49kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi, 50bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua. 51Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Chapter 25

1"Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi. 2Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. 3Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta. 4Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao. 5Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala. 6Usiku wa manane kukawa na kelele: `Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.` 7Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao. 8Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: `Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.` 9Lakini wale wenye busara wakawaambia, `Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!` 10Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa. 11Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: `Bwana, bwana, tufungulie!` 12Lakini yeye akawajibu, `Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."` 13Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa. 14"Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng`ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake. 15Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri. 16Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano. 17Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili. 18Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake. 19"Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake. 20Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, `Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.` 21Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.` 22"Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, `Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.` 23Bwana wake akamwambia, `Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.` 24"Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, `Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. 25Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.` 26"Bwana wake akamwambia, `Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya. 27Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake! 28Basi, mnyang`anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi. 29Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 30Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.` 31"Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu, 32na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. 33Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto. 34"Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, `Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; 36nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.` 37Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme `Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji? 38Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika? 39Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?` 40Mfalme atawajibu, `Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.` 41"Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, `Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake. 42Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji. 43Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.` 44"Hapo nao watajibu, `Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?` 45Naye atawajibu, `Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.` 46Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele."

Chapter 26

1Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, 2"Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe." 3Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, Kuhani Mkuu. 4Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue. 5Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu. 6Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma, 7mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani. 8Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, "Ya nini hasara hii? 9Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha." 10Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema. 11Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. 12Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. 13Nawaambieni kweli, popote ambapo hii Habari Njema itahubiriwa ulimwenguni, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye." 14Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu, 15akawaambia, "Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?" Wakamhesabia sarafu thelathini za fedha; 16na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti. 17Siku ya kwanza kabla ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, "Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?" 18Yeye akawajibu, "Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie: `Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu."` 19Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka. 20Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 21Walipokuwa wakila, Yesu akasema, "Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti." 22Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, "Bwana! Je, ni mimi?" 23Yesu akajibu, "Atakayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.fm 24Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa." 25Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, "Mwalimu! Je, ni mimi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema." 26Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni mle; huu ni mwili wangu." 27Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa akisema, "Nyweni nyote; 28maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano,fn damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi. 29Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu." 30Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. 31Kisha Yesu akawaambia, "Usiku huu wa leo, ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: `Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.` 32Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya." 33Petro akamwambia Yesu "Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe." 34Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." 35Petro akamwambia, "Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe." Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo. 36Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali." 37Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. 38Hapo akawaambia, "Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami." 39Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: "Baba yangu, kama inawezekana, aacha kikombefo hiki cha mateso kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe." 40Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, "Ndiyo kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i tayari lakini mwili ni dhaifu." 42Akaenda tena mara ya pili akasali: "Baba yangu, kama haiwezekani kikombefp hiki kinipite bila mimi kukinywa, basi, mapenzi yako yafanyike." 43Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. 44Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. 45Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, "Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. 46Amkeni, twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti." 47Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. 48Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha wapa ishara akisema: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni." 49Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, "Shikamoo, Mwalimu!" Kisha akambusu. 50Yesu akamwambia, "Rafiki, fanya ulichokuja kufanya." Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. 51Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. 52Hapo Yesu akamwambia, "Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. 53Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?" 55Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, "Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama kwamba mimi ni mnyang`anyi? Kila siku nilikuwa Hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! 56Lakini haya yote yametendeka ili Maandiko ya manabii yatimie." Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. 57Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokusanyika walimu wa Sheria na wazee. 58Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa Kuhani Mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa. 59Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumwua, 60lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili, 61wakasema, "Mtu huyu alisema: `Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu."` 62Kuhani Mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, "Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?" 63Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani Mkuu akamwambia, "Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, twambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!" 64Yesu akamwambia, "Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa Mwenyezi, akija juu ya mawingu ya mbinguni." 65Hapo, Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akasema, "Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake. 66Ninyi mwaonaje?" Wao wakamjibu, "Anastahili kufa!" 67Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi, 68wakasema, "Haya Kristo, tutabirie; ni nani amekupiga!" 69Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, "Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya." 70Petro akakana mbele ya wote akisema, "Sijui hata unasema nini." 71Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, "Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti." 72Petro akakana tena kwa kiapo: "Simjui mtu huyo." 73Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, "Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha." 74Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, "Simjui mtu huyo!" Mara jogoo akawika. 75Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: "Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." Basi, akatoka nje akalia sana.

Chapter 27

1Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua. 2Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa. 3Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha. 4Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako." 5Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga. 6Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu." 7Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. 8Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu. 9Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei, 10wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza." 11Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema." 12Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno. 13Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?" 14Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana. 15Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka. 16Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba. 17Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Barabafq ama Yesu aitwae Kristo?" 18Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu. 19Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake." 20Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe. 21Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!" 22Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!" 23Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!" 24Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe." 25Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!" 26Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe. 27Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. 28Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. 29Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!" 30Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. 31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. 32Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. 33Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa," 34wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. 35Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. 36Wakaketi, wakawa wanamchunga. 37Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi." 38Wanyang`anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. 39Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, 40"Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!" 41Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema, 42"Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. 43Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka." 44Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. 45Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza. 46Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" 47Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya." 48Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. 49Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa." 50Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. 51Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; 52makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; 53nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. 54Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu." 55Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. 57Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe. 59Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani, 60akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. 61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi. 62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, 63Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, `Baada ya siku tatu nitafufuka.` 64Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali." 65Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo." 66Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.

Chapter 28

1Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi. 2Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia. 3Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa. 5Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, "Ninyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. 6Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala. 7Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni." 8Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake. 9Mara, Yesu akakutana nao, akawasalimu: "Salamu." Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake. 10Kisha Yesu akawaambia, "Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona." 11Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia. 12Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13wakisema, "Ninyi mtasema hivi: `Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.` 14Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi hamtapata matatizo." 15Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo. 16Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu. 17Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka. 18Yesu akaja karibu, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. 20Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."

Mark

Chapter 1

1Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.fa 2Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako. 3Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito yake."` 4Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. 5Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. 6Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 7Naye alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. 8Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu." 9Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. 10Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. 11Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe." 12Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, 13akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamtumikia. 14Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, 15"Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!" 16Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. 17Yesu akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 19Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata. 21Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha. 22Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. 23Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, 24akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!" 25Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu." 26Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. 27Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!" 28Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya. 29Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. 30Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. 31Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. 32Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. 33Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. 34Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani. 35Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta. 37Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu anakutafuta." 38Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo." 39Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo. 40Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!" 41Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika!" 42Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. 43Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya vikali, 44"Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona." 45Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

Chapter 2

1Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani. 2Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake, 3wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne. 4Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka. 5Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Mwanangu, umesamehewa dhambi zako." 6Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao, 7"Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake." 8Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 9Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, `Umesamehewa dhambi zako`, au kumwambia, `Inuka! Chukua mkeka wako utembee?` 10Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, 11"Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende nyumbani!" 12Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, "Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili." 13Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha. 14Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, "Nifuate!" Lawi akasimama, akamfuata. 15Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake. 16Basi, baadhi ya walimu wa Sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watoza ushuru, wakawauliza wanafunzi wake, "Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?" 17Yesu alipowasikia, akawaambia, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi." 18Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, "Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?" 19Yesu akajibu, "Walioalikwa harusini wanawezaje kufunga kama bwana harusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana harusi hawawezi kufunga. 20Lakini wakati utafika ambapo bwana harusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. 21"Hakuna mtu anayekata kiraka kutoka katika nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama akifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi. 22Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama akifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!" 23Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano. 24Mafarisayo wakawaambia, "Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya wakati wa Sabato?" 25Yesu akawajibu, "Je, hamjapata kusoma juu ya kile alichofanya Daudi wakati alipohitaji chakula? Yeye pamoja na wenzake waliona njaa, 26naye akaingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa Kuhani Mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake." 27Basi, Yesu akawaambia, "Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato! 28Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ni Bwana hata wa Sabato."

Chapter 3

1Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza. 2Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya sabato ili wapate kumshtaki. 3Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, "Njoo hapa katikati." 4Kisha, akawauliza, "Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?" Lakini wao hawakusema neno. 5Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena. 6Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu. 7Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea, 8Idumea, ng`ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda. 9Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga. 10Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa. 11Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaaza sauti, "Wewe ni Mwana wa Mungu!" 12Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu. 13Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea, 14naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume,fb wakae naye, awatume kuhubiri 15na wawe na mamlaka ya kuwafukuza pepo. 16Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro), 17Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake "wanangurumo"), 18Andrea na Filipo, Batholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanani na 19Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. 20Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula. 21Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba amepatwa na wazimu. 22Nao walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, "Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo." 23Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano,"Shetani anawezaje kumfukuza Shetani? 24Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopigana, utawala huo hauwezi kudumu. 25Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia. 26Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa. 27"Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake. 28"Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote; 29lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele." 30Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, "Ana pepo mchafu.") 31Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kutaka kumwona. 32Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, wakamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona." 33Yesu akawaambia, "Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?" 34Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, "Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu."

Chapter 4

1Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. 2Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, 3"Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. 4Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. 5Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Mbegu hizo ziliota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. 6Jua lilipochomoza, zikachomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. 7Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. 8Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikakua na kuzaa: moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia." 9Kisha akawaambia, "Mwenye masikio na asikie!" 10Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. 11Naye akawaambia, "Ninyi mmejaliwa kujua siri ya Utawala wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, 12ili, `Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe."` 13Basi, Yesu akawauliza, "Je, ninyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? 14Mpanzi hupanda neno la Mungu. 15Watu wengine ni kama wale walio njiani ambapo mbegu zilianguka. Hawa hulisikia hilo neno lakini mara Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. 16Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu wanapolisikia hilo neno hulipokea kwa furaha. 17Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno mara wanakata tamaa. 18Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaolisikia hilo neno, 19lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. 20Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia moja." 21Yesu akaendelea kuwaambia, "Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa pishi au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. 22Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. 23Mwenye masikio na asikie!" 24Akawaambia pia, "Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. 25Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa." 26Yesu akaendelea kusema, "Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. 27Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. 28Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. 29Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika." 30Tena, Yesu akasema, "Tuufananishe Utawala wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? 31Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. 32Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake." 33Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. 34Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu. 35Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng`ambo." 36Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo. 37Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. 38Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?" 39Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. 40Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?" 41Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?"

Chapter 5

1Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng`ambo ya ziwa. 2Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye. 3Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo. 4Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia. 5Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe. 6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia 7akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!" 8Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.") 9Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni `Jeshi`, maana sisi tu wengi." 10Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile. 11Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima. 12Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie." 13Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini. 14Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia. 15Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa. 16Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe. 17Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao. 18Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye. 19Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma." 20Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa. 21Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. 22Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, 23akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi." 24Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande. 25Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. 26Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. 28Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona." 29Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. 30Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?" 31Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?" 32Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. 33Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. 34Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako." 35Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?" 36Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu." 37Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. 38Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. 39Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu." 40Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. 41Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!" 42Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. 43Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.

Chapter 6

1Yesu aliondoka hapo akaenda katika kijiji chake, akifuatwa na wanafunzi wake. 2Siku ya Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sunagogi. Wengi waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, ameyapata wapi mambo haya? Ni hekima gani hii aliyopewa? Tena, anatendaje maajabu haya anayoyafanya? 3Je, huyu si yule seremala mwana wa Maria, na ndugu yao kina Yakobo, Yose, Yuda na Simoni; Je, dada zake si wanaishi papa hapa kwetu?" Basi, wakawa na mashaka naye. ic\is Ndani ya Sunagogi (Marko 6:2)\ie 4Yesu akawaambia, "Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake, kwa jamaa zake na nyumbani mwake." 5Hakuweza kutenda miujiza hapo, ila aliwawekea mikono wagonjwa wachache, akawaponya. 6Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao. Kisha Yesu alivitembelea vijiji vya pale karibu akiwafundisha watu. 7Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwatoa pepo wachafu, 8na kuwaamuru, "Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni. 9Vaeni viatu lakini msivae kanzu mbili." 10Tena aliwaambia, "Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 11Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakung`uta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao." 12Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu. 13Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya. 14Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, "Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake." 15Wengine walisema, "Mtu huyu ni Eliya." Wengine walisema, "Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale." 16Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, "Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka." 17Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake. 18Yohane alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako." 19Basi Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumwua, asiweze. 20Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana. 21Ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya. 22Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, "Niombe chochote utakacho, nami nitakupa." 23Tena akamwapia, "Chochote utakachoniomba, nitakupa: hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu." 24Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, "Niombe nini?" Naye akamjibu, "Kichwa cha Yohane mbatizaji." 25Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, "Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji." 26Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia. 27Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani, 28akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake. 29Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakachukua mwili wake, wakauzika kaburini. 30Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha. 31Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno walikuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, Yesu akawaambia, "Twendeni peke yetu mahali pa faragha kula chakula, mkapumzike kidogo." 32Basi, Wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha. 33Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika. 34Waliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi. 35Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, "Hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa. 36Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula." 37Lakini Yesu akawaambia, "Wapeni ninyi chakula." Nao wakamwuliza, "Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari mia mbili, na kuwapa chakula?" 38Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame." Walipokwisha tazama, wakamwambia, "Kuna mikate mitano na samaki wawili." ic\is Mikate na samaki (Marko 6:38)\ie 39Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi. 40Nao wakaketi makundimakundi ya watu mia moja na ya watu hamsini. 41Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume elfu tano. 45Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ng`ambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu. 46Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali. 47Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea akitembea juu ya maji. Alitaka kuwapita. 49Lakini walimwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu, wakapiga yowe. 50Maana wote walipomwona waliogopa sana. Mara Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!" 51Kisha akapanda mashuani walimokuwa, na upepo ukatulia. Nao wakashangaa sana. 52maana hawakuwa bado wameelewa maana ya ile mikate. Akili zao zilikuwa bado zimepumbazika. 53Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54Walipotoka mashuani, mara watu wakamtambua Yesu. 55Basi, kwa haraka wakazunguka katika nchi ile yote, wakaanza kuwachukua wagonjwa wamelala juu ya mikeka yao, wakawapeleka kila mahali waliposikia Yesu yupo. 56Kila mahali Yesu alipokwenda, vijijini, mijini, au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi waguse walau pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.

Chapter 7

1Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. 2Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. 3Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. 4Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza.fc Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba. 5Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, "Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?" 6Yesu akawajibu, "Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: `Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. 7Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.` 8Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu." 9Yesu akaendelea kusema, "Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu. 10Maana Mose aliamuru: `Waheshimu baba yako na mama yako,` na, `Anayemlaani baba au mama, lazima afe.` 11Lakini ninyi mwafundisha, `Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu), 12basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake.` 13Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo." 14Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, "Nisikilizeni nyote, mkaelewe. 15Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi."fd 16missing 17Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. 18Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi, 19kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.) 20Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi. 21Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, 22uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. 23Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi." 24Yesu aliondoka hapo, akaenda hadi wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. 25Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. 26Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. 27Yesu akamwambia, "Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." 28Lakini huyo mama akasema, "Sawa, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto." 29Yesu akamwambia, "Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!" 30Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka. 31Kisha Yesu aliondoka wilayani Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. 32Basi, wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. 33Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. 34Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, "Efatha," maana yake, "Funguka." 35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. 36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. 37Watu walishangaa sana, wakasema, "Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema!"

Chapter 8

1Wakati huo umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, 2"Nawahurumia watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu, wala hawana chakula. 3Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali." 4Wanafunzi wake wakamwuliza, "Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?" 5Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Nao wakamjibu, "Saba." 6Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia. 7Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile. 8Watu wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki yaliyosalia wakajaza makapu saba. 9Nao waliokula walikuwa watu wapatao elfu nne. Yesu akawaaga, 10na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha. 11Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka awafanyie ishara kuonyesha anayo idhini kutoka mbinguni. 12Yesu akahuzunika rohoni, akasema, "Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote!" 13Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng`ambo ya pili ya ziwa. 14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. 15Yesu akawaonya, "Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode." 16Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, "Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate." 17Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa? 18Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki 19wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu elfu tano? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki ya makombo?" Wakamjibu, "Kumi na viwili." 20"Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu elfu nne, mlikusanya makapu mangapi ya makombo?" Wakamjibu, "Saba." 21Basi, akawaambia, "Na bado hamjaelewa?" 22Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu mmoja, wakamwomba amguse. 23Yesu akamshika mkono huyo kipofu, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, "Je, unaweza kuona kitu?" 24Huyo kipofu akatazama, akasema, "Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea." 25Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa. 26Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, "Usirudi kijijini!" 27Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?" 28Wakamjibu, "Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya na wengine mmojawapo wa manabii." 29Naye akawauliza, "Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?" Petro akamjibu, "Wewe ndiwe Kristo." 30Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake. 31Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake: "Ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Atauawa na baada ya siku tatu atafufuka." 32Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Basi, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. 33Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, "Ondoka mbele yangu, Shetani! Fikira zako si za kimungu ila ni za kibinadamu!" 34Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa. 36Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake? 37Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake? 38Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisichomjali Mungu anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu."

Chapter 9

1Yesu akaendelea kuwaambia, "Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa enzi." 2Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, 3mavazi yake yakang`aa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. 4Eliya na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. 5Petro akamwambia Yesu, "Mwalimu, ni vizuri sana kwamba tuko hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya." 6Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. 7Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni." 8Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao. 9Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka wafu. 10Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka wafu. 11Wakamwuliza Yesu, "Mbona walimu wa Sheria wanasema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?" 12Naye akawajibu, "Naam, Eliya anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa? 13Lakini nawaambieni, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake." 14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya walimu wa Sheria walikuwa wanajadiliana nao. 15Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu. 16Yesu akawauliza, "Mnajadiliana nini nao?" 17Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, "Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu. 18Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza." 19Yesu akawaambia, "Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu." 20Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto, 21"Amepatwa na mambo hayo tangu lini?" Naye akamjibu, "Tangu utoto wake. 22Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!" 23Yesu akamwambia, "Eti ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani." 24Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, "Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie!" 25Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu, "Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu-kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!" 26Hapo huyo pepo alipaaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, "Amekufa!" 27Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama. 28Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, "Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?" 29Naye akawaambia, "Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala tu." 30Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa, 31kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, "Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka." 32Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza. 33Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, "Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?" 34Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliye mkuu kati yao. 35Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, "Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na kuwa mtumishi wa wote." 36Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamku mbatia, halafu akawaambia, 37"Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma." 38Yohane akamwambia, "Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu." 39Lakini Yesu akasema, "Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya muujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu. 40Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu. 41Mtu yeyote atakeyewapeni kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu ninyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake. 42"Mtu yeyote atakayemfanya mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini. 43Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia kwenye uzima bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu.fe 44missing 45Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uzima bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.ff 46missing 47Na jicho lako likikukosesha, ling`oe! Afadhali kuingia katika utawala wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. 48Humo wadudu wake hawafi, na moto hauzimiki. ic\is Mawe ya kusagia (Marko 9:42)\ie moto hauzimiki. moto hauzimiki. 49"Maana kila mmoja atakolezwa kwa moto. 50Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu."

Chapter 10

1Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea na hata ng`ambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake. 2Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, "Je, ni halali mtu kumpa talaka mkewe?" 3Yesu akawajibu, "Mose aliwapa maagizo gani?" 4Nao wakasema, "Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha." 5Yesu akawaambia, "Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke. 7Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, 8nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. 9Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe." 10Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo. 11Naye akawaambia, "Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe. 12Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini." 13Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. 14Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. 15Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia katika Ufalme huo." 16Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki. 17Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, "Mwalimu mwema, nifanyeje ili niupate uzima wa milele?" 18Yesu akamjibu, "Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. 19Unazijua amri: `Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Usidanganye; Waheshimu baba na mama yako."` 20Naye akamjibu, "Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu." 21Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, "Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda ukauze vitu ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate." 22Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi. 23Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, "Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!" 24Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, "Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu." 26Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, "Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?" 27Yesu akawatazama, akawaambia, "Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana." 28Petro akamwambia, "Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!" 29Yesu akasema, "Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, 30atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uzima wa milele. 31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza." 32Basi, walikuwa njiani kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata: 33"Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa. 34Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua. Na baada ya siku tatu atafufuka." 35Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, "Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba." 36Yesu akawauliza, "Mnataka niwafanyie nini?" 37Wakamjibu, "Uturuhusu tuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wa Ufalme wako." 38Yesu akawaambia, "Hamjui mnachoomba! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?" 39Wakamjibu, "Tunaweza." Yesu akawaambia, "Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. 40Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga, bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa." 41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. 42Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. 43Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. 44Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. 45Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila alikuja kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi." 46Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mwombaji aitwaye Bartimayo mwana wa Timayo alikuwa ameketi kando ya barabara. 47Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaaza sauti, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!" 48Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaaza sauti, "Mwana wa Daudi, nihurumie!" 49Yesu alisimama, akasema, "Mwiteni." Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, "Jipe moyo! Simama, anakuita." 50Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu. 51Yesu akamwuliza, "Unataka nikufanyie nini?" Huyo kipofu akamwambia, "Mwalimu, naomba nipate kuona." 52Yesu akamwambia, "Nenda, imani yako imekuponya." Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.

Chapter 11

1Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, 2akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwana punda amefungwa ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. 3Kama mtu akiwauliza, `Mbona mnafanya hivyo?` Mwambieni, `Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara."` ic\is Bethania (Marko 11:1)\ie 4Basi, wakaenda, wakamkuta mwana punda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, 5baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza "Kwa nini mnamfungua huyo mwana punda?" 6Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. 7Wakampelekea Yesu huyo mwana punda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana punda, na Yesu akaketi juu yake. 8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. 9Watu wote waliotangulia na wale waliofuata wakapaaza sauti zao wakisema, "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! 10Ubarikiwe Ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni!" 11Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka Hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili. 12Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. 13Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila majani matupu, kwa vile hayakuwa majira ya mtini kuzaa matunda. 14Hapo akauambia mtini, "Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako." Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo. 15Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia Hekaluni, akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16Hakumruhusu mtu yeyote kupitia Hekaluni akichukua kitu. 17Kisha akawafundisha, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!` Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi!" 18Makuhani wakuu na walimu wa Sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. 19Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini. 20Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. 21Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, "Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!" 22Yesu akawaambia, "Mwaminini Mungu. 23Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: `Ng`oka ukajitose baharini` bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo. 24Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa. 25Mnaposimama kusali, sameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu.fg hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu." 26missing 27Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walimwendea, 28wakamwuliza, "Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?" 29Lakini Yesu akawaambia, "Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, na pia nitawaambieni ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni." 31Wakaanza kujadiliana, "Tukisema, `Yalitoka mbinguni`, atatuuliza, `Basi, mbona hamkumsadiki?` 32Na tukisema, `Yalitoka kwa watu..."` (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.) 33Basi, wakamjibu Yesu, "Sisi hatujui." Naye Yesu akawaambia, "Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani."

Chapter 12

1Yesu alianza kusema nao kwa mifano: "Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali. 2Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake. 3Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu. 4Akatuma tena mtumishi mwingine; huyu wakamuumiza kichwa na kumtendea vibaya. 5Mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena, na huyo wakamuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa. 6Alibakiwa bado na mtu mmoja, yaani mwanawe mpendwa. Mwishowe akamtuma huyo akisema, `Watamheshimu mwanangu.` 7Lakini hao wakulima wakaambiana, `Huyu ndiye mrithi, basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu!` 8Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu. ic Mnara ndani ya shamba la mizabibu (Marko 12:1) 9"Basi, mwenye shamba atafanya nini? Atakuja kuwaangamiza hao wakulima na kulikodisha hilo shamba la mizabibu kwa watu wengine. 10Je, hamjasoma Maandiko haya? `Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. 11Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu."` 12Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walifahamu ya kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu. Kwa hiyo walijaribu kumtia nguvuni, lakini waliogopa umati wa watu. Basi, wakamwacha wakaenda zao. 13Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake. 14Wakamwendea, wakamwambia, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu unayesema ukweli mtupu, wala humjali mtu yeyote. Wala cheo cha mtu si kitu kwako, lakini wafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? Tulipe au tusilipe?" 15Lakini Yesu alijua unafiki wao, akawaambia, "Mbona mnanijaribu? Nionyesheni sarafu." 16Wakamwonyesha. Naye akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?" Wakamjibu, "Ni ya Kaisari." 17Basi, Yesu akawaambia, "Mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na Mungu yaliyo yake Mungu." Wakashangazwa sana naye. 18Masadukayo wasemao kwamba hakuna ufufuo walimwendea Yesu, wakamwuliza, 19"Mwalimu, Mose alituagiza hivi: `Mtu akifa na kuacha mke bila mtoto, ndugu yake lazima amchukue huyo mama mjane amzalie watoto ndugu yake marehemu.` 20Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa, akafa bila kuacha mtoto. 21Ndugu wa pili akamwoa huyo mjane, naye pia akafa bila kuacha mtoto; na ndugu watatu hali kadhalika. 22Wote saba walikufa bila kuacha mtoto. Mwishowe yule mama mjane naye akafa. 23Basi, siku watu watakapofufuka, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa." 24Yesu akawaambia, "Ninyi mmekosea sana, kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. 25Maana wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamjasoma kitabu cha Mose katika sehemu inayohusu kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto? Mungu alimwambia Mose, `Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.` 27Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Ninyi mmekosea sana!" 28Mmojawapo wa walimu wa Sheria alifika, akasikia mabishano yao. Alipoona kwamba Yesu aliwajibu vyema, akajitokeza akamwuliza, "Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?" 29Yesu akamjibu, "Ya kwanza ndiyo hii: `Sikiliza, Israeli! Bwana Mungu wetu ndiye peke yake Bwana. 30Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.` 31Na ya pili ndiyo hii: `Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.` Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi." 32Basi, yule mwalimu wa Sheria akamwambia, "Vyema Mwalimu! Umesema kweli kwamba Mungu ni mmoja tu wala hakuna mwingine ila yeye. 33Na ni lazima mtu kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa akili yote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe. Jambo hili ni muhimu zaidi kuliko dhabihu na sadaka zote za kuteketezwa." 34Yesu alipoona kwamba huyu mtu alimjibu kwa ujasiri, akamwambia, "Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu." Baada ya hayo, hakuna mtu aliyethubutu tena kumwuliza kitu. 35Wakati Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, aliuliza, "Mbona walimu wa Sheria wanasema ya kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36Daudi mwenyewe akiongozwa na Roho Mtakatifu alisema: `Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, Mpaka nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako."` 37"Daudi mwenyewe anamwita Kristo Bwana. Basi, Kristo atakuwaje mwanae?" Umati wa watu ulikuwa ukimsikiliza kwa furaha. 38Katika mafundisho yake, Yesu alisema, "Jihadharini na walimu wa Sheria ambao hupenda kupitapita wamejivalia kanzu ndefu na kusalimiwa na watu kwa heshima sokoni; hupenda kuketi mahali pa heshima katika masunagogi, 39na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. 40Huwanyonya wajane huku wakijisingizia kusali sala ndefu. Siku ya hukumu watapata adhabu kali!" 41Yesu alikuwa ameketi karibu na sanduku la hazina. Akawa anatazama jinsi watu wengi walivyokuwa wakitoa fedha na kuzitia katika hazina ya Hekalu. Matajiri wengi walitoa fedha nyingi. 42Hapo akaja mama mmoja mjane maskini, akatoa sarafu mbili ndogo za fedha. 43Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, "Kweli nawaambieni, huyu mama mjane maskini ametoa zaidi kuliko wengine wote waliotia fedha katika sanduku la hazina. 44Maana wote walitoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa yote aliyokuwa nayo, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi."

Chapter 13

1Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!" 2Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa." 3Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, 4"Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?" 5Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. 6Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi. 7Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. 8Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. 9"Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao. 10Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. 11Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. 12Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 13Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. 14"Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani. 15Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. 16Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. 17Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! 18Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. 19Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. 20Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. 21"Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki. 22Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana. 23Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. 24"Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. 25Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. 26Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. 27Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. 28"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 29Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. 30Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. 31Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 32"Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. 33Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. 34Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho. 35Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. 36Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. 37Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"

Chapter 14

1Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue. 2Lakini walisema, "Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia." 3Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani. 4Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika wakajisemea, "Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya? 5Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha denari mia tatu, wakapewa maskini!" Wakamkemea huyo mama. 6Lakini Yesu akawaambia, "Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema. 7Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. 8Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa maziko. 9Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa ajili ya kumkumbuka." 10Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alienda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu. 11Makuhani wakuu waliposikia habari hiyo, walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti Yesu. 12Siku ya kwanza ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wakati ambapo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, "Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?" 13Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, "Nendeni mjini, nanyi mtakutana na mtu anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni 14mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, `Mwalimu anasema: wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?` 15Naye atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo." 16Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka. 17Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 18Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti." 19Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, "Je, ni mimi?" 20Yesu akawaambia, "Ni mmoja wenu ninyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli. 21Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!" 22Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni; huu ni mwili wangu." 23Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa; nao wote wakanywa katika kikombe hicho. 24Akawaambia, "Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi. 25Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika Ufalme wa Mungu." 26Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. 27Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema: `Nitampiga mchungaji nao kondoo watatawanyika.` 28Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya." 29Petro akamwambia "Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!" 30Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu." 31Lakini Petro akasisitiza, "Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe." Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo. 32Basi, wakafika katika bustani iitwayo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa wakati mimi nasali." 33Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. 34Akawaambia, "Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe." 35Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso. 36Akasema, "Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe." ic\is Bustani ya Gethsemane (Marko 14:32)\ie 37Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, "Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?" 38Kisha akawaambia, "Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu." 39Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale. 40Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu. 41Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, "Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu. 42Amkeni, twendeni zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia." 43Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee. 44Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni, mkampeleke chini ya ulinzi." 45Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akasema, "Mwalimu!" Kisha akambusu. 46Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. 47Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. 48Yesu akawaambia, "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang`anyi? 49Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie." 50Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. 51Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata. 52Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi. 53Basi, wakampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na walimu wa Sheria walikuwa wamekutanika. 54Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ya wa Kuhani Mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. 55Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakupata. 56Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana. 57Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema: 58"Tulimsikia mtu huyu akisema, `Nitaliharibu Hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono."` 59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana. 60Basi, Kuhani Mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, "Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?" 61Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, "Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?" 62Yesu akajibu, "Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa Mwenyezi, akija katika mawingu ya mbinguni." 63Hapo Kuhani Mkuu akararua joho lake, akasema, "Tuna haja gani tena ya mashahidi? 64Mmesikia kufuru yake! Ninyi mwaonaje?" Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa. 65Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, "Bashiri ni nani aliyekupiga!" Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi. 66Petro alipokuwa bado chini ukumbini, mmoja wa wajakazi wa kuhani Mkuu alikuja. 67Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, "Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti." 68Lakini Petro akakana, "Sijui, wala sielewi unayosema!" Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika. 69Yule mjakazi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, "Mtu huyu ni mmoja wao." 70Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, "Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya." 71Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, "Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake." 72Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: "Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu." Petro akabubujika machozi.

Chapter 15

1Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, walimu wa Sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato. 2Pilato akamwuliza Yesu, "Je, wewe ni mfalme wa Wayahudi?" Yesu akajibu, "Wewe umesema." 3Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi. 4Pilato akamwuliza tena Yesu, "Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako." 5Lakini Yesu hakujibu neno, hata pilato akashangaa. 6Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka. 7Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji. 8Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake. 9Pilato akawauliza, "Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?" 10Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu. 11Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba. 12Pilato akawauliza tena, "Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?" 13Watu wote wakapaaza sauti tena: "Msulubishe!" 14Lakini Pilato akawauliza, "Kwa nini! Amefanya kosa gani?" Lakini wao wakazidi kupaaza sauti, "Msulubishe!" 15Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe. 16Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari. 17Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani. 18Wakaanza kumsalimu, "Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!" 19Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia. 20Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. 21Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba wa Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha auchukue msalaba wa Yesu. 22Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la Kichwa." 23Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye akaikataa. 24Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini. 25Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26Na mshtaka wake ulikuwa umeandikwa: "Mfalme wa Wayahudi." 27Pamoja naye waliwasulubisha wanyang`anyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.fh Matakatifu yanayosema, "Aliwekwa kundi moja na waovu." 28missing 29Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, "Aha! Wewe mwenye kuvunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu! 30Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!" 31Nao makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria walimdhihaki wakisema, "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! 32Eti yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke msalabani ili tuone na kuamini." Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana. 33Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa kulikuwa giza nchini kote. 34Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eloi, Eloi, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" 35Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, "Sikiliza! Anamwita Eliya!" 36Mtu mmoja akakimbia, akachovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, "Hebu tuone kama Eliya atakuja kumteremsha msalabani!" 37Yesu akapaaza sauti kubwa, akakata roho. 38Basi, pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini. 39Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake aliona jinsi Yesu alivyolia kwa sauti na kukata roho, akasema, "Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!" 40Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria toka mji wa Magdala, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose. 41Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye. 42Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato. 43Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Armathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila uoga, akaomba apewe mwili wa Yesu. 44Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo. 45Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu auchukue mwili wake. 46Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango. 47Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.

Chapter 16

1Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. 2Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, jua lilipoanza kuchomoza, walienda kaburini. 3Nao wakawa wanaambiana, "Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?" 4Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.) 5Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana. 6Lakini huyo kijana akawaambia, "Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza. 7Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni." 8Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno. [[[ 9Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo saba. 10Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia. 11Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini. 12Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani. 13Nao pia wakaenda wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini. 14Mwishowe, Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka. 15Basi, akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu. 16Anayeamini na kubatizwa ataokolewa; asiyeamini atahukumiwa. 17Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya. 18Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona." 19Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu. 20Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.]fi

Luke

Chapter 1

1Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. 2Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. 3Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, 4ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa. 5Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. 8Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake." 18Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." 19Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. 20Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia." 21Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. 22Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. 23Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25"Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu." 26Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake. 39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. 40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti. 41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu, 42akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. 43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia." 46Naye Maria akasema, 47"Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. 48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. 49Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu. 50Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. 51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; 52amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. 53Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu. 54Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake. 55Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele." 56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake. 57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. 58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. 59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya. 60Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane." 61Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?" 62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. 63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu. 64Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. 66Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. 67Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu: 68"Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake. 69Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. 70Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, 71kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. 72Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. 73Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi 74tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, 75kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. 76Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; 77kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. 78Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu, 79na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani." 80Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.

Chapter 2

1Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe. 2Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. 3Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake. 4Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi. 5Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito. 6Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, 7akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. 8Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. 9Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. 10Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote. 11Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. 12Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini." 13Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: 14"Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!" 15Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha." 16Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. 17Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. 18Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. 19Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. 20Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. 21Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. 22Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana. 23Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana." 24Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana. 25Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. 26Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana. 27Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria, 28Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema: 29"Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani. 30Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako, 31ambao umeutayarisha mbele ya watu wote: 32Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli." 33Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. 34Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; 35na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako." 36Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. 37Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. 38Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. 39Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya. 40Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye. 41Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni." 49Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?" 50Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.

Chapter 3

1Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, alikuwa mkuu wa mikoa ya Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mkuu wa mkoa wa Abilene, 2na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu mjini Yerusalem. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane, mwana wa Zakariya, kule jangwani. 3Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani, akihubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi. 4Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake. 5Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa. 6Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu."` 7Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja? 8Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kusema: `Sisi ni watoto wa Abrahamu.` Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyageuza mawe haya yawe watoto wa Abrahamu! 9Lakini, sasa hivi shoka limewekwa tayari kukata mizizi ya miti. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni." 10Umati wa watu ukamwuliza, "Tufanye nini basi?" 11Akawajibu, "Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo." 12Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, "Mwalimu, tufanye nini?" 13Naye akawaambia, "Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa." 14Nao askari wakamwuliza, "Na sisi tufanye nini?" Naye akawajibu, "Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu." 15Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane: kuwa labda yeye ndiye Kristo. 16Hapo Yohane akawaambia wote, "Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17Yeye ni kama mtu anayeshika mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka, aipure nafaka yake, akusanye ngano ghalani mwake, na makapi ayachome kwa moto usiozimika." 18Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema. 19Lakini Yohane alimgombeza Herode, mkuu wa mkoa, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia, mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya. 20Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani. 21Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka, 22na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe." 23Yesu alipoanza kazi yake hadharani, alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mwana wa Yosefu, mwana wa Heli. 24Heli alikuwa mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yanai, mwana wa Yosefu, 25mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Hesli, mwana wa Nagai, 26mwana wa Maathi, mwana wa Matathia, mwana wa Shemeni, mwana wa Yoseki, mwana wa Yuda, 27mwana wa Yohanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri, 28mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri, 29mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri, mwana wa Yorimu, mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, 30mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yosefu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliakimu, 31mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi, 32mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni, 33mwana wa Aminadabu, mwana wa Admini, mwana wa Arni, mwana wa Hesroni, mwana wa Feresi, mwana wa Yuda, 34mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Abrahamu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori, 35mwana wa Serugi, mwana wa Reu, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala, 36mwana wa Kainani, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Noa, mwana wa Lameki, 37mwana wa Mathusala, mwana wa Henoki, mwana wa Yaredi, mwana wa Mahalaleli, mwana wa Kenani, 38mwana wa Enosi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, aliyekuwa wa Mungu.

Chapter 4

1Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. 2Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. 3Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate." 4Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Mtu haishi kwa mkate tu."` 5Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, 6"Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. 7Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu." 8Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."` 9Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, 10kwa maana imeandikwa: `Atawaamuru malaika wake wakulinde,` 11na tena, `Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."` 12Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Usimjaribu Bwana Mungu wako."` 13Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda. 14Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. 15Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote. 16Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. 17Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa: 18"Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, 19na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana." 20Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. 21Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo." 22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?" 23Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: `Mganga jiponye mwenyewe`, na pia mtasema: `Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."` 24Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake. 25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. 26Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni. 27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria." 28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. 29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. 30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake. 31Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. 32Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. 33Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: 34"We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!" 35Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. 36Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!" 37Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule. 38Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. 39Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia. 40Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. 41Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo. 42Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. 43Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo." 44Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.

Chapter 5

1Siku moja Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongana wanalisikiliza neno la Mungu. 2Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa; wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao. 3Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja, iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua. 4Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, "Peleka mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki." 5Simoni akamjibu, "Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu." 6Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. 7Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama. 8Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, "Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!" 9Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. 10Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, "Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu." 11Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata. 12Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: "Mheshimiwa, ukitaka, waweza kunitakasa." 13Yesu akaunyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka, takasika!" Mara ule ukoma ukamwacha. 14Yesu akamwamuru: "Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama inavyotakiwa na Sheria ya Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona." 15Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko. 17Siku moja Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na walimu wa Sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponyea wagonjwa. 18Mara watu wakaja wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani wamweke mbele ya Yesu. 19Lakini kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya dari, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. 20Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, "Rafiki, umesamehewa dhambi zako." 21Walimu wa Sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: "Nani huyu anayemkufuru Mungu kwa maneno yake? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!" 22Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, "Mnawaza nini mioyoni mwenu? 23Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, `Umesamehewa dhambi,` au kusema, `Simama utembee`? 24Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kusamehe dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Simama, chukua kitanda chako uende zako nyumbani." 25Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda zake nyumbani huku akimtukuza Mungu. 26Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: "Tumeona maajabu leo." 27Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtoza ushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, "Nifuate!" 28Lawi akaacha yote, akamfuata. 29Kisha Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake; na kundi kubwa la watoza ushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. 30Mafarisayo na walimu wa Sheria wakawanung`unikia wafuasi wake wakisema: "Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?" 31Yesu akawajibu, "Wenye afya hawahitaji daktari, lakini wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. 32Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, ili wapate kutubu." 33Watu wengine wakamwambia Yesu, "Wafuasi wa Yohane mbatizaji hufunga mara nyingi na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa." 34Yesu akawajibu, "Je, mnaweza kuwataka wale walioalikwa arusini wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao? 35Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao, na wakati huo ndipo watakapofunga." 36Yesu akawaambia mfano huu: "Hakuna mtu akataye kiraka cha nguo mpya na kukitia katika vazi kuukuu; kama akifanya hivyo, atakuwa amelikata hilo vazi jipya, na hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu. 37Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38Divai mpya hutiwa katika viriba vipya! 39Wala hakuna mtu ambaye hutamani kunywa divai mpya baada ya kunywa ya zamani, kwani husema: `Ile ya zamani ni nzuri zaidi."`

Chapter 6

1Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, "Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?" 3Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Kisheria, ni makuhani tu peke yao ndio walioruhusiwa kula mikate hiyo." 5Hivyo akawaambia, "Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato." 6Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani mlikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. 7Walimu wa Sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisingizio cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, "Inuka, simama katikati." Yule mtu akaenda akasimama katikati. 9Kisha Yesu akawaambia, "Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?" 10Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu. 12Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu. 13Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akachagua kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti. 17Baada ya kushuka mlimani pamoja na mitume, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo palikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote. 20Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: "Heri ninyi mlio maskini, maana Ufalme wa Mungu ni wenu. 21Heri ninyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri ninyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. 22"Heri yenu ninyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu! 23Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. 24Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. 25Ole wenu ninyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. 26Ole wenu ninyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo. 27"Lakini nawaambieni ninyi mnaonisikiliza: wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang`anya koti lako mwachie pia shati lako. 30Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyang`anya mali yako usimtake akurudishie. 31Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi. 32"Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda ninyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo! 34Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile! 35Ila nyinyi wapendeni adui zenu, na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia malipo, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. 37"Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho ambacho Mungu atatumia kwenu." 39Akawaambia mfano huu: "Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40Mwanafunzi hamshindi mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41Unawezaje kukiona kibanzi kilicho katika jicho la mwenzio, usione boriti iliyo katika jicho lako mwenyewe? 42Au, unawezaje kumwambia mwenzako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi katika jicho lako,` na huku huioni boriti iliyoko katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako, na hivyo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako. 43"Mti mwema hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake. 46"Mbona mwaniita `Bwana, Bwana,` na huku hamtimizi yale ninayosema? 47Nitawapeni mfano unaofaa kuonyesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49Lakini yeyote anayesikia maneno yangu lakini asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!"

Chapter 7

1Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu. 2Huko kulikuwa na jemadari mmoja Mroma ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu kufa. 3Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje amponye mtumishi wake. 4Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: "Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo, 5maana analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi." 6Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu kufika nyumbani kwa yule jemadari Mroma, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: "Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu. 7Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako; amuru tu, na mtumishi wangu atapona. 8Mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, `Nenda!`, naye huenda; namwambia mwingine, `Njoo!` naye huja; na nikimwambia mtumishi wangu, `Fanya hiki!`, hufanya." 9Yesu aliposikia hayo, alishangaa; halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, "Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli." 10Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa. 11Baadaye kidogo Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake pamoja na kundi kubwa la watu waliandamana naye. 12Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya kijana mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. 13Bwana alipomwona mama huyo, alimwonea huruma, akamwambia, "Usilie." 14Kisha akaenda, akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wanalichukua wakasimama. Halafu akasema, "Kijana! Nakuamuru, amka!" 15Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. 16Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema: "Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake." 17Habari hizo zikaenea kote katika Uyahudi na katika nchi za jirani. 18Wanafunzi wa Yohane walimpa habari Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake, 19aliwatuma kwa Bwana wamwulize: "Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?" 20Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, "Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: `Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?"` 21Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya, akawawezesha vipofu wengi kuona tena. 22Basi, Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari njema. 23Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!" 24Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: "Mlikwenda kule jangwani, hivi mlitaka kuona kitu gani? Mlitaka kuona unyasi unaotikiswa na upepo? 25Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevalia mavazi maridadi? La hasha! Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme! 26Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. 27Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: `Hapa ni mtumishi wangu, asema Bwana; ninamtuma akutangulie, akutayarishie njia."` 28Yesu akamalizia kwa kusema, "Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko yeye." 29Waliposikia hayo watu wote na watoza ushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane. 30Lakini Mafarisayo na walimu wa Sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu wakakataa kubatizwa na Yohane. 31Yesu akaendelea kusema, "Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani? 32Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: `Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeomboleza, lakini hamkulia!` 33Kwa maana Yohane alikuja, yeye alifunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: `Amepagawa na pepo!` 34Akaja Mwana wa Mtu; anakula na kunywa, mkasema: `Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!` 35Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali." 36Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula. 37Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi. 38Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi. 39Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, "Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi." 40Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, "Simoni, ninacho kitu cha kukwambia." Naye Simoni akamwambia, "Ndio Mwalimu, sema." Yesu akasema, 41"Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: mmoja alikuwa amekopa dinari mia tano, na mwingine hamsini. 42Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?" 43Simoni akamjibu, "Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana." Yesu akamwambia, "Sawa." 44Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, "Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake. 45Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu. 46Wewe hukunionyesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu. 47Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonyesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo." 48Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, "Umesamehewa dhambi zako." 49Na hapo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, "Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?" 50Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, "Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani."

Chapter 8

1Baada ya hayo, Yesu alipitia katika miji na vijiji akitangaza Habari Njema za Ufalme wa Mungu. Wale kumi na wawili waliandamana naye. 2Pia wanawake kadhaa ambao Yesu alikuwa amewatoa pepo wabaya na kuwaponya magonjwa, waliandamana naye. Hao ndio akina Maria (aitwaye Magdalene), ambaye alitolewa pepo wabaya saba; 3Yoana, mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa. Hao wanawake walikuwa wakiwatumikia kwa mali yao wenyewe. 4Kundi kubwa la watu lilikuwa linakusanyika, na watu walikuwa wanamjia Yesu kutoka kila mji. Naye akawaambia mfano huu: 5"Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda zile mbegu, nyingine zilianguka njiani, na wapita njia wakazikanyaga, na ndege wakazila. 6Nyingine zilianguka penye mawe, na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji. 7Nyingine zilianguka kati ya miti ya miiba. Ile miti ya miiba ilipoota ikazisonga. 8Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikaota na kuzaa asilimia mia." Baada ya kusema hayo, akapaaza sauti, akasema, "Mwenye masikio na asikie!" 9Wanafunzi wake wakamwuliza Yesu maana ya mfano huo. 10Naye akajibu, "Ninyi mmejaliwa kujua siri za Ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu. 11"Basi, maana ya mfano huu ni hii: mbegu ni neno la Mungu. 12Zile zilizoanguka njiani zinaonyesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini na hivyo wakaokoka. 13Zile zilizoanguka penye mawe zinaonyesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Hata hivyo, kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa. 14Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, na hawazai matunda yakakomaa. 15Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda. 16"Watu hawawashi taa na kuifunika kwa chombo au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga. 17"Chochote kilichofichwa kitafichuliwa na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani. 18"Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani kuwa anacho, kitachukuliwa." 19Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu. 20Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona. 21Lakini Yesu akawaambia watu wote, "Mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika." 22Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Tuvuke ziwa twende mpaka ng`ambo." Basi, wakaanza safari. 23Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari. 24Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, "Bwana, Bwana! Tunaangamia!" Yesu akaamka, akaikemea dhoruba na mawimbi, navyo vikatulia, kukawa shwari. 25Kisha akawaambia, "Iko wapi imani yenu?" Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, "Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?" 26Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ng`ambo ya ziwa. 27Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo, hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini. 28Alipomwona Yesu, alipiga kelele na kujitupa chini mbele yake, na kusema kwa sauti kubwa "We, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Juu una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!" 29Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikwishamwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani. 30Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Yeye akajibu, "Jina langu ni `Jeshi"`--kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa. 31Hao pepo wakamsihi asiwaamuru wamtoke na kwenda kwenye shimo lisilo na mwisho. ic 32Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa. 33Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakazama majini. 34Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari, mjini na mashambani. 35Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa. 36Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa. 37Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka. 38Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia, 39"Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea." Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea. 40Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea. 41Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake, 42kwa kuwa binti yake wa pekee, mwana wa pekee mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa mahututi. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande. 43Kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya. 44Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu. 45Yesu akasema, "Ni nani aliyenigusa?" Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, "Mwalimu, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!" 46Lakini Yesu akasema, "Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka." 47Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponyeshwa mara moja. 48Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani." 49Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: "Binti yako ameshakufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?" 50Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, "Usiogope; amini tu, naye atapona." 51Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana. 52Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, "Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!" 53Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa. 54Lakini Yesu akamshika mkono akasema, "Mtoto amka!" 55Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula. 56Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.

Chapter 9

1Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo juu ya pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa. 2Halafu akawatuma waende kuhubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3Akawaambia, "Mnaposafiri msichukue chochote: msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada. 4Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho. 5Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kung`uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao." 6Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali. 7Sasa, mtawala Herode, alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: "Yohane amefufuka kutoka wafu!" 8Wengine walisema kwamba Eliya ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani. 9Lakini Herode akasema, "Huyo Yohane nilimkata kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?" Akawa na hamu ya kumwona. 10Wale mitume waliporudi, walimweleza yote waliyoyafanya. Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida. 11Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya Ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa. 12Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, "Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani." 13Lakini Yesu akawaambia, "Wapeni ninyi chakula." Wakamjibu, "Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!" 14(Walikuwepo pale wanaume wapatao elfu tano.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini." 15Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote. 16Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. 17Wakala wote, wakashiba; wakakusanya makombo ya chakula, wakajaza vikapu kumi na viwili. 18Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, "Eti watu wanasema mimi ni nani?" 19Nao wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, hali wengine wanasema kuwa wewe ni mmoja wa manabii wa kale ambaye amefufuka." 20Hapo akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?" Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo wa Mungu." 21Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo. 22Akaendelea kusema: "Ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria; atauawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa." 23Kisha akawaambia watu wote, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa. 25Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe? 26Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. 27Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu." 28Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali. 29Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kung`aa sana. 30Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao ni Mose na Eliya, 31ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kifo chake ambacho angekikamilisha huko Yerusalemu. 32Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri kwamba tupo hapa: basi, tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."--Kwa kweli hakujua anasema nini. 34Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana. 35Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni." 36Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona. 37Kesho yake walipokuwa wakishuka kutoka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu. 38Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaaza sauti, akasema, "Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu--mwanangu wa pekee! 39Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi. 40Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza." 41Yesu akasema, "Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?" Kisha akamwambia huyo mtu, "Mlete mtoto wako hapa." 42Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake. 43Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu. Wale watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, 44"Tegeni masikio, myasikie mambo haya: Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu." 45Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo huo. 46Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi. 47Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye, 48akawaambia, "Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkubwa kuliko wote." 49Yohane alidakia na kusema, "Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu." 50Lakini Yesu akamwambia, "Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu." 51Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu. 52Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali. 53Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu alikuwa anaelekea Yerusalemu. 54Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona hayo, wakasema, "Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni uwateketeze?" 55Lakini yeye akawageukia, akawakemea.fa 56Wakatoka, wakaenda kijiji kingine. gani mliyo nayo; kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa." 57Walipokuwa wakisafiri njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, "Nitakufuata kokote utakakokwenda." 58Yesu akasema, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia." 59Kisha akamwambia mtu mwingine, "Nifuate." Lakini huyo akasema, "Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba yangu." 60Yesu akamwambia, "Waache wafu wazike wafu wao; bali wewe nenda ukatangaze Ufalme wa Mungu." 61Na mtu mwingine akamwambia, "Nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikawaage wale walio nyumbani kwangu." 62Yesu akamwambia, "Yeyote anayeshika jembe tayari kulima na huku anaangalia nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu."

Chapter 10

1Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda. 2Akawaambia, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. 3Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma ninyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwa mwitu. 4Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani. 5Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: `Amani iwe katika nyumba hii!` 6Kama akiwako mwenye kupenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni. 7Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile. 8Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni. 9Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: `Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.` 10Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni: 11`Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunawakung`utieni. Lakini, jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.` 12Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Sodoma. 13"Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwishavaa mavazi ya gunia kitambo, na kukaa katika majivu kuonyesha kwamba wametubu. 14Hata hivyo, Siku ya Hukumu ninyi mtapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Tiro na Sidoni. 15Na wewe Kafarnaumu, unataka kujikweza mpaka mbinguni? La; utaporomoshwa mpaka Kuzimu." 16Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma." 17Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, "Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako." 18Yeye akawaambia, "Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni. 19Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na ng`e, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru. 20Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni." ic 21Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa kuwa umewaficha wenye hekima na elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza." 22Kisha akasema, "Baba yangu ameweka yote mikononi mwangu. Hakuna amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala amjuaye Baba ni nani ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anataka kumfunulia hayo." 23Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, "Heri wanaoona yale mnayoyaona ninyi! 24Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona ninyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie." 25Baadaye mwalimu mmoja wa Sheria alisimama akamwuliza akitaka kumtega, "Mwalimu, nifanye nini ili nipate uzima wa milele?" 26Yesu akamwuliza, "Imeandikwa nini katika Sheria? Unaelewaje?" 27Akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe." 28Yesu akawaambia, "Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi." 29Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, "Na jirani yangu ni nani?" 30Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyang`anya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. 31Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. 32Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali akamwona, akapita kando. 33Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. 34Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai; na kuyafunga halafu akampandisha juu ya punda wake akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamuuguza. 35Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, `Muuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi."` 36Kisha Yesu akauliza, "Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonyesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?" 37Yule mwalimu wa Sheria akamjibu, "Ni yule aliyemwonea huruma." Yesu akamwambia, "Nenda ukafanye vivyo hivyo." 38Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja, aitwaye Martha, alimkaribisha nyumbani kwake. 39Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. 40Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, "Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie." 41Lakini Bwana akamjibu, "Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi. 42Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyag`anya."

Chapter 11

1Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, "Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake." 2Yesu akawaambia, "Mnaposali, semeni: `Baba! Jina lako litukuzwe; Ufalme wako ufike. 3Utupe daima chakula chetu cha kila siku. 4Utusamehe dhambi zetu, maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea; wala usitutie katika majaribu."` 5Kisha akawaambia, "Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: `Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu, 6kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.` 7Naye, akiwa ndani angemjibu: `Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!` 8Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. 9Kwa hiyo, ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa. 10Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye hufunguliwa. 11Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki? 12Na kama akimwomba yai, je, atampa ng`e? 13Ninyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Basi, baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba." 14Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea hata umati wa watu ukashangaa. 15Lakini baadhi ya watu hao wakasema, "Anamfukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo." 16Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonyesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. 17Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliofarakana wenyewe, hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yeyote inayofarakana huangamia. 18Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? 19Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu ninyi. 20Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. 21"Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. 22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. 23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. 24"Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: `Nitarudi kwenye makao yangu nilikotoka.` 25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. 26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko pale mwanzo." 27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: "Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!" 28Lakini Yesu akasema, "Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika." 29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, "Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona. 30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. 31Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni. 32Watu wa Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona! 33"Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga. 34Jicho lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza. 35Uwe mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. 36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang`aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake." 37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. 38Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa. 39Bwana akamwambia, "Ninyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. 40Wapumbavu ninyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? 41Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu. 42"Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine. 43"Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. 44Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu." 45Mmoja wa walimu wa Sheria akamwambia, "Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia." 46Yesu akamjibu, "Na ninyi walimu wa Sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. 47Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. 48Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. 49Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: `Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.` 50Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; 51tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka kifo cha Zakariya ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo haya. 52"Ole wenu ninyi walimu wa Sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; ninyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie." 53Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi 54ili wapate kumnasa kwa maneno yake.

Chapter 12

1Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. 2Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. 3Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonong`ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba. 4"Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. 5Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. 6Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. 7Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi! 8"Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. 9Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. 10"Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 11"Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. 12Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema." 13Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, "Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba." 14Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi mwamuzi au msuluhishi kati yenu?" 15Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo." 16Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. 17Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: `Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? 18Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu. 19Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.` 20Lakini Mungu akamwambia: `Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?"` 21Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu." 22Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. 23Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. 24Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi kuliko ndege! 25Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza urefu wa maisha yake? 26Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? 27Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. 28Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! 29"Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. 30Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. 31Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote mtapewa kwa ziada. 32"Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni Ufalme. 33Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. 34Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako. 35"Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; 36muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi. 37Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. 38Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri. 39Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. 40Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia." 41Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?" 42Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao? 43Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote. 45Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na kusema: `Bwana wangu amekawia sana kurudi` halafu aanze kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa, 46bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini.fb 47Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. 48Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi atatakiwa kutoa vingi zaidi. 49"Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa umewaka tayari! 50Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike! 51Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano. 52Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. 53Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake." 54Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: `Mvua itanyesha`, na kweli hunyesha. 55Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema `Kutakuwa na hali ya joto` na ndivyo inavyokuwa. 56Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi? 57"Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya? 58Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani. 59Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho."

Chapter 13

1Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko. 2Naye Yesu akawaambia, "Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu zaidi kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo? 3Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu, mtaangamia kama wao. 4Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu zaidi kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu? 5Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao." 6Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: "Mtu mmoja alikuwa na mtini katika shamba lake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja. 7Basi, akamwambia mfanyakazi wake: `Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, nami nisiambulie kitu. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?` 8Lakini naye akamjibu: `Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea. 9Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata."` 10Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato. 11Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima. 12Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama, umeponywa ugonjwa wako." 13Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu. 14Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato." 15Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng`ombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato? 16Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?" 17Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda. 18Yesu akauliza: "Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini? 19NI kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota hata ikawa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake." 20Tena akauliza: "Nitaulinganisha Ufalme wa Mungu na nini? 21Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga debe moja kisha unga wote ukaumuka wote." 22Yesu alindelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri. 23Mtu mmoja akamwuliza, "Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?" 24Yesu akawaambia, "Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. 25"Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Ninyi mtasimama nje na kuanza kupiga hodi mkisema: `Bwana, tufungulie mlango.` Lakini yeye atawajibu: `Sijui mmetoka wapi.` 26Nanyi mtaanza kumwambia: `Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.` 27Lakini yeye atasema: `Sijui ninyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.` 28Ndipo mtakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo, na manabii wote wapo katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi wenyewe mmetupwa nje! 29Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini, watakuja na kukaa kwenye karamu katika Ufalme wa Mungu. 30Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho." 31Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, "Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua." 32Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: `Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.` 33Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu. 34"Yerusalemu! We Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, Lakini wewe umekataa. 35Haya, utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Naam, hakika nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: `Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."`

Chapter 14

1Siku moja ya Sabato, Yesu alikwenda kula chakula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo; watu waliokuwapo hapo wakawa wanamchunguza. 2Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili. 3Yesu akawauliza walimu wa Sheria na Mafarisayo, "Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya sabato?" 4Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake. 5Halafu akawaambia, "Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng`ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?" 6Nao hawakuweza kumjibu swali hilo. 7Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano: 8"Kama mtu akikualika arusini, usiketi mahali pa heshima isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe; 9na mwenyeji wenu ninyi wawili atakuja na kukwambia: `Mwachie huyu nafasi.` Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho. 10Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akwambie: `Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.` Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe. 11Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa, na anayejishusha, atakwezwa." 12Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, "Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri, wasije nao wakakualika nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea. 13Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema viwete na vipofu, 14nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka." 15Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, "Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika Ufalme wa Mungu." 16Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi. 17Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake awaambie walioalikwa, `Njoni, kila kitu ni tayari.` 18Lakini wote, kwa namna moja, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: `Nimenunua shamba, kwa hiyo sina budi kwenda kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.` 19Mwingine akasema: `Nimenunua ng`ombe jozi tano wa kulima; sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.` 20Na mwingine akasema: `Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.` 21Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: `Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na waliolemaa.` 22Baadaye, mtumishi huyo akasema: `Bwana mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.` 23Yule bwana akamwambia mtumishi: `Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae. 24Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu."` 25Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia akawaambia, 26"Mtu yeyote akija kwangu, asipowachukia baba na mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 27Mtu asipochukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 28Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia? 29La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka 30wakisema: `Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.` 31"Au, ni mfalme gani ambaye, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza chini na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake elfu ishirini? 32Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali. 33Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho. 34"Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? 35Haifai kitu wala kwa udongo wala kwa mbolea. Watu huitupilia mbali. Sikieni basi, kama mna masikio!"

Chapter 15

1Siku moja, watoza ushuru na wahalifu wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. 2Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kunung`unika: "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao." 3Yesu akawajibu kwa mfano: 4"Hivi, mtu akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. 5Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. 6Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake akiwaambia, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.` 7Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. ic 8"Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, aifagie nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. 9Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake akisema, `Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.` 10Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu." 11Yesu akaendelea kusema, "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili. 12Yule mdogo, alimwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye akawagawia mali yake. 13Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. 14Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. 15Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. 16Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. 17Alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? 18Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. 19Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.` 20Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. 21"Mwanawe akamwambia: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.` 22Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! 23Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea! 24Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe. 25"Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani akasikia vifijo na ngoma. 26Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: `Kuna nini?` 27Huyo mtumishi akamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.` 28Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. 29Lakini yeye akamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! 30Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.` 31Baba yake akamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. 32Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."`

Chapter 16

1Yesu aliwaambia wanafunzi wake: "Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake. 2Yule tajiri akamwita akamwambia: `Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.` 3Yule karani akafikiri: `Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu. 4Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.` 5Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmoja mmoja, akamwambia yule wa kwanza: `Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?` 6Yeye akamjibu: `Mapipa mia ya mafuta ya zeituni.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.` 7Kisha akamwuliza mdeni mwingine: `Wewe unadaiwa kiasi gani?` Yeye akamjibu: `Magunia mia ya ngano.` Yule karani akamwambia: `Chukua hati yako ya deni, andika themanini.` 8"Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga." 9Naye Yesu akaendelea kusema, "Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, mweze kupokewa nao katika makao ya milele. 10Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa. 11Kama basi, ninyi si hamjawa waaminifu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli? 12Na kama hamjakuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe? 13"Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali." 14Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu. 15Hapo akawaambia, "Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka. 16"Sheria na maandishi ya manabii vilikuweko mpaka wakati wa Yohane mbatizaji. Tangu hapo, Ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu. 17Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya Sheria kufutwa. 18"Yeyote anayemwacha mke wake na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. 19"Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau, na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku. 20Kulikuwa pia na maskini mmoja jina lake Lazaro, aliyekuwa amejaa vidonda na alikuwa analazwa mlangoni pa nyumba ya huyo tajiri. 21Lazaro alitamani kula makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kulamba vidonda vyake! 22"Ikatokea kwamba huyo maskini akafa, malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa. 23Huyo tajiri, alikuwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye. 24Basi, akaita kwa sauti: `Baba Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.` 25Lakini Abrahamu akamjibu: `Kumbuka mwanangu, kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa. 26Licha ya hayo, kati yetu na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, wala wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.` 27Huyo aliyekuwa tajiri akasema: `Basi baba, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu, 28maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.` 29Lakini Abrahamu akamwambia: `Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.` 30Lakini yeye akasema: `Sivyo baba Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka wafu na kuwaendea, watatubu.` 31Naye Abrahamu akasema: `Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka wafu."`

Chapter 17

1Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. 2Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa. 3Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, mwonye; akitubu, msamehe. 4Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema `Nimetubu`, lazima umsamehe." 5Mitume wakamwambia Bwana, "Utuongezee imani." 6Naye Bwana akajibu, "Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: `Ng`oka ukajipandikize baharini`, nao ungewatii. 7"Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia: `Haraka, njoo ule chakula?` 8La! Atamwambia: `Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na unywe.` 9Je utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa? 10Hali kadhalika na ninyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: `Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya."` 11Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia mipakani mwa Samaria na Galilaya. 12Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali. 13Wakapaza sauti wakisema, "Yesu Mwalimu, tuonee huruma!" 14Alipowaona akawaambia, "Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani." Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika. 15Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. 16Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria. 17Hapo Yesu akasema, "Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi? 18Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?" 19Halafu akamwambia huyo mtu, "Simama, uende zako; imani yako imekuponya." 20Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, "Ufalme wa Mungu utakuja lini?" Naye akawajibu, "Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana. 21Wala hakuna atakayeweza kusema, `Uko hapa`, au `Uko pale`. Kwa kweli Ufalme wa Mungu uko kati yenu." 22Halafu akawaambia wanafunzi wake, "Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona. 23Na watu watawaambieni: `Tazameni yuko hapa`; ninyi msitoke wala msiwafuate. 24Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku yake. 25Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki. 26Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu. 27Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote. 28Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga. 29Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote. 30Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa. 31"Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma. 32Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti. 33Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa. 34Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa. 35Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa."fc atachukuliwa na mwingine ataachwa.\ie 36missing 37Hapo wakamwuliza, "Ni wapi Bwana?" Naye akawaambia, "Ulipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia."

Chapter 18

1Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa. 2Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu. 3Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake. 4Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: `Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu, 5lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!"` 6Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya. 7Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza? 8Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?" 9Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine. 10"Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru. 11Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: `Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru. 12Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.` 13Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: `Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.` 14Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa." 15Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali. 16Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa. 17Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo." 18Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?" 19Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. 20Unazijua amri: `Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako."` 21Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu." 22Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate." 23Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana. 24Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu." 26Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?" 27Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu." 28Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!" 29Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, 30atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao." 31Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa. 32Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate. 33Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka." 34Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa. 35Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba. 36Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?" 37Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita." 38Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!" 39Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;" 40Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza, 41"Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena." 42Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya." 43Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.

Chapter 19

1Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo. 2Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri. 3Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu. 4Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo. 5Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako." 6Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha. 7Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung`unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi." 8Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang`anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne." 9Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu. 10Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea." ic 11Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.) 12Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi. 13Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: `Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.` 14Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: `Hatumtaki huyu atutawale.` 15"Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani. 16Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.` 17Naye akamwambia: `Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!` 18Mtumishi wa pili akaja, akasema: `Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.` 19Naye akamwambia pia: `Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.` 20"Mtumishi mwingine akaja, akasema: `Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa, 21kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.` 22Naye akamwambia: `Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda. 23Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?` 24Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: `Mnyang`anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.` 25Nao wakamwambia: `Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!` 26Naye akawajibu: `Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 27Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."` 28Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu. 29Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 30akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa. 31Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, `Bwana ana haja naye."` 32Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. 33Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?" 34Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji." 35Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu. 36Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. 37Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; 38wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!" 39Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!" 40Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti." 41Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia 42akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. 43Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. 44Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa." 45Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara 46akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi." 47Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, 48lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.

Chapter 20

1Siku moja, Yesu alipokuwa akiwafundisha watu Hekaluni na kuwahubiria juu ya Habari Njema, makuhani wakuu na walimu wa Sheria pamoja na wazee walifika, 2wakasema, "Tuambie! Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani?" 3Yesu akawaambia, "Na mimi nitawaulizeni swali: 4mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa Mungu au kwa watu?" 5Lakini wao wakajadiliana hivi: "Tukisema yalitoka mbinguni, yeye atatuuliza: `Mbona hamkumsadiki?` 6Na tukisema yalitoka kwa binadamu, watu wote hapa watatupiga mawe, maana wote wanaamini kwamba Yohane alikuwa nabii." 7Basi, wakamwambia, "Hatujui mamlaka hayo yalitoka wapi." 8Yesu akawaambia, "Hata mimi sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani." 9Yesu akaendelea kuwaambia watu mfano huu: "Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima; kisha akasafiri hadi nchi ya mbali, akakaa huko kwa muda mrefu. 10Wakati wa mavuno, mtu huyo alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akachukue sehemu ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga mtumishi huyo wakamrudisha mikono mitupu. 11Yule bwana akamtuma tena mtumishi mwingine; lakini wao wakampiga huyo vilevile na kumtendea vibaya, wakamrudisha mikono mitupu. 12Akamtuma tena wa tatu; huyu naye, baada ya kumwumiza, wakamfukuza. 13Yule mwenye shamba akafikiri: `Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpenzi; labda watamjali yeye.` 14Wale wakulima walipomwona tu, wakasemezana: `Huyu ndiye mrithi. Basi, tumwue ili urithi wake uwe wetu.` 15Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamwua." Yesu akauliza, "Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima? 16Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na atawapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu." Watu waliposikia maneno hayo, walisema: "Hasha! Yasitukie hata kidogo!" 17Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, "Maandiko haya Matakatifu yana maana gani basi? `Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!` 18Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo, atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamsaga kabisa." 19Walimu wa Sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu. 20Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali. 21Hao wapelelezi wakamwambia, "Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu. 22Basi, twambie kama ni halali, au la, kulipa kodi kwa Kaisari!" 23Yesu alitambua mtego wao, akawaambia, 24"Nionyesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?" 25Nao wakamjibu, "Ni vya Kaisari." Yesu akawaambia, "Basi, mpeni Kaisari vilivyo vyake Kaisari, na Mungu vilivyo vyake Mungu." 26Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake. 27Kisha Masadukayo, ambao husema kwamba wafu hawafufuki, wakamjia Yesu, wakasema: 28"Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu ya mtu fulani akifa na kumwacha mjane wake bila watoto, ni lazima ndugu yake amchukue huyo mama mjane, amzalie watoto ndugu yake marehemu. 29Sasa, wakati mmoja kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza alioa na baadaye akafa bila kuacha mtoto. 30Yule ndugu wa pili akamwoa yule mjane, naye pia, akafa; 31na ndugu wa tatu vilevile. Mambo yakawa yaleyale kwa wote saba--wote walikufa bila kuacha watoto. 32Mwishowe akafa pia yule mwanamke. 33Je, siku wafu watakapofufuliwa, mwanamke huyo atakuwa mke wa nani? Alikuwa ameolewa na wote saba." 34Yesu akawaambia, "Watu wa nyakati hizi huoa na kuolewa; 35lakini wale ambao Mungu atawawezesha kushiriki ule wakati wa ufufuo, hawataoa wala kuolewa. 36Ama hakika, hawawezi kufa tena, kwa sababu watakuwa kama malaika, na ni watoto wa Mungu kwa vile wamefufuliwa katika wafu. 37Lakini, kwamba kuna kufufuka kutoka wafu, hata Mose alithibitisha jambo hilo katika Maandiko Matakatifu. Katika sehemu ya Maandiko Matakatifu juu ya kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto, anamtaja Bwana kama Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo. 38Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa wale walio hai; maana wale aliowaita kwake, wanaishi naye." 39Baadhi ya wale walimu wa Sheria wakasema, "Mwalimu, umejibu vema kabisa." 40Walisema hivyo kwa sababu hawakuthubutu kumwuliza tena maswali mengine. 41Yesu akawauliza, "Yasemekanaje kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 42Maana Daudi mwenyewe anasema katika Zaburi: `Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia 43mpaka niwafanye adui zako kama kiti cha kuwekea miguu yako.` 44Ikiwa Daudi anamwita yeye, `Bwana,` basi atakuwaje mwanawe?" 45Yesu aliwaambia wanafunzi wake mbele ya watu wote, 46"Jihadharini na walimu wa Sheria ambao hupenda kupitapita wamevalia kanzu. Hupenda kusalimiwa na watu kwa heshima masokoni, huketi mahali pa heshima katika masunagogi na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. 47Huwadhulumu wajane huku wakisingizia kuwa wema kwa kusali sala ndefu. Hao watapata hukumu kali zaidi!"

Chapter 21

1Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu, 2akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. 3Basi, akasema, "Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote. 4Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi." 5Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, 6"Haya yote mnayoyaona--zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa." 7Basi, wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?" 8Yesu akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye`, na, `Wakati ule umekaribia`. Lakini ninyi msiwafuate! 9Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado." 10Halafu akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. 11Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. 12Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu. 13Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema. 14Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, 15kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. 16Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa. 17Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. 18Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. 19Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu. 20"Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. 21Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. 22Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. 23Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. 24Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia. 25"Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. 26Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. 27Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia." 29Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti mingine yote. 30Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 31Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia. 32Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. 33Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita. 34"Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla. 35Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote. 36Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu." 37Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. 38Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.

Chapter 22

1Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. 2Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. 3Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. 4Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. 5Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. 6Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. 7Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, "Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka." 9Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?" 10Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. 11Mwambieni mwenye nyumba: `Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?` 12Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo." 13Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka. 14Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. 15Akawaambia, "Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika Ufalme wa Mungu." 17Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema, "Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi. 18Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja." 19Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, "Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka." 20Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula, akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.fd 21"Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. 22Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti." 23Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo. 24Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine. 25Yesu akawaambia, "Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. 26Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. 27Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. 28"Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; 29na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme. 30Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 31"Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano. 32Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako." 33Naye Petro akamjibu, "Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa." 34Yesu akamjibu, "Nakwambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu." 35Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, "Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?" Wakajibu, "La." 36Naye akawaambia, "Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. 37Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: `Aliwekwa kundi moja na wahalifu,` ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake." 38Nao wakasema, "Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili." Naye akasema, "Basi!" 39Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata. 40Alipofika huko akawaambia, "Salini, msije mkaingia katika kishawishi." 41Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali: 42"Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu." 43Hapo, malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo. 44Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.fe ic 45Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni. 46Akawaambia, "Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi." 47Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu. 48Lakini Yesu akamwambia, "Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?" 49Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, "Bwana, tutumie panga zetu?" 50Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia. 51Hapo, Yesu akasema, "Acha! Hii inatosha." Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya. 52Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang`anyi? 53Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza." 54Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali. 55Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao. 56Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, "Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu." 57Lakini Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi." 58Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao." Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!" 59Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati." 60Lakini Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika. 61Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." 62Hapo akatoka nje, akalia sana. 63Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki. 64Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, "Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!" 65Wakamtolea maneno mengi ya matusi. 66Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo. 67Nao wakamwambia, "Twambie! Je, wewe ndiwe Kristo?" Lakini Yesu akawaambia, "Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki; 68na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu. 69Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi." 70Hapo wote wakasema, "Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?" Naye akasema, "Ninyi mnasema kwamba mimi ndiye." 71Nao wakasema, "Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe."sw4323

Chapter 23

1Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato. 2Wakaanza kumshtaki wakisema: "Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme." 3Pilato akamwuliza Yesu, "Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema." 4Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, "Sioni kosa lolote katika mtu huyu." 5Lakini wao wakasisitiza wakisema: "Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa." 6Pilato aliposikia hayo, akauliza, "Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?" 7Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu. 8Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza. 9Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno. 10Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana. 11Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato. 12Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki. 13Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu, 14akawaambia, "Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake. 15Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo. 16Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia."ff mmoja. 17missing 18Lakini wote wakapiga kelele pamoja: "Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!" 19Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.) 20Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena; 21lakini wao wakapiga kelele: "Msulubishe, msulubishe!" 22Pilato akawaambia mara ya tatu, "Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie." 23Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda. 24Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe. 25Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka. 26Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. 27Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. 28Yesu akawageukia, akasema, "Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. 29Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: `Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!` 30Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: `Tuangukieni!` na vilima, `Tufunikeni!` 31Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?" 32Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. 33Walipofika mahali paitwapo, "Fuvu la Kichwa," ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. 34Yesu akasema, "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya." Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. 35Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: "Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!" 36Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki 37wakisema: "Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe." 38Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: "Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi." 39Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: "Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia." 40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: "Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo. 41Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya." 42Kisha akasema, "Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako." 43Yesu akamwambia, "Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi." 44Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa, 45na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka vipande viwili. 46Yesu akalia kwa sauti kubwa: "Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako." Alipokwisha sema hayo, akakata roho. ic 47Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: "Hakika huyu alikuwa mtu mwema." 48Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. 49Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo. 50Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika; 51Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao. 52Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. 53Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika. 54Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza. 55Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa 56Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi kuyapaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.

Chapter 24

1Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha. 2Walikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi. 3Walipoingia ndani, hawakuona mwili wa Bwana Yesu. 4Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kung`aa sana, wakasimama karibu nao. 5Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, "Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? 6Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya: 7`Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha, na siku ya tatu atafufuka."` 8Hapo wanawake wakayakumbuka maneno yake, 9wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wengine habari za mambo hayo yote. 10Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. 11Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini. 12Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea. 13Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. 14Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. 15Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. 16Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. 17Akawauliza, "Mnazungumza nini huku mnatembea?" Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. 18Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, "Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?" 19Naye akawajibu, "Mambo gani?" Wao wakamjibu, "Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. 20Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. 21Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. 22Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, 23wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. 24Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona." 25Kisha Yesu akawaambia, "Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? 26Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?" 27Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. 28Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; 29lakini wao wakamsihi wakisema, "Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia." Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. 30Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. 31Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. 32Basi, wakaambiana, "Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?" 33Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika 34wakisema, "Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni." 35Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate. 36Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia "Amani kwenu." 37Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. 38Lakini yeye akawaambia, "Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? 39Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo." 40Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu. 41Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, "Mnacho chakula chochote hapa?" 42Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. 43Akakichukua, akala, wote wakimwona. 44Halafu akawaambia, "Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi." 45Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. 46Akawaambia, "Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu, 47na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi. 48Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo. 49Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu." 50Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki. 51Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. 52Wao wakamwabudu, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: 53wakakaa muda wote Hekaluni wakimsifu Mungu.

John

Chapter 1

1Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. 3Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. 4Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. 5Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. 6Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, 7ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. 8Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. 9Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. 10Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. 11Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. 12Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu. 13Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao. 14Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. 15Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: `Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."` 16Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo. 17Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo. 18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. 19Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?" 20Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye Kristo." 21Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!" 22Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma." 23Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: `Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."` 24Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. 25Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?" 26Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. 27Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake." 28Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng`ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza. 29Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye niliyesema juu yake: `Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!` 31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua." 32Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. 33Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: `Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.` 34Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu." 35Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. 36Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu." 37Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. 38Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?" 39Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni. 40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. 41Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo). 42Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.") 43Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate." 44Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro. 45Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti." 46Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone." 47Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake." 48Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona." 49Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!" 50Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya." 51Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu."

Chapter 2

1Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo, 2naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. 3Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!" 4Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado." 5Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni." 6Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha. 7Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu. 8Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu." 9Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi, 10akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!" 11Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini. 12Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache. 13Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu. 14Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng`ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao. 15Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng`ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao. 16Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!" 17Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua." 18Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?" 19Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu." 20Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?" 21Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake. 22Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu. 23Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya. 24Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote. 25Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.

Chapter 3

1Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo. 2Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye." 3Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu." 4Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!" 5Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. 6Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. 7Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. 8Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho." 9Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?" 10Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya? 11Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu. 12Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni? 13Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni. 14"Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo, 15ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele. 16Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu. 18"Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu. 19Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. 20Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. 21Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu." 22Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu. 23Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza. 24Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.) 25Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha. 26Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng`ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea." 27Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu. 28Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: `Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!` 29Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa. 30Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue. 31"Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote. 32Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake. 33Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli. 34Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo. 35Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote. 36Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."

Chapter 4

1Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane. 2Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.) 3Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya; 4na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria. 5Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. 6Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. 7Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe." 8(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) 9Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.) 10Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: `Nipatie maji ninywe,` ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai." 11Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai? 12Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki." 13Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele." 15Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji." 16Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa." 17Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume. 18Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli." 19Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii. 20Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu." 21Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka. 24Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake." 25Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu." 26Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye." 27Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?" 28Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu, 29"Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?" 30Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu. 31Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula." 32Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi." 33Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?" 34Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake. 35Ninyi mwasema: `Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!` Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa. 36Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. 37Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: `Mmoja hupanda na mwingine huvuna.` 38Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao." 39Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya." 40Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. 41Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake. 42Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu." 43Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. 44Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi yake." 45Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. 46Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. 47Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. 48Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!" 49Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa." 50Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake. 51Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. 52Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha." 53Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. 54Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.

Chapter 5

1Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu. 2Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao. 3Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza.fa 4missing 4maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao. 5Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. 6Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?" 7Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia." 8Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee." 9Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato. 10Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako." 11Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: `Chukua mkeka wako, tembea."` 12Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: `Chukua mkeka wako, tembea,` ni nani?" 13Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu. 14Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi." 15Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya. 16Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu. 17Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi." 18Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu. 19Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile. 20Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu. 21Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana, 23ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma. 24"Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima. 25Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi. 26Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa asili ya uhai. 27Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu. 28Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, 29nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa. 30"Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. 31Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. 32Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. 33Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. 34Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. 35Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. 36Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. 37Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, 38na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. 39Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! 40Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima. ic 41"Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. 42Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. 44Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? 45Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. 46Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu yangu. 47Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?"

Chapter 6

1Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au Ziwa Tiberia). 2Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. 3Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. 4Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. 5Basi, Yesu na alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?" 6Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) 7Filipo akamjibu, "Mikate ya denari mia mbili za fedha haiwatoshi watu hawa hata kama ila mmoja atapata kipande kidogo tu!" 8Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, 9"Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?" 10Yesu akasema, "Waketisheni watu." Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano. 11Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. 12Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee." 13Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. 14Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, "Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni." 15Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake. ic 16Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani, 17wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado. 18Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. 20Yesu akawaambia, "Ni mimi, msiogope!" 21Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walipokuwa wanakwenda. 22Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao. 23Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu. 24Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta. 25Wale watu walipomkuta Yesu ng`ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, "Mwalimu, ulifika lini hapa?" 26Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho." 28Wao wakamwuliza, "Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?" 29Yesu akawajibu, "Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule aliyemtuma." 30Hapo wakamwambia, "Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani? 31Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: `Aliwalisha mkate kutoka mbinguni."` 32Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni. 33Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uzima." 34Basi, wakamwambia, "Mheshimiwa, tupe daima mkate huo." 35Yesu akawaambia, "Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe. 36Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. 37Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu, 38kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. 39Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho. 40Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho." 41Basi, Wayahudi wakaanza kunung`unika kwa kuwa alisema: "Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni." 42Wakasema, "Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?" 43Yesu akawaambia, "Acheni kunung`unika ninyi kwa ninyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho. 45Manabii wameandika: `Watu wote watafundishwa na Mungu.` Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. 46Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. 47Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele. 48Mimi ni mkate wa uzima. 49Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. 50Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa. 51Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu." 52Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: 53Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu. 54Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake. 57Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu. 58Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zetu, wakafa. Aulaye mkate huu ataishi milele." 59Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu. 60Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, "Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?" 61Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung`unika juu ya jambo hilo, akawauliza, "Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka? 62Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza? 63Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi. Maneno niliyowaambieni ni Roho, ni uzima. 64Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini." (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.) 65Kisha akasema, "Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu." 66Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane naye tena. 67Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, "Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?" 68Simoni Petro akamjibu, "Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele. 69Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu." 70Yesu akawaambia, "Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!" 71Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.

Chapter 7

1Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumwua. 2Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 3Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya. 4Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu." 5Hata ndugu zake hawakumwamini!) 6Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa. 7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu. 8Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika." 9Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya. 10Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. 11Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: "Yuko wapi?" 12Kulikuwa na minong`ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, "Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu." 13Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. 14Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha. 15Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?" 16Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. 17Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. 18Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. 19Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?" 20Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?" 21Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. 22Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. 23Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? 24Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki." 25Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? 26Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? 27Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!" 28Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. 29Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma." 30Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. 31Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, "Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?" 32Mafarisayo waliwasikia watu wakinong`ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. 33Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. 34Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika." 35Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? 36Ana maana gani anaposema: `Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?"` 37Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe. 38Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: `Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!"` 39Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.) 40Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!" 41Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? 42Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: `Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!"` 43Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. 44Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. 45Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, "Kwa nini hamkumleta?" 46Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!" 47Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika? 48Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? 49Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!" 50Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, 51"Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?" 52Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!" [[[ 53Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake;

Chapter 8

1lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni. 2Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha. 3Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao. 4Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. 5Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?" 6Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. 7Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe." 8Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. 9Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. 10Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?" 11Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena."]fb mahali pengine. 12Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima." 13Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali." 14Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. 15Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu. 16Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali. 18Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia." 19Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia." 20Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. 21Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi,ninyi hamwezi kufika." 22Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: `Niendako ninyi hamwezi kufika?"` 23Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 24Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba `Mimi ndimi`, mtakufa katika dhambi zenu." 25Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo! 26Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake." 27Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba. 28Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba `Mimi ndimi`, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha. 29Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza." 30Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini. 31Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. 32Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru." 33Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: `mtakuwa huru?"` 34Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. 36Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. 37Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu. 38Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu." 39Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu, 40Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo! 41Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu." 42Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu. 44Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo. 45Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini. 46Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini? 47Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu." 48Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?" 49Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu. 50Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu. 51Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele." 52Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, `Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!` 53Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?" 54Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza. 55Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake. 56Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi." 57Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?" 58Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko." 59Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.

Chapter 9

1Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa. 2Basi, wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?" 3Yesu akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake. 4Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi. 5Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu." 6Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni, 7akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina hili ni "aliyetumwa"). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona. 8Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?" 9Baadhi yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana naye." Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!" 10Basi, wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?" 11Naye akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: `Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.` Basi, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona." 12Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi sijui!" 13Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo. 14Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato. 15Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia, "Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona." 16Baadhi ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao. 17Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!" 18Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake. 19Basi, wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?" 20Wazazi wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu. 21Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe." 22Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi. 23Ndiyo maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni." 24Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi." 25Yeye akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona." 26Basi, wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?" 27Huyo mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?" 28Lakini wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose. 29Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!" 30Naye akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu! 31Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake. 32Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. 33Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!" 34Wao wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali. 35Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, "Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?" 36Huyo mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini." 37Yesu akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa." 38Basi, huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia. 39Yesu akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu." 40Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, "Je, sisi pia ni vipofu?" 41Yesu akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi mwasema: `Sisi tunaona`, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.

Chapter 10

1Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang`anyi. 2Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. 3Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje. 4Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. 5Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake." 6Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. 7Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. 8Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang`anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. 9Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. 10Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili. 11"Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. 12Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya. 13Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. 14Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, 15kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. 16Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. 17"Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. 18Hakuna mtu anayeninyang`anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye." 19Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. 20Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?" 21Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?" 22Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. 23Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. 24Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi." 25Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. 26Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu. 27Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. 28Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. 29Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. 30Mimi na Baba, tu mmoja." 31Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. 32Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?" 33Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu." 34Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: `Mimi nimesema, ninyi ni miungu?` 35Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. 36Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: `Unakufuru`, eti kwa sababu nilisema: `Mimi ni Mwana wa Mungu?` 37Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini. 38Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake." 39Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. 40Yesu akaenda tena ng`ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. 41Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa." 42Watu wengi mahali hapo wakamwamini.

Chapter 11

1Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. 2Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.) 3Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!" 4Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe." 5Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. 6Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. 7Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!" 8Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?" 9Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. 10Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake." 11Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha." 12Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona." 13Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. 14Basi, Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa; 15Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake." 16Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe pamoja naye!" 17Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. 18Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu. 19Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao. 20Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. 21Martha akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! 22Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa." 23Yesu akamwambia, "Kaka yako atafufuka." 24Martha akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho." 25Yesu akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi: 26na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?" 27Martha akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni." 28Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, "Mwalimu yuko hapa, anakuita." 29Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu. 30Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki. 31Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza. 32Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!" 33Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni. 34Kisha akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone." 35Yesu akalia machozi. 36Basi, Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!" 37Lakini baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?" 38Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe. 39Yesu akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!" 40Yesu akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?" 41Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, "Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza. 42Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma." 43Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: "Lazaro! Toka nje!" 44Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, "Mfungueni, mkamwache aende zake." 45Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini. 46Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu. 47kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. 48Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!" 49Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu! 50Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?" 51Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao; 52na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika. 53Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu. 54Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. 55Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo. 56Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?" 57Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.

Chapter 12

1Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. 2Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. 3Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. 4Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, 5"Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?" 6Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. 7Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. 8Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote." ic 9Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. 10Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, 11Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu. 12Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. 13Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli." 14Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko: 15"Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda." 16Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. 17Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia. 18Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. 19Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata." 20Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. 21Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu." 22Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. 23Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! 24Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. 25Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele. 26Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima. 27"Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: `Baba, usiruhusu saa hii inifikie`? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii. 28Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena." 29Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!" 30Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. 31Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. 32Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu." 33Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani). 34Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?" 35Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. 36Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. 37Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. 38Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?" 39Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema: 40"Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya." 41Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. 42Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. 43Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu 44Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. 45Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. 46Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. 47Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. 48Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. 49Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. 50Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."

Chapter 13

1Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho! 2Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu. 3Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. 4Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. 5Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. 6Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?" 7Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye." 8Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena." 9Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia." 10Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote." 11Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.") 12Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? 13Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. 14Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. 15Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. 16Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma. 17Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza. 18"Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: `Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.` 19Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi. 20Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma." 21Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!" 22Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani. 23Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu. 24Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani." 25Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?" 26Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. 27Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!" 28Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo. 29Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini. 30Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku. 31Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara. 33"Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: `Niendako ninyi hamwezi kwenda!` 34Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. 35Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu." 36Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye." 37Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!" 38Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"

Chapter 14

1Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. 2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. 3Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. 4Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda." 5Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?" 6Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. 7Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona." 8Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka." 9Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: `Tuonyeshe Baba?` 10Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. 11Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. 12Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba. 13Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. 14Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni. 15"Mkinipenda mtazishika amri zangu. 16Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. 17Yeye ni Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu. 18"Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu. 19Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. 20Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu. 21Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake." 22Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?" 23Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. 24Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma. 25"Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi 26lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. 27"Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. 28Mlikwisha sikia nikiwaambieni: `Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.` Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. 29Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. 30Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; 31lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!"

Chapter 15

1"Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. 4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. ic 5"Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. 6Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. 7Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. 8Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. 9Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. 10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike. 12Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. 13Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu. 17Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni. 18"Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. 19Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. 20Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. 21Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma. 22Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi. 23Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. 24Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia. 25Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: `Wamenichukia bure!` 26"Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.

Chapter 16

1"Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu. 2Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu. 3Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi. 4Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi. 5Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: `Unakwenda wapi?` 6Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. 7Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. 8Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu. 9Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; 10kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena; 11kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa. 12"Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. 13Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja. 14Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 15Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 16"Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!" 17Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?` Tena anasema: `Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"` 18Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: `Bado kitambo kidogo?` Hatuelewi anaongelea nini." 19Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?` 20Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani. 22Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. 23Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni. 24Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike. 25"Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. 26Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; 27maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba." 29Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo. 30Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu." 31Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa? 32Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami. 33Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!"

Chapter 17

1Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, "Baba, saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza. 2Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wote hao uliompa. 3Na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma. 4Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa nifanye. 5Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu. 6"Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako. 7Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako. 8Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma. 9"Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea hao ulionipa, maana ni wako. 10Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana ndani yao. 11Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja. 12Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule aliyelazimika kupotea ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia. 13Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu. 14Mimi nimewapa neno lako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 15Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu. 16Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 17Waweke wakfu kwa ukweli; neno lako ni ukweli. 18Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni; 19na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli. 20"Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao. 21Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. 22Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja; 23mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi. 24"Baba! Nataka wao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu. 25Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma. 26Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao."

Chapter 18

1Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng`ambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake. 2Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko. 3Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha. 4Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, "Mnamtafuta nani?" 5Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu akawaambia, "Mimi ndiye." Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao. 6Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi nyuma, wakaanguka chini. 7Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?" Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" 8Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao." 9Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: "Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.") 10Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa Kuhani Mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko. 11Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe alichonipa Baba?" 12Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga 13na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo. 14Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa. 15Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu. 16Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani. 17Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si mimi!" 18Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. 19Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake. 20Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na Hekaluni, mahali wakutanikiapo Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri. 21Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua nilivyosema." 22Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?" 23Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?" 24Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani Mkuu Kayafa. 25Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, "Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema, "Si mimi!" 26Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?" 27Petro akakana tena; mara jogoo akawika. 28Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa najisi. 29Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?" 30Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako." 31Pilato akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na Sheria yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote." 32Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa kifo gani.) 33Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?" 34Yesu akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia habari zangu?" 35Pilato akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?" 36Yesu akamjibu, "Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa." 37Hapo Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu, "Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli hunisikiliza." 38Pilato akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia yoyote kwake. 39Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?" 40Hapo wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba alikuwa mnyang`anyi.

Chapter 19

1Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko. 2Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau. 3Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: "Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!" Wakampiga makofi. 4Pilato akatoka tena nje, akawaambia, "Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake." 5Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, "Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo." 6Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaaza sauti: "Msulubishe! Msulubishe!" Pilato akawaambia, "Mchukueni basi, ninyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake." 7Wayahudi wakamjibu, "Sisi tunayo Sheria, na kufuatana na Sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu." 8Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa. 9Basi, akaingia tena ndani ya ikulu, akamwuliza Yesu, "Umetoka wapi wewe?" Lakini Yesu hakumjibu neno. 10Hivyo Pilato akamwambia, "Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?" 11Yesu akamjibu, "Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi." 12Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: "Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa Mfalme humpinga Kaisari!" 13Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo: "Sakafu ya Mawe" (kwa Kiebrania, Gabatha). 14Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, "Tazameni, Mfalme wenu!" 15Wao wakapaaza sauti: "Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!" Makuhani wakuu wakajibu, "Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!" 16Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu. 17Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo "Fuvu la Kichwa", (kwa Kiebrania Golgotha). 18Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. 19Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: "Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi." 20Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. 21Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, "Usiandike: `Mfalme wa Wayahudi`, ila `Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi."` 22Pilato akajibu, "Niliyoandika, nimeandika!" 23Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. 24Basi, hao askari wakashauriana: "Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani." Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: "Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura." Basi, ndivyo walivyofanya hao askari. ic 25Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. 26Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: "Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao." 27Halafu akamwambia yule mwanafunzi: "Tazama, huyo ndiye mama yako." Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake. 28Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, "Naona kiu." 29Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. 30Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, "Yametimia!" Kisha akainama kichwa, akatoa roho. 31Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe. 32Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. 33Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu. 34Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. 35Naye aliyeona tukio hilo ametoa habari zake ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli.) 36Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: "Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa." 37Tena Maandiko mengine yanasema: "Watamtazama yule waliyemtoboa." 38Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Armathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu. 39Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini. 40Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika. 41Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. 42Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.

Chapter 20

1Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. 2Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka." 3Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. 4Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. 6Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda, 7na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. 8Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini. 9Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu). 10Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani. 11Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini, 12akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. 13Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini unalia?" Naye akawaambia, "Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!" 14Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu. 15Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?" Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, "Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua." 16Yesu akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, "Raboni" (yaani "Mwalimu"). 17Yesu akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu." 18Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo. 19Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, "Amani kwenu!" 20Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana. 21Yesu akawaambia tena, "Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi." 22Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, "Pokeeni Roho Mtakatifu. 23Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi." 24Thoma mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. 25Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, "Tumemwona Bwana." Thoma akawaambia, "Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki." 26Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, "Amani kwenu!" 27Kisha akamwambia Thoma, "Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!" 28Thoma akamjibu, "Bwana wangu na Mungu wangu!" 29Yesu akamwambia, "Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini." 30Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki. 31Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uzima kwa nguvu ya jina lake.

Chapter 21

1Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi: 2Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja. 3Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote. 4Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye. 5Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu." 6Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki. 7Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini. 8Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja kutoka ukingoni. 9Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate. 10Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua." 11Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika. 12Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana. 13Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki. 14Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu. 15Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu." 16Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu." 17Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu! 18Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda." 19(Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate." 20Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?") 21Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?" 22Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi." 23Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?" 24Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli. 25Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.

Acts

Chapter 1

1Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake 2mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. 4Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: "Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. 5Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu." 6Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, "Je Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?" 7Lakini Yesu akawaambia, "Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. 8Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia." 9Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena. 10Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, 11wakasema, "Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni." 12Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. 13Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake. 15Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao, 16akasema, "Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. 17Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu. 18"Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. 19Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba `Hekeli Dama`, maana yake, `Shamba la Damu.`) 20Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: `Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake.` Tena imeandikwa: `Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.` 21Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu. Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni." 22[] 23Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. 24Kisha wakasali: "Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe." 26Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.

Chapter 2

1Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja. 2Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. 3Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. 4Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. 5Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. 6Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7Walistaajabu na kushangaa, wakisema, "Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? 8Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? 9Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, 10Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, 11Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu." 12Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, "Hii ina maana gani?" 13Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, "Watu hawa wamelewa divai mpya!" 14Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: "Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. 15Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? 16Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: 17`Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. 18Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu. 19Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; 20jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. 21Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.` 22"Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. 23Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. 24Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge. 25Maana Daudi alisema juu yake hivi: `Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika. 26Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini; 27kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. 28Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako kwanijaza furaha!` 29"Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo. 30Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake. 31Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: `Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.` 32Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. 33Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho. 34Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: `Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, 35hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.` 36"Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo." 37Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: "Ndugu zetu, tufanye nini?" 38Petro akajibu, "Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya Roho Mtakatifu. 39Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake." 40Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, "Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu." 41Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo. 42Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kidugu, kumega mkate na kusali. 43Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu. 44Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja. 45Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja. 46Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu. 47Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.

Chapter 3

1Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala. 2Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao "Mlango Mzuri", palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia Hekaluni. 3Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe chochote. 4Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, "Tutazame!" 5Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. 6Kisha Petro akamwambia, "Sina fedha wala dhahabu lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!" 7Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. 8Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. 9Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. 10Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule "Mlango Mzuri" wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata. 11Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa "Ukumbi wa Solomoni," ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. 12Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, "Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea? 13Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru. 14Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe. 15Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo. 16Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote. 17"Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu. 18Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke. 19Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu. 20Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu. 21Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani. 22Kwa maana Mose alisema, `Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe. 23Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.` 24Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi. 25Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: `Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.` 26Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake."

Chapter 4

1Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na Masadukayo *walifika. 2Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba wafu watafufuka. 3Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. 4Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu elfu tano. 5Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Sheria, walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. 6Walikutana pamoja na Anasi, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa Kuhani Mkuu. 7Waliwasimamisha mitume mbele yao, wakawauliza, "Ninyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?" 8Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, "Viongozi na wazee wa watu! 9Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, 10basi, ninyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye ninyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka wafu. 11Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: `Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.` 12Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye." 13Hao wazee wa baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. 14Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. 15Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. 16Wakaulizana, "Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba mwujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. 17Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu." 18Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. 19Lakini Petro na Yohane wakawajibu, "Amueni ninyi wenyewe kama ni haki mbele ya Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii yeye. 20Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia." 21Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. 22Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arobaini. 23Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. 24Waliposikia habari hiyo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, "Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo! 25Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, babu yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: `Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? 26Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, ili kumwasi Bwana na Kristo wake.` 27"Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye umemtia mafuta. 28Naam, walikutana ili wafanye yale ambayo ulikusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. 29Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. 30Nyosha mkono wako uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu." 31Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila uoga. 32Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. 33Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. 34Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza 35na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. 36Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita jina Barnaba (maana yake, "Mtu mwenye kutia moyo"). 37Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Chapter 5

1Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vilevile. 2Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume. 3Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? 4Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!" 5Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana. 6Vijana wakafika wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje, wakamzika. 7Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani. 8Petro akamwambia, "Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?" Yeye akamjibu, "Naam, ni kiasi hicho." 9Naye Petro akamwambia, "Mbona mmekula njama kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako, sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia." 10Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia, walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake. 11Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana. 12Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni. 13Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu. 14Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi. 15Kwa sababu hiyo, watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kando kando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa. 17Kisha, Kuhani Mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu. 18Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu. 19Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia, 20"Nendeni mkasimame Hekaluni na kuwaambia watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya." 21Mitume walitii, wakaingia Hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani Mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu, yaani halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume. 22Lakini hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi, wakatoa taarifa mkutanoni, 23wakisema, "Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani." 24Mkuu wa walinzi wa Hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi, wasijue yaliyowapata. 25Akafika mtu mmoja, akawaambia, "Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo Hekaluni, wanawafundisha watu." 26Hapo mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na watu wake walikwenda Hekaluni, akawaleta. Lakini hawakuwakamata kwa kutumia nguvu, maana waliogopa kwamba watu wangewapiga mawe. 27Basi, wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani Mkuu akawaambia, 28"Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo." 29Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, "Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu. 30Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani. 31Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao. 32Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo." 33Wajumbe wote wa lile Baraza waliposikia hayo, wakawaka hasira, hata wakaamua kuwaua. 34Lakini Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa Sheria na aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi. 35Kisha akawaambia wale wajumbe wa Baraza, "Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa! 36Zamani kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na watu karibu mia nne wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote wakatawanyika na kikundi chake kikafa. 37Tena, baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye, aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake wakatawanyika. 38Na sasa pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa maana, ikiwa mpango huu au shughuli hii yao imeanzishwa na binadamu, itatoweka yenyewe. 39Lakini kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta mnapigana na Mungu." Basi, wakakubaliana naye. 40Hivyo wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao. 41Basi, mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri wakiwa wamejaa furaha, kwani walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu. 42Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo, Hekaluni na nyumbani mwa watu.

Chapter 6

1Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung`uniko kati ya wanafunzi waliosema Kigiriki na wale waliosema Kiebrania. Wale waliosema Kigiriki walinung`unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku. 2Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, "Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji. 3Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo. 4Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu." 5Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujawa na Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanora, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye hapo awali alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi. 6Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono. 7Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani. 8Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu. 9Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa "Sunagogi la Watu Huru", nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia. 10Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyeongoza maneno yake. 11Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: "Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu." 12Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na walimu wa Sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza kuu. 13Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, "Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na Sheria ya Mose. 14Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose." 15Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.

Chapter 7

1Basi, Kuhani Mkuu akamwuliza, "Je, mambo haya ni kweli?" 2Naye Stefano akasema, "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea baba yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani. 3Mungu alimwambia: `Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonyesha!` 4Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa. 5Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidia kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto. 6Mungu alimwambia hivi: `Wazao wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka mia nne. 7Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.` 8Halafu Mungu aliifanya tohara iwe ishara ya agano. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka, siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo. 9"Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamuuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme. 11Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote. 12Basi, Yakobo alipopata habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza. 13Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu. 14Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na tano, waje Misri. 15Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa. 16Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi Abrahamu alilonunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha. 17"Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi. 18Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri. 19Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe. 20Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu, 21na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake. 22Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo. 23"Alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli. 24Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. 25Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo.) 26Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha, akisema: `Ninyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya ninyi kwa ninyi?` 27Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: `Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu? 28Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?` 29Baada ya kusikia hayo Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili. 30"Miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai. 31Mose alistaajabu sana kuona jambo hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana: 32`Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!` Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi. 33Bwana akamwambia: `Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu. 34Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.` 35"Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: `Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?` Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi. 36Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa muda wa miaka arobaini. 37Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: `Mungu atawateulieni nabii kama mimi kutoka katika ndugu zenu ninyi wenyewe.` 38Wakati watu wa Israeli walipokutana pamoja kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko pamoja nao. Alikuwa huko pamoja na babu zetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai; ndiye aliyekabidhiwa yale maneno yaletayo uzima atupe sisi. 39"Lakini yeye ndiye babu zetu waliyemkataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri. 40Walimwambia Aroni: `Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata Mose huyu aliyetuongoza kutoka Misri!` 41Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe. 42Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii: `Enyi watu wa Israeli! Si mimi mliyenitolea dhabihu na sadaka kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani! 43Ninyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki, na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani. Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu. Kwa sababu hiyo nitakupeleka mateka mbali kupita Babuloni!` 44Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema lililoshuhudia kuweko kwa Mungu. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichoonyeshwa. 45Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi. 46Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo. 47Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba. 48"Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo: 49`Bwana asema: Mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu. 50Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea, na ni mahali gani nitakapopumzika? Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?` 51"Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Ninyi ni kama baba zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu. 52Je, yuko nabii yeyote ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, ninyi mmemsaliti, mkamuua. 53Ninyi mliipokea ile Sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii." 54Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira. 55Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia wa Mungu. 56Akasema, "Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu." 57Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja, 58wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo. 59Waliendelea kumpiga mawe Stefano, huku akiwa anasali: "Bwana Yesu, ipokee roho yangu!" 60Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: "Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii." Baada ya kusema hivyo, akafa.

Chapter 8

1Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua Stefano kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria. 2Watu wamchao Mungu, walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa. 3Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani. 4Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe. 5Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo. 6Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya. 7Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa. 8Kukawa na furaha kubwa katika mji ule. 9Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu. 10Watu wote, wadogo na wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, "Simoni ndiye ile nguvu ya kimungu inayoitwa `Nguvu Kubwa."` 11Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu. 12Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume. 13Hata Simoni aliamini; baada ya kubatizwa ilikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika. 14Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma kwao Petro na Yohane. 15Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu; 16maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa ameshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu. 17Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu. 18Hapo Simoni aling`amua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema, 19"Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu." 20Lakini Petro akamjibu, "Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! 21Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu. 22Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo. 23Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na mfungwa wa dhambi!" 24Simoni akajibu, "Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema." 25Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria. 26Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, "Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza." (Njia hiyo hupita jangwani.) 27Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa ofisa maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa. 28Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya. 29Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, "Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo." 30Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, "Je, unaelewa hayo unayosoma?" 31Huyo mtu akamjibu, "Ninawezaje kuelewa bila mtu kunielewesha?" Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye. 32Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii: "Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa; kimya kama vile mwana kondoo anaponyolewa manyoya, yeye naye hakutoa sauti hata kidogo. 33Alifedheheshwa na kunyimwa haki. Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake, kwa maana maisha yake yameondolewa duniani." 34Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, "Niambie, huyu nabii anasema juu ya nani? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?" 35Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu. 36Walipokuwa bado wanaendelea na safari walifika mahali penye maji na huyo ofisa akasema, "Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?"fa 37missing 38Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo ofisa wakashuka majini, naye Filipo akambatiza. 39Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo Mwethiopia hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake akiwa amejaa furaha. 40Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Habari Njema mpaka alipofika Kaisarea. kubatizwa." Naye akajibu, "Naam, ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu."

Chapter 9

1Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu, 2akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu. 3Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote. 4Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: "Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?" 5Naye Saulo akauliza, "Ni nani wewe Bwana?" Na ile sauti ikajibu, "Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. 6Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya." 7Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu. 8Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko. 9Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote. 10Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, "Anania!" Anania akaitika, "Niko hapa, Bwana." 11Naye Bwana akamwambia, "Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali; 12na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena." 13Lakini Anania akajibu, "Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu. 14Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako." 15Lakini Bwana akamwambia, "Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli. 16Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu." 17Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, "Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu." 18Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa. 19Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko. 20Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. 21Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!" 22Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa. 23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumwua Saulo. 24Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumwua. 25Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani. ic 26Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa, na hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi. 27Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila uoga kule Damasko. 28Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu. 29Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wasemao Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua. 30Wale ndugu walipogundua jambo hilo walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso. 31Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu. 32Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda. 33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Enea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza. 34Basi, Petro akamwambia, "Enea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako." Enea akaamka mara. 35Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Enea, na wote wakamgeukia Bwana. 36Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima. 37Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakauzika katika chumba ghorofani. 38Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: "Njoo kwetu haraka iwezekanavyo." 39Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonyesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai. 40Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akamgeukia yule maiti, akasema, "Tabitha, amka" Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima. 42Habari ya tukio hili ilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana. 43Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni.

Chapter 10

1Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, Jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho "Kikosi cha Italia." 2Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. 3Yapata saa tisa mchana, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, "Kornelio!" 4Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, "Kuna nini Mheshimiwa?" Huyo malaika akamwambia, "Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini. 5Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 6Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari." 7Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, 8akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa. 9Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. 10Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, alipatwa na usingizi mzito akaona maono. 11Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. 12Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. 13Akasikia sauti ikimwambia: "Petro, amka uchinje, ule!" 14Petro akajibu, "La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu." 15Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: "Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!" 16Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni. 17Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hilo maono alilokuwa ameliona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, 18Wakaita kwa sauti: "Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?" 19Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa lile maono, na hapo Roho akamwambia, "Sikiliza! kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. 20Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma." 21Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, "Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?" 22Wao wakamjibu, "Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema." 23Petro akawaalika ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye. 24Siku ya pili yake, walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika. 25Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa. 26Lakini Petro alimwinua, akamwambia, "Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu." 27Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika. 28Petro akawaambia, "Ninyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na Sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu. 29Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: kwa nini mmeniita?" 30Kornelio akasema, "Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kun`gaa alisimama mbele yangu, 31akasema: `Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini vimekubaliwa na Mungu. 32Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petroi; yuko nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi karibu na bahari.` 33Kwa hiyo nilikutumia ujumbe bila kuchelewa, nawe umefanya vyema kuja. Sasa, sisi tuko mbele ya Mungu, kusikiliza chochote ambacho bwana amekuamuru kusema." 34Hapo Petro akaanza kusema: "Sasa nimetambua kwamba hakika Mungu hana ubaguzi. 35Mtu wa taifa lolote anayemcha Mungu na kutenda haki anapokelewa naye. 36Huu ndio ule ujumbe Mungu alioupeleka kwa watu wa Israeli, akitangaza Habari Njema iletayo amani kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote. 37Ninyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. 38Mnajua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi. 39Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; 40lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane 41si kwa watu wote ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka wafu. 42Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa wazima na wafu. 43Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake." 44Wakati Petro alipokuwa bado anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanasikiliza ujumbe huo. 45Wale Wayahudi waumini waliokuja pamoja na Petro kutoka Yopa walishangaa kuona kuwa Mungu aliwamiminia zawadi ya Roho Mtakatifu watu wa mataifa mengine pia; 46maana waliwasikia wakiongea kwa lugha mbalimbali wakimtukuza Mungu. Hapo Petro akasema, 47"Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi wenyewe tulivyompokea. Je, kuna yeyote atakayeweza kuwazuia wasibatizwe kwa maji?" 48Basi, akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae nao kwa siku chache.

Chapter 11

1Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. 2Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: 3"Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! 4Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: 5"Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu. 6Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. 7Kisha nikasikia sauti ikiniambia: `Petro amka, chinja, ule.` 8Lakini mimi nikasema: `La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.` 9Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: `Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.` 10Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. 11Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa. 12Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. 13Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: `Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 14Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.` 15Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. 16Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: `Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.` 17Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?" 18Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!" 19Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. 20Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu. 21Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. 22Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. 24Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. 25Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo 26Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. ic 27Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. 28Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala). 29Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. 30Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo.

Chapter 12

1Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa baadhi ya Wakristo. 2Alimwua kwa upanga Yakobo ndugu yake Yohane. 3Alipoona kuwa kitendo hiki kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu.) 4Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka. 5Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo. 6Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza. 7Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa akisema, "Amka upesi!" Mara ile minyororo ikaanguka kutoka katika mikono yake. 8Malaika akamwambia, "Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako." Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, "Vaa koti lako, unifuate." 9Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto. 10Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake. 11Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, "Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa kutoka katika mkono wa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia." 12Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali. 13Petro alibisha mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia. 14Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni. 15Wakamwambia yule msichana, "Una wazimu!" Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, "Huyo ni malaika wake." 16Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa. 17Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine. 18Kulipokucha, ulitokea wasiwasi mkubwa kati ya wale askari kuhusu yaliyokuwa yamempata Petro. 19Herode aliamuru ufanywe msako lakini hawakuweza kumpata. Hivyo aliamuru wale askari wahojiwe, akatoa amri wauawe. Halafu akatoka huko Yudea akaenda Kaisarea ambako alikaa. 20Herode alikasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Lakini wao walimpelekea wajumbe. Nao wakafaulu kwanza kumpata Blasto awe upande wao. Blasto alikuwa msimamizi mkuu wa ikulu ya mfalme. Kisha, wakamwendea Herode wakamwomba kuwe na amani, kwa maana nchi yao ilitegemea nchi ya mfalme kwa chakula. 21Siku moja iliyochaguliwa, Herode akiwa amevaa mavazi rasmi na kuketi katika kiti cha kifalme aliwahutubia watu. 22Wale watu walimpigia kelele za shangwe wakisema, "Hii ni sauti ya mungu, si ya mtu." 23Papo hapo malaika wa Bwana akamwangusha Herode chini kwa sababu hakumpa Mungu hizo sifa. Akaliwa na wadudu, akafa. 24Neno la Mungu likazidi kuenea na kukua. 25Baada ya Barnaba na Saulo kutekeleza shughuli zao, walitoka tena Yerusalemu wakamchukua Yohane aitwaye pia Marko.

Chapter 13

1Katika kanisa la Antiokia kulikuwa na watu wengine waliokuwa manabii na walimu; miongoni mwao akiwa Barnaba, Simoni aitwaye pia Mweusi, Lukio wa Kurene, Manaeni ambaye alikuwa amelelewa pamoja na mfalme Herode, na Saulo. 2Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema: "Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia." 3Basi, baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawawekea mikono, wakawaacha waende zao. 4Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro. 5Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao. 6Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii. 7Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu. 8Lakini huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo. 9Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi, 10akasema, "Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka. 11Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo." Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze. 12Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana. 13Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu. 14Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa. 15Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: "Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni." 16Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: "Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni! 17Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu. 18Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani. 19Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao. 20Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli. 21Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arobaini. 22Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: `Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda.` 23Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu. 24Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa. 25Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: `Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.` 26"Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. 27Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo. 28Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe. 29Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini. 30Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu. 31Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. 32Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: `Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.` 33[] 34Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: `Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.` 35Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema: `Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.` 36Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza. 37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza. 38Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo; na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya Sheria ya Mose. 39[] 40Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii: 41`Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni."` 42Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo. 43Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu. 44Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana. 45Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana. 46Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, "Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni ninyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uzima wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine. 47Maana Bwana alituagiza hivi: `Nimekuteua wewe uwe mwanga kwa mataifa, uwe njia ya wokovu kwa ulimwengu wote."` 48Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uzima wa milele, wakawa waumini. 49Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile. 50Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao. 51Basi, mitume wakayakung`uta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio. 52Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.

Chapter 14

1Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini. 2Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu. 3Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu. 4Watu wa mji huo waligawanyika: wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume. 5Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe. 6Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani, 7wakawa wanahubiri Habari Njema huko. 8Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa amelemaa miguu tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe. 9Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa, 10akasema kwa sauti kubwa, "Simama wima kwa miguu yako!" Huyo mtu aliyelemaa akainuka ghafla, akaanza kutembea. 11Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, ulianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: "Miungu imetujia katika sura za binadamu!" 12Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme. 13Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, na pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume. 14Barnaba na Paulo walipopata habari hiyo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa: 15"Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama ninyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo. 16Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda. 17Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha." 18Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie. 19Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa. 20Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe. 21Baada ya Paulo na Barnabas kuhubiri Habari Njema huko Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia Lustra na Ikonio. 22Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo wabaki imara katika imani. Wakawaambia, "Ni lazima sisi sote tupitie katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu." 23Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini, na baada ya kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye walikuwa wanamwamini. 24Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika Pamfulia. 25Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda Atalia. 26Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza. 27Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na jinsi alivyowafungulia mlango watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika imani. 28Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu.

Chapter 15

1Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, "Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo ya Sheria ya Mose, hamtaweza kuokolewa." 2Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo. 3Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote. 4Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. 5Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, "Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose." 6Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo. 7Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, "Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini. 8Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. 9Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani. 10Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba? 11Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu." 12Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine. 13Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: "Ndugu zangu, nisikilizeni! 14Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake. 15Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: 16`Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena. 17Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana. 18Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.` 19"Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu wa mataifa wanomgeukia Mungu. 20Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu. 21Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato." ic 22Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu. 23Wakawapa barua hii: mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia. 24Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu. 25Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo, 26ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika. 28Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu: 29Msile vyakula vilivyotambikiwa sanamu; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!" 30Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua. 31Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana. 32Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha. 33Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma.fb 34missing 35Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda; wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi. 36Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, "Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana tukajionee jinsi wanavyoendelea." 37Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko. 38Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao. 39Basi kukatokea ubishi mkali kati yao, na wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro. 40Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka. 41Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia akiyaimarisha makanisa.

Chapter 16

1Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. 2Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. 3Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. 4Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. 5Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku. 6Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. 7Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. 9Usiku huo, Paulo aliona ono ambalo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: "Vuka, uje Makedonia ukatusaidie." 10Mara baada ya Paulo kuona ono hilo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwapelekee Habari Njema. 11Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli. 12Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa. 13Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo. 14Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema. 15Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, "Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae." Akatuhimiza twende. 16Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake. 17Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, "Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu." 18Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, "Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!" Mara huyo pepo akamtoka. 19Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu. 20Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, "Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu. 21Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata." 22Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko. 23Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali. 24Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo. 25Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. 26Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana. 27Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua. 28Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: "Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa." 29Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu. 30Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, "Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?" 31Wao wakamjibu, "Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote." 32Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake. 33Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. 34Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu. 35Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, "Wafungueni wale watu." 36Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: "Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani." 37Lakini Paulo alimjibu, "Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie." 38Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa. 39Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule. 40Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.

Chapter 17

1Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonika ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi. 2Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akatumia Maandiko Matakatifu. 3Aliyaeleza na kuonyesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka wafu. Akawaambia, "Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo." 4Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao. 5Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani. 6Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: "Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini. 7Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti `Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu."` 8Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu. 9Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao. 10Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi. 11Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonika. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli. 12Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia. 13Lakini, Wayahudi wa Thesalonika walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu. 14Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo. 16Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu. 17Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote wale waliojitokeza. 18Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, "Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?" Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, "Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni." 19Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, "Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia. 20Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani." 21Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya. ic 22Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, "Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana. 23Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa: `Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana.` Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu. 24Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu. 25Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu. 26Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi. 27Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28Kama alivyosema mtu mmoja: `Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko!` Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: `Sisi ni watoto wake.` 29Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu. 30Mungu alifanya kama kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu. 31Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka wafu!" 32Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, "Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!" 33Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani. 34Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini. Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, mwanamke mmoja aitwaye Damari na wengineo.

Chapter 18

1Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho. 2Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona, 3na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama alivyokuwa yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi. 4Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki. 5Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo. 6Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakung`uta mavazi yake mbele yao akisema, "Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine." 7Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto. Nyumba yake Tito ilikuwa karibu na lile sunagogi. 8Lakini Krispo, mkuu wa sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa. 9Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: "Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo, 10maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu." 11Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. 12Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani. 13Wakasema, "Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na Sheria." 14Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, "Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni. 15Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina ya Sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo haya!" 16Basi, akawafukuza kutoka mahakamani. 17Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo. 18Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka. 19Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi. 20Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda. 21Bali alipokuwa anaondoka, alisema, "Mungu akipenda nitakuja kwenu tena." Akaondoka Efeso kwa meli. 22Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia. 23Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote. 24Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu. 25Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu. Akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu. 26Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo Njia ya Mungu kwa usahihi zaidi. 27Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini; 28kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.

Chapter 19

1Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa. 2Akauliza, "Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?" Nao wakamjibu, "La! Hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatujasikia." 3Naye akasema, "Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?" Wakamjibu, "Ubatizo wa Yohane." 4Naye Paulo akasema, "Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonyesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu." 5Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu. 6Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha mbalimbali na kutangaza ujumbe wa Mungu. 7Wote jumla, walikuwa watu wapatao kumi na wawili. 8Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya Ufalme wa Mungu. 9Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya hadharani juu ya Njia ya Bwana. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano. 10Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana. 11Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. 12Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. 13Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya, walisafiri huko na huko, wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: "Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri." 14Watoto saba wa Skewa, Kuhani Mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. 15Lakini pepo mbaya aliwajibu, "Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?" 16Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. 17Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. 18Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda. 19Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha elfu hamsini. 20Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi. 21Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, "Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia." 22Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia. 23Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo Njia ya Bwana. 24Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi faida kubwa. 25Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, "Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii. 26Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si tu hapa Efeso, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo. 27Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha." ic 28Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: "Mkuu ni Artemi, wa Efeso!" 29Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo. 30Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia. 31Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimtumia Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo. 32Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao. 33Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu. 34Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: "Mkuu ni Artemi wa Efeso!" Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili. 35Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, "Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni. 36Hakuna anayeweza kukana mambo haya. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari. 37Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike. 38Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko. 39Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali. 40Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo." 41Baada ya kusema hayo aliuvunja mkutano.

Chapter 20

1Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia. 2Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki. 3ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia. 4Sopatro, mwana wa Pirho kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonika, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia. 5Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa. 6Sisi, baada ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja. 7Jumamosi jioni, tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. 8Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka. 9Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. 10Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, "Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake." 11Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. 12Wale watu walimchukua yule kijana nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa. 13Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. 14Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. 15Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. 16Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana. 17Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye. 18Walipofika kwake aliwaambia, "Mnajua jinsi nilivyotumia wakati wote pamoja nanyi tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia. 19Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi. 20Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni. 21Niliwaonya wote--Wayahudi kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu. 22Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko. 23Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea. 24Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa ni kitu sana kwangu. Nataka tu nikamilishe ule utume wangu na kumaliza ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nitangaze Habari Njema ya neema ya Mungu. 25"Nimekuwa nikienda huko na huko kati yenu nikiuhubiri Ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena. 26Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote. 27Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu. 28Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae. 29Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo. 30Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu. 31Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi. 32"Na sasa basi, ninawaweka ninyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga ninyi na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake. 33Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote. 34Mnajua ninyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu. 35Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: `Heri zaidi kutoa kuliko kupokea."` 36Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali. 37Wote walikuwa wanalia; wakamwaga kwa kumkumbatia na kumbusu. 38Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.

Chapter 21

1Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rodo, na kutoka huko tulikwenda Patara. 2Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri. 3Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake. 4Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa waongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. 5Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali. 6Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli nao wakarudi makwao. 7Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja. 8Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko Kaisarea tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu. 9Alikuwa na binti watatu ambao walikuwa na kipaji cha unabii. 10Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea. 11Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema "Roho Mtakatifu asema hivi: `Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye ukanda na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa."` 12Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13Lakini yeye alijibu, "Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu." 14Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: "Mapenzi ya Bwana yafanyike" 15Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu. 16Wengine kati ya wale wafuasi wa Kaisarea walienda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa muumini kwa siku nyingi. 17Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana. 18Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwako pia. 19Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya mataifa kwa njia ya utumishi wake. 20Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, "Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanashika kwa makini Sheria ya Mose. 21Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa mengine kuwa wasiijali Sheria ya Mose, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi. 22Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa. 23Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri. 24Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya Sheria za Mose. 25Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati." 26Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia Hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu dhabihu itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao. 27Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo Hekaluni. Wakachochea hasira kati ya kundi lote la watu, wakamtia nguvuni 28wakipiga kelele: "Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga Sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine Hekaluni na kupatia najisi mahali hapa patakatifu." 29Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo mwenyeji, wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni. 30Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya Hekalu na papo hapo milango ya Hekalu ikafungwa. 31Walikuwa tayari kumuua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia. 32Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo. 33Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, "Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?" 34Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome. 35Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu. 36Kwa maana kundi kubwa la watu walimfuata wakipiga kelele, "Muulie mbali!" ic 37Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, "Naweza kukwambia kitu?" Yule mkuu wa jeshi akamjibu, "Je unajua Kigiriki? 38Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili elfu nne hadi jangwani?" 39Paulo akajibu, "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu. 40Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania.

Chapter 22

1"Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!" 2Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema, 3"Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo. 4Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani. 5Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe. 6"Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote. 7Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: `Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?` 8Nami nikauliza: `Nani wewe, Bwana?` Naye akaniambia: `Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.` 9Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami. 10Basi, mimi nikauliza: `Nifanye nini Bwana?` Naye Bwana akaniambia: `Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.` 11Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko. 12"Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko. 13Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema: `Ndugu Saulo! Ona tena.` Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia. 14Halafu Anania akasema: `Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea. 15Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia. 16Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.` 17"Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali Hekaluni, niliona maono. 18Nilimwona Bwana akiniambia: `Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.` 19Nami nikamjibu: `Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini. 20Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.` 21Naye Bwana akaniambia: `Nenda; ninakutuma mbali kwa mataifa mengine."` 22Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, "Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi." 23Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani. 24Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele. 25Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, "Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?" 26Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, "Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!" 27Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, "Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?" Paulo akamjibu, "Naam." 28Mkuu wa jeshi akasema, "Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa." Paulo akasema, "Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa." 29Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo. 30Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.

Chapter 23

1Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, "Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu." 2Hapo Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni. 3Basi, Paulo akamwambia, "Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja Sheria kwa kuamuru nipigwe?" 4Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, "Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu!" 5Paulo akajibu, "Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni Kuhani Mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: `Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako."` 6Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaaza sauti yake mbele ya Baraza: "Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka." 7Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili. 8Kisa chenyewe kilikuwa hiki: Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu. 9Kelele ziliongezeka na baadhi ya walimu wa Sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: "Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye." 10Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome. 11Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, "Jipe moyo! Umenishuhudia katika Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma." 12Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: "Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo." 13Watu zaidi ya arobaini ndio waliokula njama kufanya hivyo. 14Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, "Sisi tumeapa kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo. 15Sasa basi, ninyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumuua hata kabla hajafika karibu." 16Lakini mtoto wa kiume wa dada yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo. 17Hapo Paulo akamwita mmoja wa askari, akamwambia, "Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia." 18Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, "Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukwambia." 19Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, "Una nini cha kuniambia?" 20Yeye akasema, "Wayahudi wamepatana wakuombe umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari kamili zaidi juu yake. 21Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya arobaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa mpaka watakapokuwa wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako." 22Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo. 23Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, "Wekeni tayari askari mia mbili, wapanda farasi sabini na askari mia mbili wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku. 24Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa." 25Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi: 26"Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu! 27"Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa. 28Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao. 29Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za Sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani. 30Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumuua, niliamua kumleta kwako. Nikamwambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako." 31Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri. 32Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapanda farasi waendelee na safari pamoja na Paulo. 33Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake. 34Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia, 35akasema, "Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika." Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode.

Chapter 24

1Baada ya siku tano, Kuhani Mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo. 2Paulo aliitwa na Tertulo akafungua mashtaka hivi: "Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu. 3Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali. 4Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi. 5Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti. 6Tena alijaribu kulikufuru Hekalu nasi tukamtia nguvuni. Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo."fc 7missing 8missing 9Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli. jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu. 8 Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako. 10Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, "Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi. 11Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu. 12Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu Hekaluni wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo. 13Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu. 14Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu na wazee wetu nikiishi kufuatana na Njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya Sheria na manabii. 15Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka. 16Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu. 17"Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa dhabihu. 18Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta Hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia. 19Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu. 20Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu, 21isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: `Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!"` 22Hapo, Felisi, ambaye mwenyewe alikuwa anaifahamu hiyo Njia vizuri, aliahirisha kesi hiyo. Akawaambia, "Nitatoa hukumu juu ya kesi hiyo wakati Luisa, mkuu wa jeshi, atakapokuja hapa." 23Kisha akamwamuru yule jemadari amweke Paulo kizuizini, lakini awe na uhuru kiasi, na rafiki zake wasizuiwe kumpatia mahitaji yake. 24Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo. 25Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, "Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi." 26Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye. 27Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa Mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini.

Chapter 25

1Siku tatu baada ya kufika mkoani, Festo alitoka Kaisarea, akaenda Yerusalemu. 2Makuhani wakuu pamoja na viongozi wa Wayahudi walimpa habari kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Paulo. Walimsihi Festo 3awafanyie fadhili kwa kumleta Paulo Yerusalemu; walikuwa wamekula njama wamuue akiwa njiani. 4Lakini Festo alijibu, "Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni. 5Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu." 6Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani. 7Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha. 8Kwa kujitetea, Paulo alisema, "Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu Sheria ya Wayahudi, wala kuhusu Hekalu, wala kumhusu Kaisari." 9Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, "Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?" 10Paulo akajibu, "Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote. 11Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!" 12Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, "Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari." 13Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo. 14Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: "Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini. 15Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu. 16Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka. 17Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe. 18Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia. 19Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai. 20Sikujua la kufanya kuhusu shauri hilo. Basi, nilimwuliza Paulo kama angependa kwenda mahakamani kule Yerusalemu kwa ajili ya mashtaka hayo. 21Lakini Paulo alikata rufani, akaomba aachwe kizuizini mpaka uamuzi wa shauri hilo ufanywe na Kaisari. Kwa hiyo niliamua akae kizuizini mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari." 22Basi Agripa akamwambia Festo, "Ningependa kumsikia mtu huyu mimi mwenyewe." Festo akamwambia, "Utamsikia kesho." 23Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani, 24Kisha akasema, "Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena. 25Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka. 26Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika. 27Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili."

Chapter 26

1Basi, Agripa akamwambia Paulo, "Unaruhusiwa kujitetea." Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi: 2"Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. 3Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu. 4"Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. 5Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali zaidi katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo. 6Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidia babu zetu. 7Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo! 8Kwa nini ninyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu? 9Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. 10Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. 11Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali. 12"Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. 13Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. 14Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: `Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama punda anayepiga teke fimbo ya bwana wake.` 15Mimi nikauliza: `Ni nani wewe Bwana?` Naye Bwana akajibu: `Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. 16Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonyesha. 17Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. 18Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.` 19"Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hilo la mbinguni. 20Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonyesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. 21Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa Hekaluni, wakajaribu kuniua. 22Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; 23yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine." 24Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, "Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!" 25Lakini Paulo akasema, "Sina wazimu mheshimiwa Festo: Ninachosema ni ukweli mtupu. 26Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila uoga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini." 28Agripa akamjibu Paulo, "Kidogo tu utanifanya Mkristo!" 29Paulo akamjibu, "Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo." 30Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. 31Walipokwisha ondoka, waliambiana, "Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo." 32Naye Agripa akamwambia Festo, "Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari."

Chapter 27

1Walipokwisha amua tusafiri mpaka Italia, walimweka Paulo pamoja na wafungwa wengine chini ya ulinzi wa Yulio aliyekuwa ofisa wa jeshi katika kikosi kiitwacho "Kikosi cha Augusto." 2Tulipanda meli ya Adiramito iliyokuwa inasafiri na kupitia bandari kadhaa za mkoa wa Asia, tukaanza safari. Aristarko, mwenyeji wa Makedonia kutoka Thesalonika, alikuwa pamoja nasi. 3Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji yake. 4Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi. 5Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia nanga Mura, mji wa Lukia. 6Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani. 7Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi. 8Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo "Bandari Nzuri", karibu na mji wa Lasea. 9Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo: 10"Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu." 11Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo. 12Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi. 13Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakang`oa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete. 14Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao "Upepo wa Kaskazi" ulianza kuvuma kutoka kisiwani. 15Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo. 16Kisiwa kimoja kiitwacho Kanda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli. 17Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libya. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo. 18Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli. 19Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe. 20Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia. 21Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, "Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote. 22Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea. 23Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea, 24akaniambia: `Paulo usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.` 25Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa. 26Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani." 27Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huku katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu. 28Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arobaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini. 29Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi. 30Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli. 31Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, "Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka." 32Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji. 33Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: "Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote. 34Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea." 35Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula. 36Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula. 37Jumla tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita katika meli. 38Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha, walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini. 39Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana. 40Hivyo walikata nanga na kuziacha baharini, na wakati huohuo wakazifungua kamba zilizokuwa zimeufunga usukani, kisha wakatweka tanga moja mbele kushika upepo, wakaelekea ufukoni. 41Lakini walifika mahali ambapo mikondo miwili ya bahari hukutana, na meli ikakwama. Sehemu ya mbele ilikuwa imezama mchangani bila kutikisika. Sehemu ya nyuma ya meli ilianza kuvunjika vipandevipande kwa mapigo ya nguvu ya mawimbi. 42Askari walitaka kuwaua wafungwa wote kwa kuogopa kwamba wangeogelea hadi pwani na kutoroka. 43Lakini kwa vile yule ofisajeshi alitaka kumwokoa Paulo, aliwazuia wasifanye hivyo. Aliamuru wale waliojua kuogelea waruke kutoka melini na kuogelea hadi pwani, 44na wengine wafuate wakijishikilia kwenye mbao au kwenye vipande vya meli iliyovunjika. Ndivyo sisi sote tulivyofika salama pwani.

Chapter 28

1Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta. 2Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha. 3Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni. Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo mkononi na kujishikilia hapo. 4Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaning`inia kwenye mkono wake waliambiana, "Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, `Haki` haitamwacha aendelee kuishi!" 5Lakini Paulo alikikung`utia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo. 6Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au hapohapo angeanguka chini na kufa. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa ni mungu. 7Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu. 8Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa, ana homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya. 9Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa. 10Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji. 11Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo "Miungu Pacha". Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi. 12Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu. 13Toka huko tuling`oa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli. 14Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma. 15Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo. 16Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda. ic 17Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, "Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. 18Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yeyote, walitaka kuniacha. 19Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu. 20Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli." 21Wao wakamwambia, "Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako. 22Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali." 23Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya Ufalme wa Mungu akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia Sheria ya Mose na maandiko ya manabii. 24Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini. 25Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili, "Kweli ni sawa yale aliyoyanena Roho Mtakatifu kwa wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya 26akisema: `Nenda kwa watu hawa ukawaambie: kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. 27Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya."` 28Halafu Paulo akamaliza na kusema, "Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!"fd walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao. 29missing 30Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu. 31Alikuwa akihubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.

Romans

Chapter 1

1Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu. 2Hapo kale, Mungu aliwaahidia watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. 3Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye mintarafu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi; 4mintarafu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka wafu. 5Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii. 6Ninyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo. 7Basi, ninawaandikia ninyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. 8Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. 9Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni 10daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. 11Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. 12Ndiyo kusema, tutaimarishana: imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha ninyi. 13Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. 14Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. 15Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu ninyi mlioko huko Roma. 16Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia. 17Kwa maana Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: "Mwadilifufa kwa imani ataishi." 18Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane. 19Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhirisha. 20Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea! 21Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. 22Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. 23Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao. 24Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao. 25Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina. 26Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. 27Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu. 28Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. 29Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, 30na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; 31hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. 32Wanajua kwamba Sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.

Chapter 2

1Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu. 2Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki. 3Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu? 4Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu? 5Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za haki vitadhihirishwa. 6Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake. 7Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele. 8Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia. 10Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia. 11Maana Mungu hambagui mtu yeyote. 12Wale wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria. 13Mtu hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii Sheria. 14Mathalan: watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria ingawa hawaijui Sheria. 15Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea. 16Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo. 17Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; 18kwa njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; 19wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; 20unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli. 21Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. 22Unasema: "Msizini," na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. 23Kwa kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria unamdharau Mungu? 24Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!" 25Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. 26Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. 27Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa. 28Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. 29Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya Sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.

Chapter 3

1Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? 2Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. 3Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? 4Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kila usemapo, maneno yako ni ya haki; na katika hukumu, wewe hushinda." 5Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). 6Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu? 7Labda utasema: "Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!" 8Ni sawa na kusema: tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili! 9Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora zaidi kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. 10Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! 11Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. 12Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. 13Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. 14Vinywa vyao vimejaa laana chungu. 15Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, 16popote waendapo husababisha maafa na mateso; 17njia ya amani hawaijui. 18Hawajali kabisa kumcha Mungu." 19Tunajua kwamba Sheria huwahusu walio chini ya Sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. 20Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuishika Sheria; kazi ya Sheria ni kumwonyesha tu mtu kwamba ametenda dhambi. 21Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea Sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. 22Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. 23Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. 24Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. 25Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonyesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; 26lakini sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonyesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonyesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humkubali kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu. 27Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza Sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini. 28Maana mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya Sheria. 29Au je, Mungu nu Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa mataifa mengine pia. 30Mungu ni mmoja, naye atawakubali Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao. 31Je, tunaitumia imani kuibatilisha Sheria? Hata kidogo; bali tunaipa Sheria thamani yake kamili.

Chapter 4

1Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu? 2Kama Abrahamu alikubaliwa kuwa mwadilifu kutokana na matendo yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu. 3Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu." 4Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake. 5Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, na hivi humkubali kuwa mwadilifu. 6Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake: 7"Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. 8Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu." 9Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: "Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu." 10Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. 11Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. 12Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa. 13Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii Sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu. 14Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii Sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu. 15Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna Sheria, haiwezekani kuivunja. 16Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: si kwa wale tu wanaoishika Sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote. 17Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi." Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini--Mungu ambaye huwapa wafu uzima, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa. 18Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Wazao wako watakuwa wengi kama nyota!" 19Alikuwa mzee wa karibu miaka mia moja, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa. 20Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu. 21Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi. 22Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu. 23Inaposemwa, "Alimkubali," haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu. 24Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka wafu. 25Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na Mungu.

Chapter 5

1Sasa, kwa vile tumekubaliwa kuwa wadilifu kwa imani, basi, tunayo amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. 2Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu. 3Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, 4nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. 5Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha miminia mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia. 6Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu. 7Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. 9Kwa kuwa sasa tumekubaliwa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu. 10Maana, tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo. 11Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu. 12Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi. 13Kabla ya Sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria. 14Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha yule ambaye atakuja baadaye. 15Lakini ipo tofauti: neema ya Mungu si kama dhambi ya Adamu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake. 16Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu, na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe. 17Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kukubaliwa kuwa waadilifu, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo. 18Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kimoja kiadilifu kinawapa uhuru na uzima. 19Na kama kwa kutotii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi wakubaliwe kuwa waadilifu. 20Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi. 21Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa njia ya uadilifu, na kuleta uzima wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Chapter 6

1Tuseme nini basi? Je, twendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke? 2Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa--tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi? 3Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake. 4Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya. 5Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka wafu kama yeye. 6Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi. 7Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka katika nguvu ya dhambi. 8Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. 9Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena. 10Hivyo, kwa kuwa alikufa--mara moja tu--dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. 11Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. 12Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake. 13Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni ninyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu. 14Maana, dhambi haitawatawala ninyi tena, kwani hamko chini ya Sheria, bali chini ya neema. 15Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya Sheria bali chini ya neema? Hata kidogo! 16Mnajua kwamba mkijitolea ninyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo--au watumwa wa dhambi, na matokeo yake ni kifo, au wa utii, na matokeo yake ni kukubaliwa kuwa waadilifu. 17Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini--namshukuru Mungu--mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea. 18Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu. 19(Hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe.) Kama vile wakati fulani mlivyojitolea ninyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu. 20Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na uadilifu. 21Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo! 22Lakini sasa, mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uzima wa milele. 23Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uzima wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.

Chapter 7

1Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua Sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. 2Mathalan: mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuw hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. 3Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi. 4Hali kadhalika ninyi ndugu zangu: ninyi pia mmekufa kuhusu Sheria kwa kuwa ninyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu. 5Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na Sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo. 6Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya Sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya Sheria iliyoandikwa. 7Je, tuseme basi, kwamba Sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila Sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama Sheria isingalikuwa imesema: "Usitamani." 8Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila Sheria dhambi ni kitu kilichokufa. 9Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na Sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka, 10nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo. 11Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua. 12Basi, Sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri. 13Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Iliyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionyesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno. 14Tunajua kwamba Sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi. 15Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachochukia ndicho nikifanyacho. 16Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile Sheria ni nzuri. 17Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi iliyo ndani yangu. 18Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza. 19Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka. 20Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi iliyo ndani yangu. 21Basi, nimegundua kanuni hii: ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua. 22Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu. 23Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu. 24Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka katika mwili huu unaonipeleka kifoni? 25Shukrani kwa Mungu afanyaye hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya dhambi.

Chapter 8

1Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. 2Maana, sheria ya Roho iletayo uzima kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. 3Mungu ametekeleza jambo lile ambalo Sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu w binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. 4Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya Sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. 5Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. 6Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uzima na amani. 7Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. 8Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. 9Lakini ninyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. 10Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmekubaliwa kuwa waadilifu. 11Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. 12Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. 13Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. 14Wote wanaoongozwa na Roho wa MUngu ni watoto wa Mungu. 15Kwa maana, Roho mliyempokea si Roho mwenye kuwafanya ninyi watumwa na kuwatia tena hofu; sivyo, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya ninyi watoto wa Mungu, na kwa nguvu ya huyo Roho, sisi tunaweza kumwita Mungu, "Aba," yaani "Baba!" 16Naye Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu. 17Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake. 18Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyafananisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19Viumbe vyote vinatazamia kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. 20Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, 21maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. 22Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. 23Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukitazamia kufanywa watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. 24Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa; lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? 25Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. 26Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. 27Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. 28Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake. 29Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita aliwakubali kuwa waadilifu; na hao aliowakubali kuwa waadilifu aliwashirikisha pia utukufu wake. 31Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? 32Mungu hakumhurumia hata mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? 33Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! 34Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! 35Ni nani awezaye kututenga na mapendo ya Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kuuawa? 36Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha: tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa." 37Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. 38Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: wala kifo, wala uhai; wala malaika, au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; 39Wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu kwetu kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.

Chapter 9

1Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. 2Nataka kusema hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu 3kwa ajili ya watu wangu, walio damu moja nami! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. 4Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. 5Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina. 6Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. 7Wala, si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Wazao wake watatokana na Isaka." 8Nido kusema, wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. 9Maana ahadi yenyewe ni hii: "Nitakujia wakati maalum, naye Sara atapata mtoto." 10Tena si hayo tu ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. 11Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, 12Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. 13Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia." 14Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo! 15Maana alimwambia Mose: "Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka." 16Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu. 17Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: "Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani." 18Ni wazi,basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo. 19Labda utaniuliza: "Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?" 20Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: "Kwa nini umenitengeneza namna hii?" 21Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida. 22Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonyesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake, Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa. 23Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake. 24Maana sisi ndio hao aliowaita, si tu kutoka miongoni mwa Wayahudi bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine. 25Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: "Wale waliokuwa `Si watu wangu` nitawaita: `Watu wangu!` Naye `Sikupendi` ataitwa: `Mpenzi wangu!` 26Na pale walipoambiwa: `Ninyi si wangu` hapo wataitwa: `Watoto wa Mungu hai."` 27Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaaza sauti: "Hata kama watoto wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa; 28maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote." 29Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: "Kama Bwana Mwenye Nguvu asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa ma Gomora." 30Basi, tuseme nini? Ni hivi: watu wa mataifa ambao hawakutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu, wamekubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani, 31hali watu wa Israeli waliokuwa wakitafuta Sheria iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu, hawakuipata. 32Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa 33kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Tazama! Naweka huko Sioni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa!"

Chapter 10

1Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. 2Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. 3Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. 4Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu. 5Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi." 6Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: `Nani atapanda mpaka mbinguni?` (yaani, kumleta Kristo chini); 7wala usiseme: `Nani atashuka mpaka Kuzimu` (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)." 8Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri. 9Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka. 10Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa. 11Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika." 12Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. 13Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa." 14Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? 15Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!" 16Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?" 17Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. 18Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu." 19Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu." 20Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu." 21Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii."

Chapter 11

1Basi, nauliza: je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mini binafsi ni Mwisraeli mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini. 2Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Eliya wakati alipomnung`unikia Mungu kuhusu Israeli: 3"Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua?" 4Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: "Nimejiwekea elfu saba ambao hawakumwabudu Baali." 5Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake. 6Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena. 7Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa, 8kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao." 9Naye Daudi anasema: "Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na kuadhibiwa. 10Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!" 11Basi, nauliza: je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu. 12Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao kwa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri zaidi kwamba utimilifu wao utasababisha baraka nyingi zaidi. 13Basi, sasa nawaambieni ninyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu, 14nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee ninyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao. 15Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka! 16Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia. 17Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Ninyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini. 18Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si ninyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza ninyi. 19Lakini utasema: "Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake." 20Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari. 21Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe? 22Kumbuka, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa. 23Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena. 24Ninyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao. 25Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu. 26Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Mkombozi atakuja kutoka Sioni, atauondoa uovu wa Yakobo. 27Hili ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao." 28Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa adui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni rafiki wa Mungu kwa sababu ya baba zao. 29Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo. 30Hapo awali ninyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao. 31Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa ninyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu. 32Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili wapate kuwahurumia wote. 33Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: 34"Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake? 35Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kulipwa tena kitu hicho?" 36Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina.

Chapter 12

1Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. 2Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. 3Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. 4Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. 5Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. 7Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. 8Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. 9Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. 10Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima. 11Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. 12Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima. 13Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. 14Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. 15Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia. 16Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. 17Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. 18Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. 19Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana." 20Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake." 21Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.

Chapter 13

1Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. 2Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe, 3Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; 4maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu kwao watendao maovu. 5Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo. 6Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. 7Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima. 8Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza Sheria. 9Maana, amri hizi: "Usizini; Usiue; Usitamani;" na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe." 10Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, kwa mapendo Sheria yote hutimizwa. 11Zaidi ya hayo, ninyi mnajua tumo katika wakati gani: sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu u karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. 12Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. 13Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana; tusiwe na ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu. 14Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.

Chapter 14

1Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi. 2Watu huhitilafiana: mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani. 3Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali. 4Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha. 5Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake. 6Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu. 7Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe 8maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. 9Maana Kristo alikufa, akafufuka ili wapate kuwa Bwana wa wazima na wafu. 10Kwa nini, basi wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. 11Maana Maandiko yanasema: "Kama niishivyo, asema Bwana kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu." 12Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja yake mbele ya Mungu. 13Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu yetu au kumsababisha aanguke katika dhambi. 14Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi. 15Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na mapendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake! 16Basi, msikubalie kitu mnachokiona kuwa kwenu ni kitu chema kidharauliwe. 17Maana Utawala wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. 18Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu. 19Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana. 20Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi. 21Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke. 22Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake. 23Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.

Chapter 15

1Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. 2Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. 3Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: "Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi." 4Maana yote yalioandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na Maandiko hayo Matakatifu tupate kuwa na matumaini. 5Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni ninyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, 6ili ninyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. 7Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. 8Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonyesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; 9ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa sababu hiyo, nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako." 10Tena Maandiko yasema: "Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake." 11Na tena: "Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni." 12Tena Isaya asema: "Atatokea mtu katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia." 13Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. 14Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba ninyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. 15Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu 16ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, dhabihu iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. 17Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. 18Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, 19kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. 20Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Watu wote ambao hawakuambiwa habari zote wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa." 22Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu. 23Lakini maadam sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, 24natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. 25Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalem. 26Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoka mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalem. 27Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. 28Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni ninyi nikiwa safarini kwenda Spania. 29Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo. 30Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa ajili ya upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu. 31Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalem ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko. 32Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi. 33Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!

Chapter 16

1Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea. 2Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia. 3Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu. 4Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine. 5Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao. Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni kwa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo. 6Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu. 7Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi. 8Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana. 9Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku. 10Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo. 11Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana. 12Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana. 13Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia. 14Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao. 15Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olumpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao. 16Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo. 17Ndugu zangu, nawasihi muwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao, 18maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu. 19Kila mtu amesikia juu ya utii wenu na hivyo mmekuwa sababu ya furaha yangu. Nawatakeni muwe na hekima katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya. 20Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. 21Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipatro, wananchi wenzangu, wanawasalimu. 22Nami Tertio, ninayeandika barua hii nawasalimuni katika Bwana. 23Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu.fb 24missing 25Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya ujumbe wa Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita. 26Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirisha kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii. 27Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina.

1 Corinthians

Chapter 1

1Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene, 2tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Ninyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia. 3Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo. 4Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia ninyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu. 5Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri, 6kwani, ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu, 7hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. 8Yeye atawaimarisha ninyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia Siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. 9Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita ninyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu. 10Ndugu, ninawasihi kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja. 11Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonyesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu. 12Nataka kusema hivi: kila mmoja anasema chake: mmoja husema, "Mimi ni wa Paulo," mwingine: "Mimi ni wa Apolo," mwingine: "Mimi ni wa Kefa," na mwingine: "Mimi ni wa Kristo,". 13Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo. 15Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. 16Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) 17Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe. 18Maana ujumbe kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu ujumbe huo ni nguvu ya Mungu. 19Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu ya wataalamu nitaitupilia mbali." 20Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa Sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu. 21Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. 22Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; 23lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; 24lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara zaidi kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu zaidi kuliko nguvu za binadamu. 26Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka ya juu. 27Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. 28Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. 29Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu. 30Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha ninyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa. 31Basi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mwenye kutaka kujivuna, basi, na ajivunie kazi ya Bwana."

Chapter 2

1Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu. 2Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa. 3Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi. 4Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho. 5Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu. 6Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea. 7Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu. 8Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangalielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. 9Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao." 10Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu. 11Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12Sasa sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu. 13Basi sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. 14Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. 15Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine. 16Maandiko yasema: "Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?" Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.

Chapter 3

1Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo. 2Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari. 3Maana bado mu watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na magombano kati yenu? Mambo hayo yanaonyesha wazi kwamba ninyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia. 4Mmoja wenu anaposema, "Mimi ni wa Paulo", na mwingine, "Mimi ni wa Apolo", je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu? 5Apolo ni nani? na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni ninyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana. 6Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu. 7Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota. 8Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe. 9Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na ninyi ni shamba lake; ninyi ni jengo lake. 10Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake. 11Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo. 12Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi. 13Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati Siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, Siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonyesha ubora wake. 14Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo; 15lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni. 16Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni ninyi wenyewe. 18Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli. 19Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: "Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao." 20Na tena: "Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai." 21Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu. 22Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu. 23Lakini ninyi ni wa Kristo naye Kristo ni wa Mungu.

Chapter 4

1Mtu na atuone sisi kuwa ni watumishi wa Kristo tuliokabidhiwa siri za mungu. 2Kinachotakiwa kwa yeyote yule aliyekabidhiwa kazi ni kuwa mwaminifu. 3Kwangu mimi si kitu nikihukumiwa na ninyi, au na mahakama ya kibinadamu; wala sijihukumu. 4Dhamiri yangu hainishtaki kwa jambo lolote, lakini hiyo haionyeshi kwamba sina lawama. Bwana ndiye anayenihukumu. 5Basi, msihukumu kabla ya wakati wake acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yaliyofichika, na kuonyesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa anayostahili kutoka kwa Mungu. 6Ndugu, hayo yote niliyosema juu ya Apolo na juu yangu, ni kielelezo kwenu: kutokana na mfano wangu mimi na Apolo nataka mwelewe maana ya msemo huu: "Zingatieni yaliyoandikwa." Kati yenu pasiwe na mtu yeyote anayejivunia mtu mmoja na kumdharau mwingine. 7Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa? 8Haya, mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tuweze kutawala pamoja nanyi. 9Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu. 10Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, ninyi ni wenye nguvu. Ninyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa. 11Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi. 12Tena twataabika na kufanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa, tunawatakia baraka; tukidhulumiwa, tunavumilia; 13tukisingiziwa, tunajibu kwa adabu. Mpaka sasa tumetendewa kama uchafu wa dunia; na kwa kila mtu sisi ni takataka! 14Siandiki mambo haya kwa ajili ya kuwaaibisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwafundisheni watoto wangu wapenzi. 15Maana hata kama mnao maelfu ya walezi katika maisha yenu ya Kikristo, baba yenu ni mmoja tu, kwani katika maisha ya Kikristo mimi ndiye niliyewazaeni kwa kuihubiri Habari Njema. 16Kwa hiyo, nawasihi: fuateni mfano wangu. 17Ndiyo maana nimemtuma Timetheo kwenu. Yeye ni mtoto wangu mpenzi na mwaminifu katika Bwana. Atawakumbusheni njia ninayofuata katika kuishi maisha ya Kikristo; njia ninayofundisha kila mahali katika makanisa yote. 18Baadhi yenu wameanza kuwa na majivuno wakidhani kwamba sitakuja tena kwenu. 19Lakini, Bwana akipenda, nitakuja kwenu upesi; na hapo ndipo nitakapojionea mwenyewe, sio tu kile wanachoweza kusema hao wenye majivuno, bali pia kila wanachoweza kufanya. 20Maana Utawala wa Mungu si shauri la maneno matupu, bali ni nguvu. 21Mnapendelea lipi? Nije kwenu na fimbo, ama nije na moyo wa upendo na upole?

Chapter 5

1Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! 2Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. 3Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. 4Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, 5mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana. 6Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? 7Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko. 8Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. 9Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. 10Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa! 11Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. 12Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe? 13Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!

Chapter 6

1Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu? 2Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo? 3Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika? 4Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa? 5Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini? 6Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini. 7Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa! Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyang`anywa mali yenu? 8Lakini, badala yake, ninyi ndio mnaodhulumu na kunyang`anya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu! 9Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti, 10wevi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang`anyi, hao wote hawatashiriki Utawala wa Mungu. 11Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu. 12Mtu anaweza kusema: "Kwangu mimi kila kitu ni halali." Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote. 13Unaweza kusema: "Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula." Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake. 15Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo! 16Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye--kama ilivyoandikwa: "Nao wawili watakuwa mwili mmoja." 17Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye. 18Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. 19Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi, si mali yenu wenyewe. 20Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

Chapter 7

1Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: naam, ni vizuri kama mtu haoi; 2lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe. 4Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo. 5Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu. 6Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri. 7Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile. 8Basi, wale ambao hawajaoana na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo. 9Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia basi, na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa. 10Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: mke asiachane na mumewe; 11lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe. 12Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka. 13Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe. 14Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu. 15Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni ninyi muishi kwa amani. 16Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo? 17Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote. 18Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe. 19Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu. 20Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa. 21Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie. 22Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo. 23Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu. 24Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa. 25Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa. 26Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo. 27Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa. 28Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate ninyi. 29Ndugu, nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa; 30wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; 31nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita. 32Ningependa ninyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana. 33Mtu aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe, 34naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe. 35Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuio. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja. 36Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi. 37Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira. 38Kwa maneno mengine: yule anayeamua kumwoa huyo mchumba wake anafanya vema; naye anayeamua kutomwoa anafanya vema zaidi. 39Mwanamke huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo. 40Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu.

Chapter 8

1Yahusu sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi, lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga. 2Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa. 3Lakini anayempenda Mungu huyo anajulikana naye. 4Kwa hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu. 5Hata kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu na mabwana wengi, 6hata hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu: Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake. 7Lakini, si kila mtu anao ujuzi huu. Maana wako watu wengine waliokwisha zoea sanamu, watu ambao mpaka hivi sasa wanapokula vyakula huviona bado kama vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Na kwa vile dhamiri zao ni dhaifu, hutiwa unajisi. 8Lakini chakula hakiwezi kutupeleka karibu zaidi na Mungu. Tukiacha kukila hatupungukiwi kitu, tukikila hatuongezewi kitu. 9Lakini, jihadharini: huu uhuru wenu usiwafanye walio na imani dhaifu waanguke katika dhambi. 10Maana, mtu ambaye dhamiri yake ni dhaifu, akikuona wewe mwenye ujuzi unakula vyakula hivyo ndani ya hekalu la sanamu, je, hatatiwa moyo wa kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu? 11Hivyo, huyo ndugu yako dhaifu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, atapotea kwa sababu ya ujuzi wako. 12Kama mkiwakosesha ndugu zenu jinsi hiyo na kuzijeruhi dhamiri zao dhaifu, mtakuwa mmemkosea Kristo. 13Kwa hiyo, ikiwa chakula husababisha kuanguka kwa ndugu yangu, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi.

Chapter 9

1Je, mimi si mtu huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Je, ninyi si matokeo ya kazi yangu kwa ajili ya Bwana? 2Hata kama kwa watu wengine mimi si mtume, lakini walau kwenu ninyi mimi ni mtume. Ninyi ni uthibitisho wa mtume wangu kwa sababu ya kuungana kwenu na Bwana. 3Hoja yangu kwa wale wanaonipinga ndiyo hii: 4Je, hatuna haki ya kula na kunywa? 5Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa? 6Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi? 7Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake? 8Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, Sheria nayo haisemi hivyo? 9Imeandikwa katika Sheria ya Mose: "Usimfunge kinywa ng`ombe anapoliwata nafaka." Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng`ombe? 10Je, hakuwa anatufikiria sisi aliposema hivyo? Naam, haya yaliandikwa kwa ajili yetu; kwani yule anayelima na yule anayevuna, wote wawili wana haki ya kutumaini kupata sehemu ya mavuno. 11Ikiwa sisi tumepanda mbegu ya kiroho kati yenu, je, ni jambo kubwa tukichuma kwenu faida ya kidunia? 12Ikiwa wengine wanayo haki ya kutazamia hayo kutoka kwenu, je, sisi hatuna haki zaidi kuliko hao? Lakini, sisi hatukuitumia haki hiyo, Badala yake, tumestahimili kila kitu ili tusiiwekee kizuizi chochote Habari Njema ya Kristo. 13Je, hamjui kwamba wanaotumikia Hekaluni hupata chakula chao Hekaluni, na kwamba wanaotolea sadaka madhabahuni hupata sehemu ya hiyo sadaka? 14Bwana aliagiza vivyo hivyo; wahubiri wa Habari Njema wapate riziki zao kutokana nayo. 15Lakini, mimi sikutumia hata mojawapo ya haki hizo. Na wala siandiki nijipatie haki hizo; kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kumfanya yeyote aone kwamba najisifu bure. 16Ikiwa ninaihubiri Habari Njema, hilo si jambo la kujivunia; hilo ni jukumu nililopewa. Na, ole wangu kama sitaihubiri Habari Njema! 17Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadam naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze. 18Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri. 19Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo. 20Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya Sheria, nimejiweka chini ya Sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya Sheria. 21Na kwa wale walio nje ya Sheria, naishi kama wao, nje ya Sheria, ili niwapate hao walio nje ya Sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo. 22Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia. 23Nafanya haya yote kwa ajili ya Habari Njema, nipate kushiriki baraka zake. 24Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi? 25Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji ya kudumu daima. 26Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani. 27Naupa mwili wangu mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili, nisije mimi mwenyewe nikakataliwa baada ya kuwahubiria wengine. ic

Chapter 10

1Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. 2Wote walibatizwa katika umoja na Mose kwa lile wingu na ile bahari. 3Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, 4wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. 5Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani. 6Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. 7Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: "Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza." 8Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu ishirini na tatu elfu. 9Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. 10Wala msinung`unike kama baadhi yao walivyonung`unika, wakaangamizwa na Mwangamizi! 11Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili. 12Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. 13Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama. 14Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu. 15Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo. 16Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? 17Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo. 18Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu. 19Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu? 20Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na ushirika na pepo. 21Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo. 22Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye? 23Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga. 24Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake. 25Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu; 26maana Maandiko yasema: "Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana." 27Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu. 28Lakini mtu akiwaambieni: "Chakula hiki kimetambikiwa sanamu," basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile. 29Nasema, "kwa ajili ya dhamiri," si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: "Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine? 30Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?" 31Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu. 33Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.

Chapter 11

1Niigeni mimi kama ninavyomwiga Kristo. 2Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni. 3Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo. 4Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo. 5Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake. 6Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake. 7Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume. 8Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume. 9Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume. 10Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika. 11Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke. 12Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu. 13Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani? 14Hata maumbile yenyewe huonyesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe; 15lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike. 16Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine. 17Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa ninyi hongera kuhusu haya yafuatayo: mikutano yenu ninyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida. 18Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi, 19maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana. 20Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula chakula cha Bwana! 21Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa! 22Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili. 23Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu aliotolewa, alitwaa mkate, 24akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: "Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka." 25Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe akasema: "Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka." 26Maana kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. 27Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. 28Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; 29maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. 30Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. 31Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. 32Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. 33Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula chakula cha Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake. 34Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.

Chapter 12

1Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya: 2Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu. 3Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: "Yesu alaaniwe!" Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: "Yesu ni Bwana," asipoongozwa na Roho Mtakatifu. 4Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja. 5Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. 6Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote. 7Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote. 8Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu apendavyo Roho huyohuyo. 9Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya; 10humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua. 11Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe. 12Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote--ingawaje ni vingi--hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. 13Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja. 14Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi. 15Kama mguu ungejisemea: "Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili", je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha! 16Kama sikio lingejisemea: "Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili", je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La! 17Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa? 18Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda. 19Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja. 21Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: "Sikuhitaji wewe", wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: "Siwahitaji ninyi." 22Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi. 23Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi, 24ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, 25ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane. 26Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho. 27Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. 28Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni. 29Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza? 30Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha? 31Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote.

Chapter 13

1Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele. 2Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu. 3Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote. 4Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni. 5Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya, 6hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli. 7Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote. 8Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita. 9Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili. 10Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka. 11Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadam mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha. 12Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi. 13Sasa yanadumu haya matatu: imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.

Chapter 14

1Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu. 2Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika. 3Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo. 4Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa. 5Basi, ningependa ninyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa. 6Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani. 7Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa? 8La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita? 9Hali kadhalika na ninyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani. 10Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana. 11Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu. 12Hali kadhalika na ninyi, maadam mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa. 13Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua. 14Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure. 15Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu. 16Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema: "Amina," kama haelewi unachosema? 17Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini huyo mwingine haitamfaidia. 18Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni zaidi kuliko ninyi nyote. 19Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema maneno elfu ya lugha ngeni. 20Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu muwe kama watoto wachanga lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu waliokomaa. 21Imeandikwa katika Sheria: "Bwana asema hivi: `Kwa njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza."` 22Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili ya wasioamini. 23Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je, hawatasema kwamba ninyi mna wazimu? 24Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu. 25Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na kumwabudu Mungu akisema: "Kweli Mungu yupo pamoja nanyi." 26Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27Wakiwepo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa. 28Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu. 29Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao. 30Ikiwa mmoja anaposema mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze. 31Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo. 32Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji. 33Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani. 34Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema; ila wawe watii kama isemavyo Sheria. 35Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini. 36Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu ninyi au kwamba limewajieni ninyi peke yenu? 37Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia ninyi ni amri ya Bwana. 38Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu huyo. 39Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni. 40Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu.

Chapter 15

1Sasa ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake. 2Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure. 3Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu; 4kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa; 5kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili. 6Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa. 7Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote. 8Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati. 9Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu. 10Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo. Na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami. 11Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachuhubiri, na hiki ndicho mnachoamini. 12Sasa, maadam inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu? 13Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka; 14na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana. 15Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu na kumbe yeye hakumfufua--kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi. 16Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka. 17Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu. 18Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa. 19Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani. 20Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, limbuko lao wale waliolala katika kifo. 21Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka wafu kumesababishwa na mtu mmoja. 22Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. 23Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza, halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja. 24Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba Utawala, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu. 25Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake. 26Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. 27Maana, Maandiko yasema: "Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake." Lakini, Maandiko yanaposema: "Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale" ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo. 28Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya Utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya Utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote. 29Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao? 30Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa? 31Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili. 32Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, "Tule na tunywe, maana kesho tutakufa." 33Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema. 34Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu! 35Lakini mtu anaweza kuuliza: "Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani wakati watakapokuja tena?" 36Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota. 37Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye. 38Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee. 39Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine. 40Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine. 41Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri. 42Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika. 43Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu. 44Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho. 45Maana Maandiko yasema: "Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;" lakini adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uzima. 46Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida kisha ule mwili wa kiroho. 47Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni. 48Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni. 49Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyohuyo aliyetoka mbinguni. 50Basi, ndugu, nasema hivi: kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki Ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika. 51Sikilizeni, nawaambieni siri: sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa 52wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana mbiu itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa. 53Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa. 54Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: "Kifo kimeangamizwa ushindi umekamilika!" 55"Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?" 56Ukali wa kifo hutokana na dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika Sheria. 57Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 58Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.

Chapter 16

1Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia. 2Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja. 3Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu. 4Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami. 5Nitakuja kwenu, baada ya kupitia Makedonia--maana nataraji kupitia Makedonia. 6Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda. 7Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu. 8Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste. 9Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi. 10Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi. 11Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu. 12Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana. 13Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu. 14Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo. 15Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi ninyi ndugu zangu, 16muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumikia pamoja nao. 17Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu. 18Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii. 19Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priskila pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika Bwana. 20Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu. 21Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe. 22Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANA THA--BWANA, njoo! 23Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi. 24Mapendo yangu yawe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.

2 Corinthians

Chapter 1

1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya. 2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. 3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. 4Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. 5Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye. 6Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi. 7Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu. 8Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi. 9Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe. 10Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena, 11ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu. 12Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu. 13Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa, 14maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari. 15Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu. 16Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea. 17Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema "Ndiyo" na "Siyo" papo hapo? 18Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo" na "Siyo". 19Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni "Ndiyo" ya Mungu. 20Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo, "Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. 21Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; 22ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea. 23Mungu ndiye shahidi wangu--yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni. 24Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.

Chapter 2

1Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. 2Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! 3Ndiyo maana niliwaandikia--sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi. 4Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno. 5Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi--ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. 6Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. 7Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. 8Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda. 9Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. 10Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe--kama kweli ninacho cha kusamehe--nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo. 12Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. 13Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia. 14Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. 15Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea. 16Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? 17Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.

Chapter 3

1Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine? 2Ninyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma. 3Ni dhahiri kwamba ninyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu. 4Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo. 5Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu: 6maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali Agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uzima. 7Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mng`ao wake. Tena mng`ao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho, 8basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi. 9Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma ile iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi. 10Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka. 11Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi. 12Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu. 13Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mng`ao uliokuwa unafifia. 14Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo. 15Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo Sheria ya Mose akili zao huwa zimefunikwa. 16Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa. 17Hapa "Bwana" ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru. 18Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, twaonyesha kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.

Chapter 4

1Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo. 2Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu. 3Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea. 4Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu. 5Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo. 7Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. 8Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; 9twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. 10Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. 11Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. 12Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi. 13Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. 14Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. 15Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu. 16Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. 17Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. 18Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.

Chapter 5

1Maana tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili wetu, itakapong`olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. 2Na sasa, katika hali hii, tunaugua, tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. 3Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. 4Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. 5Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea. 6Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana. 7Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona. 8Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana. 9Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko. 10Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya. 11Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. 12Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. 13Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. 14Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. 15Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. 16Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. 17Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. 18Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye. 19Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. 20Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.

Chapter 6

1Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. 2Mungu asema hivi: "Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia." Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu! 3Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote. 4Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. 5Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. 6Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, 7kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto. 8Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; 9kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa. 10Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu. 11Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. 12Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu. 13Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya. 14Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja? 15Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini? 16Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: "Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu." 17Kwa hiyo Bwana asema pia: "Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea. 18Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo."

Chapter 7

1Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu. 2Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote. 3Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja. 4Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno. 5Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu. 6Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito. 7Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana. 8Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda. 9Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote. 10Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. 11Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili. 12Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. 13Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo. 14Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu. 15Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka. 16Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa katika kila jambo.

Chapter 8

1Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia. 2Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana. 3Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe, 4walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu. 5Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu. 6Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia muitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu. 7Ninyi mna kila kitu: imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo. 8Siwapi ninyi amri, lakini nataka tu kuonyesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli. 9Maana, ninyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe. 10Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Ninyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo. 11Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha. 12Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa: hadai zaidi. 13Ninyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki. 14Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie ninyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa. 15Kama Maandiko yasemavyo: "Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa." 16Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia. 17Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu. 18Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Habari Njema zimeenea katika makanisa yote. 19Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema. 20Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu. 21Nia yetu ni kufanya vema, si tu mbele ya Bwana, lakini pia mbele ya watu. 22Basi, pamoja na ndugu hao, tumemtuma ndugu yetu mwingine ambaye mara nyingi tumempa majaribio mbalimbali, tukamwona kuwa ni mwenye hamu kubwa ya kusaidia; hata sasa amekuwa na moyo zaidi kwa sababu ana imani sana nanyi. 23Tito ni mwenzangu; tunafanya kazi pamoja kwa ajili yenu; lakini kuhusu hawa ndugu zetu wengine, wanaokuja pamoja nao, hao ni wajumbe wa makanisa, na utukufu kwa Kristo. 24Basi, waonyesheni uthabiti wa upendo wenu, makanisa yapate kuona kweli kwamba fahari ninayoona juu yenu ni ya halali.

Chapter 9

1Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma hiyo yenu kwa ajili ya watu wa Mungu. 2Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: "Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana." Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi. 3Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema. 4Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika--bila kutaja aibu mtakayopata ninyi wenyewe--kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi. 5Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ionyeshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa. 6Kumbukeni: "Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi." 7Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. 8Mungu anaweza kuwapeni ninyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. 9Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini, wema wahudumu milele." 10Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, ziwe na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. 11Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu. 12Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si tu kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. 13Kutokana na uthibitisho unaoonyeshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote. 14Kwa hiyo watawaombea ninyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu. 15Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!

Chapter 10

1Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali wakati nikiwa mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo. 2Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia. 3Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia. 4Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu za Mungu zenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo, 5na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo. 6Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii. 7Ninyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo. 8Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa--uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa--hata hivyo sijutii hata kidogo. 9Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha ninyi kwa barua zangu. 10Mtu anaweza kusema: "Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu." 11Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi. 12Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu. 13Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu. 14Na kwa vile ninyi mu katika mipaka hiyo, hatukuipita tulipokuja kwenu, tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo. 15Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu. 16Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine. 17Lakini kama yasemavyo Maandiko: "Mwenye kuona fahari na aone fahari juu ya alichofanya Bwana." 18Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.

Chapter 11

1Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi fulani! Naam, nivumilieni kidogo. 2Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana ninyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo. 3Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo. 4Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, ninyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au habari njema tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu! 5Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao "mitume wakuu." 6Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionyesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati. 7Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekeza ili nipate kuwakweza ninyi. Je, nilifanya vibaya? 8Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia ninyi. 9Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo. 10Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya. 11Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi ninyi? Mungu anajua kwamba nawapenda! 12Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi. 13Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanojisingizia kuwa mitume wa Kristo. 14Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga! 15Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao. 16Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo. 17Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu. 18Maadam wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna. 19Ninyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu! 20Mnamvumilia hata mtu anayewafanya ninyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni! 21Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu--nasema kama mtu mpumbavu--mimi nathubutu pia. 22Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi. 23Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi--nanena hayo kiwazimu--ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi. 24Mara tano nilichapwa vile viboko thelathini na tisa vya Wayahudi. 25Nilipigwa viboko mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa. 26Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo 27Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo. 28Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote. 29Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi. ic 30Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu. 31Mungu na Baba wa Bwana Yesu--jina lake litukuzwe milele--yeye anajua kwamba sisemi uongo. 32Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili apate kunikamata. 33Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.

Chapter 12

1Nitajivuna basi, ingawa haifai! Lakini sasa nitasema juu ya maono na ufunuo alivyonijalia Bwana. 2Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.) 3Narudia: najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.) 4Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka. 5Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu. 6Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli mtupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu. 7Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga nisijivune kupita kiasi. 8Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke. 9Lakini akaniambia: "Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu." Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu. 10Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, madharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu. 11Nimekuwa kama mpumbavu, lakini, ninyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Ninyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo zaidi kuliko hao "mitume wakuu." 12Miujiza na maajabu yaonyeshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote. 13Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo! 14Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni ninyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao. 15Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda ninyi mno? 16Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: "Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai." 17Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu? 18Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja? 19Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo, yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi. 20Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyano, kunong`ona, majivuno na fujo kati yenu. 21Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujutia huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya.

Chapter 13

1Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. "Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu," yasema Maandiko. 2Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, watakiona cha mtema kuni. 3Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu. 4Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu. 5Jichunguzeni ninyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni ninyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi ninyi mmeshindwa. 6Lakini natumaini kwamba ninyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa. 7Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa. 8Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli. 9Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu. 10Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa. 11Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa mapendo na amani atakuwa pamoja nanyi. 12Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni. 13Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.

Galatians

Chapter 1

1Mimi Paulo mtume, 2na ndugu wote walio pamoja nami, tunayaandikia makanisa yaliyoko Galatia. Mimi nimepata kuwa mtume si kutokana na mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka wafu. 3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. 4Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa. 5Kwake yeye uwe utukufu milele! Amina. 6Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi yule aliyewaita kwa neema ya Kristo, mkafuata Habari Njema ya namna nyingine. 7Lakini hakuna "Habari Njema" nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Habari Njema ya Kristo. 8Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni Habari Njema tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe! 9Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: kama mtu yeyote anawahubirieni Habari Njema ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe! 10Sasa nataka kibali cha nani: cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo. 11Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Habari Njema niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu. 12Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia. 13Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa. 14Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu. 15Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie. 16Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanae kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu, 17na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko. 18Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano. 19Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. 20Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo. 21Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia. 22Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea. 23Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: "Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza." 24Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

Chapter 2

1Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami. 2Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Habari Njema niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa isije ikawa bure. 3Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa, 4ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa. 5Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Habari Njema ubaki nanyi daima. 6Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi--kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje--watu hawa hawakuwa na kitu cha kuongeza katika Habari hii Njema kama niihubirivyo. 7Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Habari Njema kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi. 8Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine. 9Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi. 10Wakatuomba lakini kitu kimoja: tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza. 11Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea. 12Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara. 13Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao. 14Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Habari Njema haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: "Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?" 15Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine hao wenye dhambi! 16Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii Sheria. 17Sasa, ikiwa katika kutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo! 18Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu. 19Maana, kuhusu Sheria hiyo, mimi nimekufa; Sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani, 20na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. 21Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu huweza kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya Sheria, basi, Kristo alikufa bure!

Chapter 3

1Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaloga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu. 2Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya Sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Habari Njema? 3Je, mu wajinga kiasi hicho? Ninyi mlianza yote kwa msaada wa Roho je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe? 4Je, mambo yale yote yaliyowapata ninyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani! 5Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Habari Njema na kuiamini? 6Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu. 7Sasa basi jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu. 8Maandiko Matakatifu yalionyesha kabla kwamba Mungu atawakubali watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: "Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa." 9Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini. 10Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na Sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria, yuko chini ya laana." 11Ni dhahiri kwamba Sheria haiwezi kumfanya mtu akubaliwe kuwa mwadilifu; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mwadilifu kwa imani ataishi." 12Lakini Sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: "Mwenye kutimiza yanayotakiwa na Sheria ataishi." 13Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya Sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: "Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa." 14Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia. 15Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. 16Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: "Na wazawa wake," yaani wengi, bali yasema, "Na mzawa wake," yaani mmoja, naye ndiye Kristo. 17Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake akalithibitisha; Sheria ambayo ilitokea miaka mia nne na thelathini baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. 18Maana, kama urithi ya Mungu inategemea Sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi. 19Ya nini basi, Sheria? Iliongezwa hapo ili kuonyesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. 21Je, Sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uzima, basi, tungeweza kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria. 22Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, kwa kumwamini Yesu Kristo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi. 23Kabla ya kujaliwa imani, Sheria ilitufanya wafungwa mpaka imani hiyo iliyokuwa inakuja ifunuliwe. 24Basi, hiyo Sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani, tukubaliwe kuwa waadilifu. 25Tangu kufika kwa hiyo imani, Sheria si mlezi wetu tena. 26Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo. 27Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. 28Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu. 29Ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.

Chapter 4

1Basi, nasema hivi: mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake. 2Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake. 3Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu. 4Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria 5apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu. 6Kwa vile sasa ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia "Aba," yaani "Baba." 7Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake. 8Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mkatumikia miungu isiyo miungu kweli. 9Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena? 10Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka! 11Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure! 12Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea ubaya wowote. 13Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Habari Njema kwa mara ya kwanza. 14Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe. 15Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyang`oa macho yenu na kunipa mimi. 16Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli? 17Hao watu wengine wanawahangaikia ninyi, lakini nia zao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili ninyi muwahangaikie wao. 18Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi. 19Watoto wangu, kama vile mama mja mzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu. 20Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi! 21Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo Sheria? 22Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru. 23Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. 24Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani. 25Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake. 26Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu. 27Maana imeandikwa: "Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paaza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi zaidi kuliko wa yule aliye na mume." 28Sasa, basi, ndugu zangu, ninyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka. 29Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi. 30Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: "Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru." 31Kwa hiyo, basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.

Chapter 5

1Kristo alitupa uhuru akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa. 2Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote. 3Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika Sheria yote. 4Kama mnatazamia kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu. 5Kwa upande wetu, lakini, sisi tunatumaini kwamba kwa nguvu ya Roho tunakubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. 6Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. ic 7Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi aliyewazuia kuuzingatia ukweli? 8Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. 9"chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!" 10Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba ninyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni--awe nani au nani--hakika ataadhibiwa. 11Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. 12Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe! 13Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. 14Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe." 15Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe! 16Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. 17Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe. 18Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya Sheria. 19Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi; 20kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; 21husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawatakuwa na nafasi yao katika ufalme wa Mungu. 22Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, 23upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo. 24Wale walio wa Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. 25Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake. 26Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.

Chapter 6

1Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. 2Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. 3Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. 4Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. 5Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba. 6Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. 7Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. 8Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele. 9Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. 10Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu. 11Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. 12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. 13Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. 14Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. 16Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu. 17Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. 18Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.

Ephesians

Chapter 1

1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. 2Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. 3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. 4Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, 5Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. 6Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu katika Mwanae mpenzi! 7Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake 8aliotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote 9Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. 10Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. 11Kila kitu hufanywa kufuatana na mpango na uamuzi wa Mungu; naye Mungu ametuteua sisi tuwe watu wake kwa mapenzi yake katika kuungana na Kristo, kufuatana na azimio alilofanya tangu mwanzo. 12Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! 13Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonyesha kuwa ninyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. 14Huyu Roho ni dhamana ya kurithi yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake! 15Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu na mapendo yenu kwa watu wa Mungu, 16sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu 17ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. 18Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, 19mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na nguvu ile kuu mno 20aliyomfufua nayo Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni. 21Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. 22Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. 23Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.

Chapter 2

1Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu. 2Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu. 3Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu. 4Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, 5hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa. 6Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni. 7Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu. 8Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. 9Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu. 10Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende. 11Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine--mnaoitwa, "wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita, "Waliotahiriwa," (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao)--kumbukeni mlivyokuwa zamani. 12Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani. 13Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo. 14Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. 15Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani. 16Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. 17Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu. 18Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja. 19Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. 20Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. 21Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana. 22Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

Chapter 3

1Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu. 2Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu. 3Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili, 4nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo.) 5Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho. 6Siri yenyewe ni hii: kwa njia ya Habari Njema watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. 7Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Habari Njema kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu. 8Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika, 9tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha siri hiyo yake tangu milele, 10kusudi, sasa kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi. 11Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Bwana wetu. 12Basi, katika kuungana na Kristo, na kwa njia ya imani katika Kristo, sisi tunathubutu kumkaribia Mungu kwa uhodari. 13Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu. 14Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, 15aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. 16Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, 17naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo 18kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. 19Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. 20Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu, aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; 21kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.

Chapter 4

1Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. 2Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni ninyi kwa ninyi kwa mapendo. 3Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. 4Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. 5Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; 6kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote. 7Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo. 8Kama yasemavyo Maandiko: "Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi." 9Basi, inaposemwa: "alipaa juu," ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani. 10Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani, ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu. 11Ndiye aliyewapa watu zawadi: wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Habari Njema, wengine wachungaji na walimu. 12Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo, 13na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. 14Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu, ili wawapotoshe wengine kwa hila. 15Ila, sisi tukisema ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua zidi katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; 16chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo. 17Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu, 18na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uzima wa Mungu, kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao. 19Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu. 20Lakini ninyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo. 21Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu. 22Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. 23Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. 24Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionyesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu. 25Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo. 26Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. 27Msimpe Ibilisi nafasi. 28Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini. 29Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu. 30Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba ninyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni. 31Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele, matusi! Achaneni na kila uovu! 32Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.

Chapter 5

1Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana ninyi ni watoto wake wapenzi. 2Upendo uongoze maisha yenu, kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri na tambiko impendezayo Mungu. 3Kwa vile ninyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. 4Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. 5Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mfisadi, (ufisadi ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika Utawala wa Kristo na wa Mungu. 6Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. 7Basi, msishirikiane nao. 8Zamani ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga: 9maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli. 10Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana. 11Msishiriki katika matendo yasiyofaa, ya giza bali yafichueni. 12Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja. 13Lakini mambo yale yanayotendwa katika mwanga, ukweli wake hudhihirishwa; 14na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: "Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka wafu, naye Kristo atakuangaza." 15Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi: Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima. 16Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya. 17Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. 18Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu. 19Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu. 20Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 21Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo. 22Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. 23Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake. 24Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote. 25Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. 26Alifanya hivyo, ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji, 27kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safu kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo. 28Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. (( 29Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa, 30maana sisi ni viungo vya mwili wake.) 31Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa hiyo, mwanamume atawaacha baba na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja." 32Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake. 33Lakini yanawahusu ninyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.

Chapter 6

1Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. 2"Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, 3"Upate fanaka na miaka mingi duniani." 4Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo. 5Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo. 6Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo. 7Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu. 8Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana. 9Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu. 10Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. 11Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi. 12Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. 13Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti. 14Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani, 15na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu. 16Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. 17Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. 18Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. 19Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti. 20Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo. 21Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya. 22Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo. 23Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. 24Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.

Colossians

Chapter 1

1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, 2tunawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu. 3Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. 4Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. 5Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani Habari Njema, ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na upendo wenu vinategemea jambo lile mnalotumainia ambalo mmewekewa salama mbinguni. 6Habari Njema inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. 7Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. 8Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. 9Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake. 10Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. 11Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili mweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. 12Na kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika utawala wa mwanga. 13Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi, 14ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. 15Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16Maana kwa njia yake vitu vyote viliumbwa duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: wenye enzi, watawala, wakuu na wenye mamlaka. Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake. 17Kristo alikuwako kabla ya vitu vyote; kwa kuungana naye, vyote vyadumu mahali pake. 18Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote. 19Maana Mungu alipenda utimilifu wote uwe ndani yake. 20Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniania; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani. 21Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa adui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. 22Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. 23Mnapaswa, lakini kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani hiyo, na msikubali kusukumwa mbali na tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Habari Njema. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Habari Njema ambayo imekwisha hubiriwa kila kiumbe duniani. 24Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa. 25Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake, 26ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake. 27Mpango wa Mungu ni kuwajulisha watu wake siri hii kuu na tukufu ambayo ni kwa ajili ya watu wote. Na, siri yenyewe ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba ninyi mtaushiriki utukufu wa Mungu. 28Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo. 29Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.

Chapter 2

1Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho. 2Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe. 3Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu. 4Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana. 5Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo. 6Maadamu ninyi mmemkubali Kristo Yesu kuwa Bwana, basi, ishini katika muungano naye. 7Mnapaswa kuwa na mizizi ndani yake, kujijenga juu yake na kuwa imara katika imani yenu kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele. 8Angalieni basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe! 9Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, 10nanyi mmepewa uzima kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote. 11Katika kuungana na Kristo ninyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi. 12Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo, mlifufuliwa pia pamoja naye kwa imani yenu katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka wafu. 13Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; 14alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. 15Juu ya msalaba Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake. 16Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya Mwezi mpya au Sabato. 17Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo. 18Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganifu za kidunia 19na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu. 20Ninyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa kutoka nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti: 21"Msishike hiki," "Msionje kile," "Msiguse kile!" 22Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu. 23Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima katika namna ya ibada ya kujitakia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutendea mwili kwa ukali; lakini kwa kweli, haifai chochote kuzuia tamaa za mwili.

Chapter 3

1Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu. 2Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani. 3Maana ninyi mmekufa na uzima wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4Uzima wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu. 5Basi, komesheni kabisa kila kitu kilicho ndani yenu ambacho chahusika na mambo ya kidunia: uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). 6Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. 7Wakati mmoja ninyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. 8Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: hasira, tamaa, uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. 9Msiambiane uongo, kwani ninyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, 10mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. 11Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote. 12Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi. 14Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. 15Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! 16Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. 17Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake. 18Enyi akina mama, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana. 19Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao. 20Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana. 21Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo watakata tamaa. 22Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana. 23Kila mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana na si kwa ajili ya mtu. 24Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana! 25Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu hana ubaguzi.

Chapter 4

1Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni. 2Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. 3Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. 4Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. 5Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo. 6Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja. 7Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. 8Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. 9Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa. 10Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni). 11Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu. 12Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu. 13Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli. 14Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni. 15Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake. 16Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao. 17Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana. 18Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.

1 Thessalonians

Chapter 1

1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo. 2Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu. 3Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti. 4Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake, 5maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu. 6Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu. 7Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa Makedonia na Akaya. 8Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi. 9Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli, 10na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.

Chapter 2

1Ndugu, ninyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu haikuwa bure. 2Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake. 3Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote. 4Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani. 5Ninyi mnajua kwamba sisi hatukuja kwenu na maneno matamu ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi! 6Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote, 7ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa Wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake. 8Tuliwapenda ninyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu! 9Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu. 10Ninyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, jinsi mwenendo wetu kati yenu ninyi mnaoamini ulivyokuwa mzuri, mwadilifu na usio na lawama. 11Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe. 12Tuliwapeni moyo, tuliwafarijini na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye aliwaiteni mshiriki Utawala na utukufu wake. 13Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini. 14Ndugu, ninyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Ninyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi, 15ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni adui za kila mtu! 16Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia. 17Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena! 18Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia. 19Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni ninyi wenyewe; ninyi ndio tumaini letu na furaha yetu. 20Naam, ninyi ni utukufu wetu na furaha yetu!

Chapter 3

1Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu, 2na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini, 3kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Ninyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso. 4Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo ndivyo ilivyotukia. 5Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu imepotea bure! 6Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni. 7Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote, 8kwani sasa tunaishi kweli ikiwa ninyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana. 9Sasa twaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu. 10Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu. 11Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu atutayarishie njia ya kuja kwenu. 12Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi. 13Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.

Chapter 4

1Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi. 2Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu. 3Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. 4Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, 5na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu. 6Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo. 7Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu. 8Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu. 9Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. 10Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi. 11Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. 12Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu. 13Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini. 15Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. 16Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. 17Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. 18Basi, farijianeni kwa maneno haya.

Chapter 5

1Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya. 2Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku. 3Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo. 4Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi. 5Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. 6Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. 7Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. 8Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. 9Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 10ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. 11Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa. 12Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo. 13Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu. 14Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. 15Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. 16Furahini daima, 17salini kila wakati 18na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. 19Msimpinge Roho Mtakatifu; 20msidharau unabii. 21Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema, 22na epukeni kila aina ya uovu. 23Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. 24Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. 25Ndugu, tuombeeni na sisi pia. 26Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. 27Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. 28Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

2 Thessalonians

Chapter 1

1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo. 2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. 3Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana. 4Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata. 5Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka. 6Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi, 7na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu 8na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. 9Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu, 10wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea. 11Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani. 12Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

Chapter 2

1Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana 2msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. 3Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. 4Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu. 5Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? 6Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. 7Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. 8Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng`ao wa kuja kwake. 9Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, 10na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. 11Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. 12Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, ila wafurahia dhambi, watahukumiwa. 13Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. 14Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15Basi, ndugu, simameni imara na zingatieni yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua zetu. 16Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda, na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, 17aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili mweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.

Chapter 3

1Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. 2Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanaoamini ujumbe huu. 3Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. 4Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. 5Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo. 6Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. 7Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; 8hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. 9Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. 10Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "Mtu asiyefanya kazi, asile." 11Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. 12Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. 13Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema. 14Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye kusudi aone aibu. 15Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu. 16Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote. 17Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika. 18Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

1 Timothy

Chapter 1

1Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, 2nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. 3Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. 4Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. 5Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli. 6Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. 7Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza. 8Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. 9Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; 10sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli. 11Mafundisho hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri. 12Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, 13ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. 14Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. 15Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, 16lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele. 17Kwake yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee--kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. 18Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, 19na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. 20Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

Chapter 2

1Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, 2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema. 3Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu, 4ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli. 5Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu, 6ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia. 7Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo! 8Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi. 9Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, 10bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu. 11Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza. 12Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya. 13Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa. 14Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu. 15Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.

Chapter 3

1Msemo huu ni wa kweli: mtu akitaka kuwa kiongozi katika kanisa, huyo anatamani kazi nzuri. 2Basi, kiongozi wa kanisa anapaswa awe mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha; 3asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha; 4anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote. 5Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu? 6Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa. 7Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi. 8Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha; 9wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani. 10Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao. 11Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote. 12Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake. 13Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu. 14Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni. 15Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli. 16Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la kibinadamu alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika. Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa popote ulimwenguni, akachukuliwa juu mbinguni katika utukufu.

Chapter 4

1Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo. 2Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto. 3Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuona na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani. 4Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani, 5kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu. 6Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli, ambayo wewe umeyafuata. 7Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. 8Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uzima katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. 9Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. 10Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. 11Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. 12Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. 13Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. 15Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. 16Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.

Chapter 5

1Usimkemee mtu mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana kama ndugu zako, 2wanawake wazee kama mama yako, na wasichana kama dada zako, kwa usafi wote. 3Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli. 4Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu. 5Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana. 6Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai. 7Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama. 8Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini. 9Usimtie katika orodha ya wajane, mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu, 10na awe mwenye sifa nzuri: aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema. 11Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo watataka kuolewa tena, 12na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali. 13Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema. 14Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili adui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu. 15Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani. 16Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachilia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa. 17Wazee wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha. 18Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Usimfunge ng`ombe kinywa anapopura nafaka." na tena "Mfanyakazi astahili malipo yake." 19Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu. 20Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa. 21Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu, na mbele ya malaika watakatifu uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda. 22Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi. 23Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara. 24Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi, nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye. 25Vivyo hivyo, matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika.

Chapter 6

1Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu. 2Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya. 3Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya dini, 4huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya, 5na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri. 6Kweli dini humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo. 7Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote. 8Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo. 9Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi. 10Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi. 11Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, mapendo, subira na unyenyekevu. 12Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uzima wa milele, uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. 13Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato, 14nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka Siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. 15Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. 16Yeye peke yake anaishi milele, katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina. 17Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie. 18Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao. 19Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uzima ambao ni uzima wa kweli. 20Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine: "Elimu". 21Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!

2 Timothy

Chapter 1

1Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uzima tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu, 2nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu. 3Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka daima katika sala zangu. 4Nakumbuka machozi yako na ninatamani usiku na mchana kukuona, ili nijazwe furaha. 5Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo. 6Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu. 7Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu. 8Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu. 9Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya matendo yetu wenyewe bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo katika Kristo Yesu kabla mwanzo wa nyakati; 10lakini sasa imefunuliwa kwetu kwa kuja kwake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uzima usio kufa. 11Mungu amenichagua mimi niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema, 12nami nateseka mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye aweza kukilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka Siku ile. 13Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha, na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu. 14Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu. 15Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene. 16Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni, 17ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata. 18Bwana amjalie huruma katika Siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.

Chapter 2

1Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu. 2Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia. 3Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo yesu. 4Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi. 5Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo. 6Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno. 7Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uyaelewe yote. 8Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri. 9Kwa sababu ya kuihubiri Habari Njema mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo, 10na hivyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele. 11Usemi huu ni wa kweli: "Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. 12Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana. 13Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe." 14Basi, wakumbushe watu wako mambo haya, na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. 15Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake, na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli. 16Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu. 17Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto. 18Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika. 19Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: "Bwana anawafahamu wale walio wake," na "Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu." 20Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine ni vya matumizi ya pekee na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida. 21Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema. 22Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi. 23Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi. 24Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu, 25ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli. 26Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.

Chapter 3

1Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. 2watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; 3watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; 4watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. 5Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. 6Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; 7wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. 8Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. 9Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre. 10Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, 11udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. 12Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. 13Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe. 14Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako. 15Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. 16Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, 17ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.

Chapter 4

1Nakuamuru mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme: 2hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote. 3Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia walimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kusikia. 4Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo. 5Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali; vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema, timiza kikamilifu utumishi wako. 6Kwa upande wangu mimi, niko karibu kabisa kutolewa dhabihu na wakati wa kufariki kwangu umefika. 7Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safari yote na imani nimeitunza. 8Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana Hakimu wa haki, atanipa mimi Siku ile na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake. 9Fanya bidii kuja kwangu karibuni. 10Dema ameupenda ulimwengu huu akaniacha na kwenda zake Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia, na Tito amekwenda Dalmatia. 11Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mpate Marko uje naye, kwa maana ataweza kunisaidia katika kazi yangu. 12Nilimtuma Tukiko kule Efeso. 13Utakapokuja niletee koti langu nililoacha kwa Karpo kule Troa; niletee pia vile vitabu, na hasa vile vilivyotengenezwa kwa ngozi. ic 14Yule sonara aitwaye Aleksanda amenitendea maovu mengi; Bwana atamlipa kufuatana na hayo matendo yake. 15Jihadhari naye kwa sababu aliupinga ujumbe wetu kwa ukali. 16Wakati nilipojitetea kwa mara ya kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu; wote waliniacha. Mungu asiwahesabie kosa hilo! 17Lakini, Bwana alikaa pamoja nami, akanipa nguvu, hata nikaweza kuutangaza ujumbe wote, watu wa mataifa wausikie; tena nikaokolewa katika hukumu ya kifo kama kinywani mwa simba. 18Bwana ataniokoa na mambo yote maovu, na kunichukua salama mpaka katika Utawala wake wa mbinguni. Kwake uwe utukufu milele na milele! Amina. 19Wasalimu Priska na Akula, pamoja na jamaa ya Onesiforo. 20Erasto alibaki Korintho, naye Trofimo nilimwacha Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa. 21Fanya bidii kuja kabla ya majira ya baridi. Ebulo, Pude, Lino na Klaudia wanakusalimu; vilevile ndugu wengine wote. 22Bwana awe nawe rohoni mwako. Nawatakieni nyote neema.

Titus

Chapter 1

1Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu, 2ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uzima wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uzima huo kabla ya mwanzo wa nyakati, 3na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo nuutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu. 4Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu. 5Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu: 6mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi. 7Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo. 8Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu. 9Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho ya kweli na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo. 10Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, wanaowapotosha wengine kwa upumbavu wao. 11Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha. 12Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: "Wakrete, husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!" 13Naye alitoboa ukweli kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu. 14Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli. 15Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa. 16Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.

Chapter 2

1Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho safi. 2Waambie wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu. 3Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, 4ili wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, 5wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa. 6Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. 7Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. 8Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu. 9Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, 10au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu. 11Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. 12Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, 13tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema. 15Basi, fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.

Chapter 3

1Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. 2Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. 3Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukawachukia. 4Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu, ulipofunuliwa, 5alituokoa. alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali alituokoa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. 6Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, 7ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia. 8Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu, wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, ambayo ni mambo mazuri na ya manufaa kwa watu. 9Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya Sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. 10Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. 11Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea. 12Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. 13Jitahidi kumsaidia mwana sheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. 14Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. 15Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Philemon

Chapter 1

1Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu 2na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo. 3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo. 4Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu 5maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. 6Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. 7Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu. 8Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. 9Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. 10Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. 11Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. 12Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. 13Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema. 14Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika. 15Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. 16Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana. 17Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. 18Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. 19Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: yako.) 20Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo. 21Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba. 22Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni. 23Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu. 24Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu. 25Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Hebrews

Chapter 1

1Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, 2lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu na akamteua avimiliki vitu vyote. 3Yeye ni mng`ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwapatia binadamu msamaha wa dhambi zao, aliketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu. 4Mwana ni mkuu zaidi kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu zaidi kuliko jina lao. 5Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Wewe ni Mwanangu; Mimi leo nimekuwa Baba yako." Wala hakusema juu ya malaika yeyote: "Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu." 6Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, alisema: "Malaika wote wa Mungu wanapaswa kumwabudu." 7Lakini kuhusu malaika, Mungu alisema: "Mungu awafanya malaika wake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa ndimi za moto." 8Lakini kumhusu Mwana, Mungu alisema: "Utawala wako ee Mungu, wadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki. 9Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako." 10Pia alisema: "Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako. 11Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi. 12Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma." 13Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako." 14Malaika ni roho tu wanaomtumikia Mungu, na Mungu huwatuma wawasaidie wale watakaopokea wokovu.

Chapter 2

1Kwa sababu hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini zaidi yote tuliyosikia, ili tusije tukapotoshwa. 2Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulionyeshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili. 3Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. 4Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake. 5Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. 6Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: "Mtu ni nini ee Mungu, hata umfikirie; mwanaadamu ni nini hata umjali? 7Ulimfanya kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu na heshima, 8ukaweka kila kitu chini ya miguu yake, avitawale." Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. 9Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. 10Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu. 11Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao ndugu zake; 12kama asemavyo: "Ee Mungu, nitawatangazia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao." 13Tena asema: "Nitamwekea Mungu tumaini langu." Na tena: "Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu." 14Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili kwa njia ya kifo chake amwangamize Ibilisi, ambaye ana mamlaka juu ya kifo, 15na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. 16Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kwa ajili ya kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko; "Anawasaidia wazawa wa Abrahamu." 17Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. 18Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.

Chapter 3

1Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. 2Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. 3Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose. 4Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. 5Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. 6Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia. 7Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, 8msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani, 9Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini. 10Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, `Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.` 11Basi, nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."` 12Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. 13Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. 14Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni. 15Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu." 16Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. 17Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. 18Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. 19Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.

Chapter 4

1Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo. 2Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. 3Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."` Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu. 4Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: "Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote." 5Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko." 6Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata. 7Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu." 8Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine. 9Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba. 10Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake. 11Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani. 12Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu. 13Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu. 14Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe--Yesu, Mwana wa Mungu. 15Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. 16Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.

Chapter 5

1Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao. 2Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. 3Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake. 4Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni. 5Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako." 6Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki." 7Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu. 8Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso. 9Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, 10naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki. 11Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa. 12Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa. 13Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini. 14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.

Chapter 6

1Basi, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa na kuyaacha nyuma yale mafundisho ya mwanzo ya Kikristo. Hatuhitaji kuweka msingi tena kwa kurudia yale mafundisho ya mwanzo kama vile kuachana na matendo ya kifo, kumwamini Mungu; 2mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. 3tusonge mbele! Hayo tutayafanya, Mungu akitujalia. 4Maana watu wanaoiasi imani yao inawezekanaje kuwarudisha watubu tena? Watu hao walikwisha kuwa katika mwanga wa Mungu, walikwisha onja zawadi ya mbinguni na kushirikishwa Roho Mtakatifu; 5walikwisha onja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, 6kisha wakaiasi imani yao! Haiwezekani kuwarudisha watubu tena, kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu na kumwaibisha hadharani. 7Mungu huibariki ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima. 8Lakini kama ardhi hiyo ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto. 9Lakini, ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tunalo tumaini kubwa juu ya hali yenu. Tunajua kwamba mmepokea baraka zile bora za wokovu wenu. 10Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. 11Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. 12Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu na hivyo wanapokea yake aliyoahidi Mungu. 13Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa. 14Mungu alisema: "Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi." 15Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo alipokea kile alichoahidiwa na Mungu. 16Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu zaidi kuliko wao, na kiapo hicho husuluhisha ubishi wote. 17Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonyesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake. 18Basi, kuna vitu hivi viwili: ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu. 19Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo ni imara na thabiti, nalo lapenya lile pazia la hekalu la mbinguni mpaka patakatifu ndani. 20Yesu ametangulia kuingia humo kwa niaba yetu, na amekuwa kuhani mkuu milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

Chapter 7

1Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki, 2naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni "Mfalme wa Uadilifu"; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya "Mfalme wa Amani.") 3Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima. 4Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani. 5Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu. 6Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. 7Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa. 8Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. 9Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. 10Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye. 11Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni. 12Maana ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike. 13Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani. 14Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani. 15Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea. 16Yeye hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho. 17Maana Maandiko yasema: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki." 18Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu. 19Maana Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu. 20Zaidi ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo. 21Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: "Bwana ameapa, wala hataigeuza nia yake: `Wewe ni kuhani milele."` 22Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. 23Kuna tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao. 24Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. 25Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu. 26Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni. 27Yeye si kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote. 28Sheria ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.

Chapter 8

1Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni. 2Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu. ic 3Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea. 4Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria. 5Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: "Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani." 6Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi. 7Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili. 8Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda. 9Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana. 10Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. 11Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: `Mjue Bwana.` Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi. 12Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao." 13Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.

Chapter 9

1Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada palipojengwa na watu. 2Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu. 3Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote. 4Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano. 5Juu ya hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo. 6Mipango hiyo ilitekelezwa kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao. 7Lakini kuhani Mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka. Anapoingia ndani huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi ambazo watu wamezitenda bila wao wenyewe kujua. 8Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu haijafunguliwa. 9Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa. Linaonyesha kwamba zawadi na dhabihu zinazotolewa kwa Mungu haziwezi kuifanya mioyo ya wale wanaoabudu kuwa mikamilifu, 10kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote. 11Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa Kuhani Mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa. 12Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, tena hakuwa amechukua damu ya mbuzi wala ng`ombe, bali aliingia kwa damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele. 13Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng`ombe pamoja na majivu ya ndama. 14Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu za Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai. 15Kwa hiyo, Kristo ndiye aliyeratibisha agano jipya ili wale walioitwa na Mungu wazipokee baraka za milele walizoahidiwa. Watazipata, kwani kifo kimetokea ambacho huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale. 16Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa. 17Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi. 18Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa. 19Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu wote. 20Mose alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii." 21Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada. 22Naam, kadiri ya Sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa. 23Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji dhabihu iliyo bora zaidi. 24Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu. 25Kuhani Mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa amechukua damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi, 26maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu, kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu. 27Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu, 28vivyo hivyo Kristo naye alijitoa dhabihu mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.

Chapter 10

1Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu? 2Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma. 3Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. 4Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. 5Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. 6Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. 7Hapo nikasema: `Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."` 8Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria. 9Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja. 10Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha. 11Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi. 12Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu. 13Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake. 14Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao. 15Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: 16"Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao." 17Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu." 18Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi. 19Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu. 20Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe. 21Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. 22Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi. 23Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu. 24Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. 25Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia. 26Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi. 27Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga. 28Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu. 29Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani? 30Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake." 31Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno! 32Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili. 33Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo. 34Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang`anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele. 35Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa. 36Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi. 37Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia. 38Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye." 39Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.

Chapter 11

1Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona. 2Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao. 3Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana. 4Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyokuwa bora zaidi kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa amekufa, bado ananena. 5Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu. 6Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta. 7Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hakuweza kuyaona bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani. 8Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. 9Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. 10Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga. 11Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri. 12Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani. 13Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani. 14Watu wanaosema mambo kama hayo, huonyesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe. 15Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndiyo maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji. 17Kwa imani, Abrahamu alimtoa mwanae Isaka sadaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanae wa pekee, 18ingawa Mungu alikuwa amemwambia: "Wazawa wako watatokana na Isaka." 19Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu: na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanae kutoka wafu. 20Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye. 21Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea ile fimbo yake. 22Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake. 23Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. 24Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo. 26Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Masiha kuna faida kubwa zaidi kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye. 27Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana. 28Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli. 29Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu, kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji. 30Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kwa muda wa siku saba. 31Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi. 32Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gedeoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii. 33Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba, 34Walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga. Walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita wakashinda majeshi ya kigeni. 35Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi. 36Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani. 37Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa. 38Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na mlimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi. 39Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidia, 40maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.

Chapter 12

1Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung`ang`ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. 2Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu. 3Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. 4Maana katika kupambana na dhambi, ninyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. 5Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja ninyi kuwa wanawe? "Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. 6Maana Bwana humwadhibu kila anayempenda, humpinga kila anayekubali kuwa mwanae." 7Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea ninyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? 8Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, ninyi si wanawe, bali ni wana haramu. 9Zaidi ya hayo sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. 10Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. 11Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili! 12Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu. 13Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe. 14Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. 15Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. 16Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja. 17Ninyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi. 18Ninyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli, hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, 19mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno jingine, 20kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: "Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe." 21Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, "Naogopa na kutetemeka." 22Lakini ninyi mmefika katika mlima wa Sioni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika elfu nyingi wasiohesabika. 23Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu. 24Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli. 25Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza yeye ambaye anasema nanyi. Kama wale walikataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni? 26Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: "Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu." 27Neno hili: "tena" linatuonyesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa. 28Sisi basi, na tushukuru kwani tunapokea utawala usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu; 29maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.

Chapter 13

1Endeleeni kupendana kidugu. 2Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua. 3Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao. 4Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. 5Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: "Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa." 6Ndiyo maana tunathubutu kusema: "Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?" 7wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni ujumbe wa Mungu. Fikirieni juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao. 8Yesu Kristo ni yuleyule, jana, leo na milele. 9Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata. 10Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi, hawana haki ya kula vitu vyake. 11Kuhani Mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. 12Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. 13Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. 14Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. 15Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa na midomo inayoliungama jina lake. 16Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo dhabihu zinazompendeza Mungu. 17Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu. 18Tuombeeni na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. 19Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo. 20Mungu amemfufua Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. 21Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze mapenzi yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina. 22Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni. 23Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu. 24Wasalimieni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni. 25Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.

James

Chapter 1

1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam! 2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. 4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. 5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu. 6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. 7Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana. 8[] 9Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, 10naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. 11Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake. 12Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda. 13Kama mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. 15Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo. 16Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! 17Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. 18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake. 19Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. 20Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. 21Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu. 22Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. 23Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. 24Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. 25Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya. 26Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. 27Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.

Chapter 2

1Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. 2Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. 3Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu," 4je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya? 5Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda. 6Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani? 7Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa? 8Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa. 9Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia. 10Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote. 11Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria. 12Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. 13Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu. 14Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? 15Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. 16Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? 17Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa. 18Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. 19Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. 20Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa? 21Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu. 22Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. 23Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu." 24Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake. 25Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine. 26Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.

Chapter 3

1Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu. Kama mjuavyo, sisi walimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine. 2Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote. 3Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka. 4Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka. 5Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. ic Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa. 6Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe. 7Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote--wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. 8Lakini hakuna mtu aliyeweza kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. 9Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huohuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. 10Maneno ya laana na ya kusifia hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. 11Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? 12Ndugu zangu, je, mti wa mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu. 13Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aonyeshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima. 14Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli. 15Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani. 16Maana popote palipo na wivu na ubinafsi hapo pana fujo na kila aina ya uovu. 17Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki. 18Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.

Chapter 4

1Mapigano na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu. 2Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu. 3Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. 4Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu. 5Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: "Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa." 6Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu." 7Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni. 8Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki! 9Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa. 10Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni. 11Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu. 12Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako? 13Basi, sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida." 14Ninyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena. 15Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile." 16Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya. 17Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi.

Chapter 5

1Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni. 2Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo. 3Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Ninyi mmejilundikia mali katika siku hizi za mwisho! 4Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana, Mwenye Nguvu. 5Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6Mmemhukumu na kumwua mtu asiye na hatia, naye hakuwapigeni. 7Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. 8Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia. 9Ndugu zangu, msinung`unikiane ninyi kwa ninyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia. 10Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana. 11Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema. 12Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni "Ndiyo" kama maana yenu ni ndiyo, na "La" kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu. 13Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. 15Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa. 16Basi, ungamanianeni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi. 17Eliya alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake. 19Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha, 20fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.

1 Peter

Chapter 1

1Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia. 2Mungu Baba aliwateua ninyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele. 3Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Ametujalia tumaini lenye uzima, 4na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza au kuharibika au kufifia. 5Hizo zitakuwa zenu ninyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati. 6Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka. 7Shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu ambayo ni ya thamani zaidi kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima Siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa. 8Ninyi mnampenda ingawaje hamjamwona, na mnamwamini ingawa hamumwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka, 9kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu. 10Manabii walipeleleza kwa makini na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo ninyi mngepewa. 11Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. 12Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo ninyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu. 13Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa kwa nia, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika baraka ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! 14Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga. 15Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu. 16Maandiko yasema: "Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu." 17Mnapomtaja Mungu ninyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu. 18Maana mnajua kwamba ninyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu, si kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu; 19bali mlikombolewa kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwana kondoo asiye na dosari wala doa. 20Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21Kwa njia yake, ninyi mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu. 22Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, ninyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote. 23Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, ninyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele. 24Kama Maandiko yasemavyo: "Kila binadamu ni kama nyasi, na utukufu wake wote ni kama maua ya porini. Nyasi hunyauka na maua huanguka. 25Lakini neno la Bwana hudumu milele." Neno hilo ni hiyo Habari Njema iliyohubiriwa kwenu.

Chapter 2

1Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena. 2Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa. 3Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua kwamba Bwana ni mwema." 4Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa. 5Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. 6Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa." 7Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi." 8Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo. 9Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. 10Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea. 11Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho. 12Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake. 13Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu, 14utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema. 15Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya. 16Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme. 18Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza. 19Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili. 20Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo. 21Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake. 22Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake. 23Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki. 24Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa. 25Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.

Chapter 3

1Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, 2kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. 3Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. 4Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. 5Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. 6Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Ninyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote. 7Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uzima anayowapeni Mungu. Hapo ndipo sala zenu hazitakataliwa. 8Mwisho nasema hivi: mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kidugu, kuwa wapole na wanyenyekevu ninyi kwa ninyi. 9Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana ninyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. 10Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, anapaswa kuacha kusema mabaya na kuacha kusema uongo. 11Na ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. 12Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu." 13Ni nani atakayeweza kuwadhuru ninyi kama mkizingatia kutenda mema? 14Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. 15Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, 16lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. 17Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu. 18Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke ninyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; 19na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. 20Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa majini, 21ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa ninyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo, 22ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.

Chapter 4

1Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi. 2Tangu sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu. 3Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu. 4Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni. 5Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu wazima na wafu! 6Kwa sababu hiyo, hao waliokufa ambao walikuwa wamehukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama anavyohukumiwa kila mmoja, walihubiriwa Habari Njema kusudi katika maisha yao ya kiroho waishi kama aishivyo Mungu. 7Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na nidhamu, ili mweze kusali. 8Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi. 9Muwe na ukarimu ninyi kwa ninyi bila kunung`unika. 10Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. 11Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina. 12Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. 13Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu. 15Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni muuaji, mwizi, mhalifu au mwovu. 16Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo. 17Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu? 18Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?" 19Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.

Chapter 5

1wazee! Mimi niliye mzee ninalo ombi moja kwenu wazee wenzangu. Mimi mwenyewe nilishuhudia kwa macho yangu mateso ya Kristo na natumaini kuushiriki ule utukufu utakaofunuliwa. Mimi nawaombeni 2mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. 3Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi. 4Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, ninyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia. 5Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Ninyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu." 6Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. 7Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni. 8Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. 9Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo. 10Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni muushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara. 11Kwake uwe uwezo milele! Amina. 12Nimewaandikieni barua hii fupi kwa msaada wa Silwano, ndugu ambaye namjua na kumwamini. Nataka kuwapeni moyo na kushuhudia kwamba jambo hili ni neema ya Mungu kweli. Kaeni imara katika neema hiyo. 13Jumuiya ya wenzenu walioteuliwa na Mungu hapa Babuloni wanawasalimuni. Vilevile mwanangu Marko anawasalimuni. 14Salimianeni kwa ishara ya upendo wa Kikristo. Nawatakieni amani ninyi mlio wake Kristo.

2 Peter

Chapter 1

1Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi. 2Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. 3Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. 4Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu. 5Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu, 6kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu, 7udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu. 8Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani. 10Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe. 11Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. 12Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea. 13Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya. 14Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi. 15Basi, nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya kufariki kwangu. 16Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe. 17Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye." 18Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu. 19Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong`ara mioyoni mwenu. 20Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu. 21Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Chapter 2

1Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo walimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe. 2Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, kwa sababu yao, wengine wataipuuza Njia ya ukweli. 3Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yu tayari, na Mwangamizi wao yu macho! 4Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea Siku ile ya Hukumu. 5Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba. 6Mungu aliadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu. 7Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi. 8Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu. 9Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi Siku ile ya hukumu, 10hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni washupavu na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. 11Lakini malaika, ambao wana uwezo na nguvu zaidi kuliko hao walimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana. 12Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili, ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe, 13na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, bali wakifurahia njia zao za udanganyifu. 14Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu! 15Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori, ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu, 16akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii. 17Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu. 18Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu. 19Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu--maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala. 20Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali. 21Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kujua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea. 22Ipo mithali isemayo: "Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe," na nyingine isemayo: "Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!" Ndivyo ilivyo kwao sasa.

Chapter 3

1Wapenzi wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya. 2Napenda mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa na mitume wenu. 3Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki ninyi 4na kusema: "Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!" 5Watu hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na nchi zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji; 6na kwa maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa. 7Lakini mbingu na nchi za sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya Siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa. 8Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja. 9Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu. 10Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake. 11Maadamu kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, ninyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani? Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu, 12mkiingojea Siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi--Siku ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa joto. 13Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu. 14Kwa hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnangojea Siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye. 15Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa, kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na Mungu. 16Hayo ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga, wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe. 17Lakini ninyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara. 18Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.

1 John

Chapter 1

1Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. 2Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. 3Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. 4Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike. 5Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. 6Tukisema kwamba tuna umoja naye,na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo. 7Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. 8Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu. 9Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote. 10Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.

Chapter 2

1Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa. 2Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote. 3Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua. 4Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. 5Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye: 6mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo. 7Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia. 8Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa ukweli umekwisha anza kuangaza. 9Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani. 10Yeyote ampendaye ndugu yake, yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine. 11Lakini anayemchukia ndugu yake, yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha. 12Ninawaandikieni ninyi watoto, kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo. 13Nawaandikieni ninyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo, Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu. 14Nawaandikieni ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni ninyi kina baba, kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mmemshinda yule Mwovu. 15Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake. 16Vitu vyote vya ulimwengu-tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali-vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu. 17Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele. 18Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba adui wa Kristo anakuja, na sasa adui wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu. 19Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; Kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu. 20Ninyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli. 21Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamuujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli. 22Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha. Mtu wa namna hiyo ni adui wa Kristo--anamkana Baba na Mwana. 23Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia. 24Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba. 25Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uzima wa milele. 26Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha ninyi. 27Lakini, kwa upande wenu ninyi, Kristo aliwamiminieni Roho wake. Na kama akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana Roho wake anawafundisheni kila kitu na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo. 28Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu Siku ya kuja kwake. 29Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu.

Chapter 3

1Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu. 2Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. 3Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa. 4Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. 5Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. 6Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo. 7Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. 8Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi. 9Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. 10Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi. 11Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana! 12Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema! 13Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi. 14Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. 15Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake. 16Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. 17Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? 18Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo. 19Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. 20Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. 21Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu, 22na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza. 23Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. 24Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.

Chapter 4

1Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, Maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. 2Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu. 3Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa Adui wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni! 4Lakini ninyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu zaidi kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu. 5Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu. 6Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo. 7Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. 8Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. 9Na Mungu alionyesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uzima kwa njia yake. 10Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu. 11Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana. 12Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana Mungu anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu. 13Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi, kwani yeye ametupa Roho wake. 14Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu. 15Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu. 16Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye. 17Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri Siku ile ya Hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo. 18Palipo na upendo hapana uoga; naam, upendo kamili hufukuza uoga wote. Basi, mtu mwenye uoga hajakamilika bado katika upendo, kwani uoga huhusikana na adhabu. 19Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. 20Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni. 21Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda ndugu yake.

Chapter 5

1Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ni Kristo, huyo ni mtoto wa Mungu; na, anayempenda mzazi humpenda pia mtoto wa huyo mzazi. 2Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu: Kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake; 3maana kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na, amri zake si ngumu, 4maana kila aliye mtoto wa Mungu anaweza kuushinda ulimwengu. Hivi ndivyo tunavyoushinda ulimwengu: kwa imani yetu. 5Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. 6Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake. Hakuja kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Naye Roho anashuhudia kwamba ni kweli, kwani Roho ni ukweli. 7Basi, wako mashahidi watatu: 8Roho, maji na damu; na ushahidi wa hawa watatu waafikiana. 9Ikiwa twaukubali ushahidi wa binadamu, ushahidi wa Mungu una uzito zaidi; na huu ndio ushahidi alioutoa Mungu mwenyewe juu ya Mwanae. 10Anayemwamini mwana wa Mungu anao ushahidi huo ndani yake; lakini asiyemwamini Mungu, anamfanya yeye kuwa mwongo, maana hakuamini ushahidi alioutoa Mungu juu ya Mwanae. 11Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uzima wa milele, na uzima huo uko kwa Bwana. 12Yeyote, aliye na Mwana wa Mungu anao uzima huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uzima. 13Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uzima wa milele ninyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu. 14Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya mapenzi yake, yeye hutusikiliza. 15Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba atupatia yote tunayomwomba. 16Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uzima. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo. 17Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu kwenye kifo. 18Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. 19Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu. 20Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli--katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uzima wa milele. 21Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu.

2 John

Chapter 1

1Mimi Mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule, pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda ninyi, 2kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. 3Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo. 4Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru. 5Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. 6Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri niliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo. 7Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu akawa binadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni Adui wa Kristo. 8Basi, jihadharini ninyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishugulikia, bali mpate tuzo lenu kamili. 9Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana. 10Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. 11Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu. 12Ninayo mengi ya kuwaambieni lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike. 13Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.

3 John

Chapter 1

1Mimi mzee nakuandikia wewe Gayo, rafiki yangu, ninayekupenda kweli. 2Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni. 3Nimefurahi sana ndugu kadhaa walipofika hapa, wakaiambia juu ya uaminifu wako kuhusu ukweli; naam, wewe unaishi daima katika ukweli. 4Hakuna kitu kinachonifurahisha zaidi kuliko kusikia kwamba watoto wangu wanaishi katika ukweli. 5Mpenzi wangu, wewe ni mwaminifu kila mara unapowahudumia ndugu, hata kama ni wageni. 6Ndugu hao wamelieleza kanisa hapa habari za upendo wako. Tafadhali uwasaidie waendelee na safari yao kwa namna itakayompendeza Mungu, 7Maana wanaanza safari yao katika utumishi wa Kristo bila kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. 8Basi, sisi tunapaswa kuwasaidia watu hawa, ili nasi tupate kushiriki katika kazi yao kwa ajili ya ukweli. 9Niliandika barua fupi kwa hilo kanisa; lakini Diotrefe, ambaye hupenda kuwa kiongozi wao, hataki kabisa kunisikiliza. 10Basi, nitakapokuja nitayafichua mambo yote anayofanya, maneno mabaya anayotutolea na uongo anaosema juu yetu. Isitoshe, yeye hukataa kuwakaribisha hao ndugu walio safarini, na hata huwazuia watu wengine wanaotaka kuwakaribisha, na hujaribu kuwafukuzia nje ya kanisa. 11Mpenzi wangu, usifuate mfano mbaya, bali mfano mwema. Kila atendaye mema ni wa Mungu; lakini anayetenda mabaya hajapata kumwona Mungu. 12Kila mtu anamsifu Demetrio; naam, ukweli wenyewe unamsifu. Nasi pia tunatoa ushahidi wetu juu yake, nawe wajua kwamba tunachosema ni kweli. 13Ninayo bado mengi ya kukwambia, lakini sipendi kuyaandika kwa kalamu na wino. 14Natumaini kukuona karibuni na hapo tutazungumza ana kwa ana. 15Nakutakia amani. Rafiki zako wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu wote kila mmoja binafsi.

Jude

Chapter 1

1Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo. 2Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi. 3Ndugu wapenzi, wakati nimo katika jitihada ya kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, nimeona lazima ya kuwaandikieni na kuwahimizeni mwendelee kupigana kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote. 4Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake kiongozi na Bwana wetu. Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu awali hukumu inayowangojea watu hao. 5Nataka kuwakumbusheni mambo fulani ambayo mmekwisha yajua: kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe Siku ile kuu. 7Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. 8Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. 9Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi waliobishana juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi; ila alisema: "Bwana mwenyewe na akukaripie." 10Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama vile wanyama wanayoyajua ndiyo yanayowaangamiza. 11Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Baalamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. 12Kwa makelele yao yasiyo na adabu, watu hao ni kama madoa machafu katika mikutano yenu ya karamu ya Bwana. Hujipendelea wao wenyewe tu, na wako kama mawingu yanayopeperushwa huko na huko na upepo bila ya kuleta mvua. Wao ni kama miti isiyozaa matunda hata wakati wa majira yake, wamekufa kabisa. 13Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanaonekana dhahiri kama vile mapovu ya mawimbi. Wao ni kama nyota zinazotangatanga, ambao Mungu amewawekea mahali pao milele katika giza kuu. 14Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hawa: "Sikilizeni! Bwana atakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu 15kutoa hukumu juu ya binadamu wote, kuwahukumu wote kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo." 16Watu hawa wananung`unika daima na kuwalaumu watu wengine. Hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kusudi wafaulu katika mipango yao. 17Lakini ninyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali ni mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo. 18Waliwaambieni: "Siku za mwisho zitakapofika, watatokea watu watakaowadhihaki ninyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya." 19Hao ndio watu wanaosababisha mafarakano, watu wanaotawaliwa na tamaa zao za kidunia, watu wasio na Roho wa Mungu. 20Lakini ninyi, wapenzi wangu, endeleeni kujijenga kikamilifu katika imani yenu takatifu. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, 21na kubaki katika upendo wa Mungu, mkiwa mnamngojea Bwana wetu Yesu Kristo awapeni uzima wa milele kwa huruma yake. 22Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka; 23waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni; na kwa wengine muwe na huruma pamoja na hofu, lakini chukieni hata mavazi yao ambayo yamechafuliwa na tamaa zao mbaya. 24Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta ninyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, 25kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.

Revelation

Chapter 1

1Hizi ni habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu alimpa Kristo ufunuo huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe Yohane, mtumishi wake, mambo hayo, 2naye Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake kuhusu ujumbe wa Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo. 3Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza maneno ya ujumbe huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati umekaribia ambapo mambo haya yatatukia. 4Mimi Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, 5na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, 6akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. 7Tazama! Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina. 8"Mimi ni Alfa na Omega," asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja. 9Mimi ni Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki pamoja nanyi katika kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa Utawala wake. Mimi nilikuwa kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe wa Mungu na ukweli wa Yesu. 10Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. 11Nayo ilisema, "Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea." 12Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, 13na katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na ukanda wa dhahabu kifuani. 14Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; 15miguu yake iling`aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya moto na kusuguliwa, na sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la maji. 16Katika mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling`aa kama jua kali. 17Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, "Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. 18Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu. 19Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. 20Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia, na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.

Chapter 2

1"Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono wake wa kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu. 2Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo. 3Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. 4Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. 5Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukayaache madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake. 6Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi. 7"Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya mti wa uzima ulioko ndani ya bustani ya Mungu. 8"Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikufa na akaishi tena. 9Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani. 10Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uzima. 11"Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili. 12"Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi: "Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili. 13Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani. 14Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi. 15Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu. 17"Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! "Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika. Nitawapa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea. 18"Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: "Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang`aa kama shaba iliyosuguliwa. 19Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali. 20Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule mwanamke Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu. 21Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki kuachana na uzinzi wake. 22Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya hivyo, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye. 23Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu. 24"Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita `Siri ya Shetani`, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine. 25Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja. 26"Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho kutenda ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa. Naam, nitawapa uwezo uleule nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na kuyavunjavunja kama chombo cha udongo. Tena nitawapa nyota ya asubuhi. 27[] 28[] 29"Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

Chapter 3

1"Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye na roho saba za Mungu na nyota saba. Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa! 2Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni makamilifu mbele ya Mungu wangu. 3Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii na ubadili nia yako mbaya. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia. 4Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe. 5"Wale wanaoshinda, watavikwa mavazi meupe kama hao. Nami sitayafuta majina yao kutoka katika kitabu cha uzima; tena nitawakiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake. 6"Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa! 7"Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, ambaye anao ule ufunguo wa Daudi, na ambaye hufungua na hakuna mtu awezaye kufungua. 8Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umezishika amri zangu, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu. 9Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe ni wadanganyifu. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako wapate kujua kwamba kweli nakupenda wewe. 10Kwa kuwa wewe umezingatia agizo langu la kuwa na uvumilivu, nami pia nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima kuwajaribu wote wanaoishi duniani. 11Naja kwako upesi! Linda, basi, ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang`anywa na mtu yeyote taji yako ya ushindi. 12"Wale wanaoshinda nitawafanya wawe minara katika Hekalu la Mungu wangu, na hawatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yao jina langu jipya. 13"Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa! 14"Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: "Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aitwaye `Amina`. Yeye ni shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu. 15Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto. 16Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! 17Wewe unajisema, `Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote.` Kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi! 18Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona. 19Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo kaza moyo, achana na dhambi zako. 20Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami. 21"Wale wanaoshinda nitawaketisha pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi. 22"Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!"

Chapter 4

1Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya tarumbeta, ikasema, "Njoo hapa juu nami nitakuonyesha mambo yatakayotukia baadaye." 2Mara nikachukuliwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake ameketi mmoja. 3Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua ulikuwa unang`aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote. 4Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani. 5Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za Mungu. 6Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe linga`aalo sana. Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kilikuwa na viumbe hai vinne. Viumbe hivyo vilikuwa vimejaa macho mbele na nyuma. 7Kiumbe cha kwanza kulikuwa kama simba, cha pili kama ng`ombe, cha tatu kilikuwa na sura kama mtu, na cha nne kilikuwa kama tai anayeruka. 8Viumbe hivyo vinne vilikuwa na mabawa sita kila kimoja, na vilikuwa vimejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika huimba: "Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana, Mungu Mwenye Uwezo, aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!" 9Kila mara viumbe vinne vilipoimba nyimbo za kumtukuza, kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, ambaye anaishi milele na milele, 10wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema: 11"Wewe ni Bwana na Mungu wetu, unastahili utukufu na heshima na nguvu; maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako kila kitu kimepewa uhai na uzima."

Chapter 5

1Kisha katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nikaona kitabu; nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na mihuri saba. 2Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: "Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?" 3Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini Kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani. 4Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani. 5Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, "Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu." 6Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo amesimama, akizungukwa kila upande na vile viumbe hai vinne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani. 7Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. 8Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja, alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu. 9Basi, wakaimba wimbo huu mpya: "Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa. 10Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu nao watatawala duniani." 11Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, vile viumbe hai vinne na wale wazee; 12wakasema kwa sauti kuu: "Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa." 13Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na baharini--viumbe vyote ulimwenguni--vikisema: "Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele na milele." 14Na vile viumbe vinne hai vikasema, "Amina!" Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.

Chapter 6

1Kisha nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia kimoja cha vile viumbe hai vinne kikisema kwa sauti kama ya ngurumo, "Njoo!" 2Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpanda farasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi aendelee kushinda. 3Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, "Njoo!" 4Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpanda farasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, akapewa upanga mkubwa. 5Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, "Njoo!" Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpanda farasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. 6Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa vile viumbe hai vinne. Nayo ilisema, "Kibaba kimoja cha unga wa ngano wa kiasi cha fedha dinari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa dinari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!" 7Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, "Njoo!" 8Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpanda farasi wake lilikuwa kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia. 9Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa. 10Basi, wakalia kwa sauti kubwa: "Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?" 11Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watawaua kama wao wenyewe walivyouawa. 12Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; 13nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. 15Kisha wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye majabali milimani. 16Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, "Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! 17Maana siku maalum ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?"

Chapter 7

1Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti. 2Kisha nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari, 3"Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso." 4Kisha nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu mia moja arobaini na nne elfu wa makabila yote ya watu wa Israeli. 5Kabila la Yuda walikuwa watu kumi na mbili elfu; kabila la Reubeni, kumi na mbili elfu, kabila la Gadi, kumi na mbili elfu; 6Kabila la Asheri, kumi na mbili elfu; kabila la Naftali, kumi na mbili elfu; kabila la Manase, kumi na mbili elfu; 7kabila la Simeoni, kumi na mbili elfu, kabila la Lawi, kumi na mbili elfu, kabila la Isakari, kumi na mbili elfu; 8kabila la Zabuloni, kumi na mbili elfu; kabila la Yosefu, kumi na mbili elfu, na kabila la Benyamini, kumi na mbili elfu. 9Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. 10Wakapaaza sauti: "Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!" 11Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na vile viumbe hai vinne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu, 12wakisema, "Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!" 13Mmoja wa hao wazee akaniuliza, "Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?" 14Nami nikamjibu, "Mheshimiwa, wewe wajua!" Naye akaniambia, "Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa. 15Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika Hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. 16Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena, 17kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao."

Chapter 8

1Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa. 2Kisha nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba. 3Malaika mwingine akafika, akiwa anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi. 4Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu. 5Kisha malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi. 6Kisha wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo. ic 7Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto, pamoja na damu, ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua, na majani yote mabichi yakaungua. 8Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto ukatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu, 9theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa na theluthi moja ya meli zikaharibiwa. 10Kisha malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto, ikaanguka kutoka mbinguni, na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji. 11(Nyota hiyo inaitwa "Uchungu.") Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu. 12Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng`ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku. 13Kisha nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani anasema kwa sauti kubwa, "Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!"

Chapter 9

1Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu. 2Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu. 3Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng`e. 4Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. 5Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng`e. 6Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia. 7Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. 8Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. 9Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. 10Walikuwa na mikia na miiba kama ng`e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. 11Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi. 12Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata. 13Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. 14Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa `Eufrate!"` 15Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu. 16Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili. 17Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao. 18Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; 19maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu. 20Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. 21Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.

Chapter 10

1Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto. 2Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu, 3na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo. 4Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!" 5Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni, 6akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha! 7Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii." 8Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu." 9Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!" 10Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu. 11Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"

Chapter 11

1Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa, "Inuka, ukalipime Hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani, na ukawahesabu watu wanaoabudu ndani ya Hekalu. 2Lakini uache ukumbi ulio nje ya Hekalu; usiupime, maana huo umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyanga mji Mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 3Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watangaze ujumbe wa Mungu kwa muda huo wa siku elfu moja mia mbili na sitini wakiwa wamevaa mavazi ya magunia." 4Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya Mizeituni na taa mbili zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia. 5Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na kuwaangamiza adui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna hiyo. 6Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotangaza ujumbe wa Mungu. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wapendavyo. 7Lakini wakisha maliza kutangaza ujumbe huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua. 8Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa; jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri. 9Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe. 10Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia. 11Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. 12Kisha hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, "Njoni hapa juu!" Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui wao wakiwa wanawatazama. 13Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu elfu saba wakauawa kwa tetemeko hilo la ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni. 14Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata hima. 15Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, "Sasa utawala juu ya ulimwengu ni wa Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!" 16Kisha wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, 17wakisema: "Bwana Mungu Mwenye uwezo, uliyeko na uliyekuwako! Tunakushukuru, maana umetumia nguvu yako kuu ukaanza kutawala! 18Watu wa mataifa waliwaka hasira, maana wakati wa ghadhabu yako umefika, wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii, watu wako na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo. Ni wakati wa kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia." 19Hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kisha kukatokea umeme, sauti, ngurumo, tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.

Chapter 12

1Kisha ishara kubwa ikaonekana mbinguni. Palikuwa hapo mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake! 2Alikuwa mja mzito, na akapaaza sauti kwa maumivu na uchungu wa kujifungua mtoto. 3Ishara nyingine ikatokea mbinguni: joka kubwa jekundu na lenye pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji. 4Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa. 5Kisha mama huyo akajifungua mtoto wa kiume, ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi. 6Huyo mama akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini. 7Kisha kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake. 8Lakini joka hilo halikuweza kuwashinda, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika wake. 9Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani. Ndiye anayeudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye. 10Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: "Sasa ukombozi utokao kwa Mungu umefika! Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika. Na Kristo wake ameonyesha mamlaka yake! Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu, aliyesimama mbele ya Mungu akiwashtaki usiku na mchana, sasa ametupwa nje. 11Ndugu zetu wameshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa. 12Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba siku zake zilizobakia ni chache." 13Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume. 14Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali, pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu. 15Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue. 16Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka. 17Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kuuzingatia ukweli wa Yesu. 18Na likajisimamia ukingoni mwa bahari.

Chapter 13

1Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa limeandikwa juu ya vichwa hivyo. 2Mnyama huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake ilikuwa kama ya dubu, na kinywa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu yake, kiti chake cha enzi na uwezo mkuu. 3Kichwa kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha jeruhiwa vibaya sana, lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima ilishangazwa na huyo mnyama na kumfuata. 4Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, "Nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?" 5Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 6Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake, na wote wakaao mbinguni. 7Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa mamlaka juu ya watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa. 8Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo aliyechinjwa. 9"Aliye na masikio, na asikie! 10Waliokusudiwa kuchukuliwa mateka lazima watatekwa; waliokusudiwa kuuawa kwa upanga lazima watauawa kwa upanga. Kutokana na hayo ni lazima watu wa Mungu wawe na uvumilivu na imani." 11Kisha nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka. 12Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona. 13Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu. 14Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena. 15Kisha alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa kwanza, hata ikaweza kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu. 16Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu huru na watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji za nyuso zao. 17Akapiga marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu mtu aliyetiwa alama hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina hilo. 18Hapa ni lazima kutumia ujasiri! Mwenye akili anaweza kufafanua maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya mtu fulani. Tarakimu hiyo ni mia sita sitini na sita.

Chapter 14

1Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake. 2Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama sauti ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao. 3Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa duniani. 4Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. 5Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote. 6Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi zote. 7Akasema kwa sauti kubwa, "Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi, bahari na chemchemi za maji." 8Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, "Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake--divai kali ya uzinzi wake!" 9Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, "Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake, 10yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu, ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo. 11Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana." 12Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu. 13Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, "Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana." Naye Roho asema, "Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata." 14Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake. 15Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, "Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva." 16Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa. 17Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali. 18Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, "Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!" 19Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu. 20Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita mia tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.

Chapter 15

1Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa. 2Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. 3Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo: "Bwana Mungu Mwenye Uwezo, matendo yako ni makuu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! 4Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yameonekana na wote." 5Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu. 6Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo Hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung`aa, na kanda za dhahabu vifuani mwao. 7Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. 8Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa makubwa saba ya wale malaika saba.

Chapter 16

1Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, "Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani." 2Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake. 3Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa. 4Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu. 5Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, "Ewe mtakatifu, Uliyeko na uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii uliyotoa. 6Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!" 7Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, "Naam, Bwana Mungu Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!" 8Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake. 9Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na kumtukuza Mungu. 10Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu za maumivu, 11wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya. 12Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa ajili ya wafalme wa mashariki. 13Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule nabii wa uongo. 14Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita kuu Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo. 15"Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu." 16Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni. 17Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, "Mwisho umefika!" 18Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu. 19Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu. 20Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena. 21Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.

Chapter 17

1Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, "Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi. 2Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake." 3Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake. 5Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo "Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani." 6Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno. 7Lakini malaika akaniambia, "Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi. 8Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena! 9"Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba. 10Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi. 11Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa. 12"Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. 13Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote. 14Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme." 15Malaika akaniambia pia, "Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha. 16Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. 17Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia. 18"Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala wafalme wa dunia."

Chapter 18

1Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng`ao wake. 2Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, "Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno. 3Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo." 4Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, "Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake. 5Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake. 6Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni. 7Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: `Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!` 8Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo." 9Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea. 10Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, "Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata." 11Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao; 12hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari; 13mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng`ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu. 14Wafanyabiashara wanamwambia: "Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!" 15Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza, 16wakisema, "Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu! 17Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!" Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali, 18na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: "Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!" 19Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: "Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!" 20Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi! 21Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, "Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa. 22Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako. 23Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!" 24Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani.

Chapter 19

1Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, "Haleluya! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu! 2Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!" 3Wakasema, "Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!" 4Na wale wazee ishirini na wanne, na vile viumbe hai vinne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, "Amina! Asifiwe Mungu!" 5Kisha kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: "Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa." 6Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, "Haleluya! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Uwezo ni Mfalme! 7Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa arusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. 8Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung`aa!" (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watu wa Mungu.) 9Kisha malaika akaniambia, "Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!" Tena akaniambia, "Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu." 10Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunauzingatia ukweli ule alioufunua Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ukweli alioufunua Yesu ndio unaowaangazia manabii." 11Kisha nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpanda farasi wake aliitwa "Mwaminifu" na "Kweli". Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki. 12Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe. 13Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni "Neno la Mungu." 14Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na walikuwa wamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi. 15Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye Uwezo. 16Juu ya vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina: "Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana." 17Kisha nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaaza sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, "Njoni! Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu. 18Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye nguvu, ya farasi na wapanda farasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu wote: walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa." 19Kisha nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya farasi, pamoja na jeshi lake. 20Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka, pamoja na nabii wa uongo aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa wameiabudu sanamu yake.) Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti. 21Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao.

Chapter 20

1Kisha nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2Akalikamata lile joka--nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani--akalifunga kwa muda wa miaka elfu moja. 3Malaika akalitupa Kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka elfu moja itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu. 4Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumtangaza Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa muda wa miaka elfu moja. 5(Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka elfu moja itimie.) Huu ndio ufufuo wa kwanza. 6Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja. 7Wakati miaka elfu mia moja itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake. 8Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani. 9Walitawanyika katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watu wa Mungu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza. 10Ibilisi, aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele. 11Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena. 12Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uzima, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo. 13Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; kifo na kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake. 14Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili. 15Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.

Chapter 21

1Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuweko tena. 2Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe. 3Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, "Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao. 4Yeye atayafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!" 5Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, "Tazama, nafanya yote mapya." Tena akaniambia, "Andika hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!" 6Kisha akaniambia, "Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima. 7Yeyote atakayeshinda atapokea hiki, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili." 9Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, "Njoo! Mimi nitakuonyesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!" 10Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionyesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni, 11uking`aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo. 12Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na malaika wanangojea kumi na wawili. Majina ya wangoja milango kumi na mawili ya Israeli yalikuwa yameandikwa juu ya milango hiyo. 13Kila upande ulikuwa na milango mitatu: upande wa mashariki, milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu. 14Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya mawe hayo yalikuwa yameandikwa majina na mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo. 15Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake. 16Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: ulikuwa na urefu, upana na urefu wa kwenda juu, kama kilomita elfu mbili na mia nne. 17Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita sitini kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia. 18Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. 19Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili yakuti samawati, la tatu kalkedoni, la nne zamaradi, 20la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarijadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasinto, na la kumi na mbili amethisto. 21Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. 22Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Uwezo na yule Mwanakondoo ndio Hekalu lake. 23Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo. 24Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake, na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao. 25Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo. 26Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani. 27Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.

Chapter 22

1Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. 3Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. 4Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. 5Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele. 6Kisha malaika akaniambia, "Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde. 7"Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki." 8Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. 9Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!" 10Tena akaniambia, "Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. 11Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu." 12"Sikiliza!" Asema Yesu, "Naja upesi, pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. 13Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho." 14Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya kula tunda la mti wa uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. 15Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji. 16"Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!" 17Roho na Bibiarusi waseme, "Njoo!" Kila mtu asikiaye hili, na aseme,"Njoo!" Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yoyote. 18Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang`anya sehemu yake katika ule mti wa uzima, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. 20Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: "Naam! Naja upesi." Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu! 21Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen.

VIEWNAME is workSection